Ijumaa, 19 Desemba 2014

MWALIMU WA MADRASAT AMPA MIMBA MWANAFUNZI, ATUPWA JELA MIAKA 7



M
walimu wa Chuo cha Madrasa kilichopo Chake Chake, Pemba, Said Khamis Salum (31) ameanza kutumikia chuo cha mafunzo jela miaka 7 baada ya kutiwa hatiani kwa kumpa ujauzito mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka 15 jina (linahifadhiwa).

Mwendesha Mashtaka wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Bilali aliiambia Mahakama ya Chake Chake mbele ya hakimu, Khamis Ramadhan Abdalla kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo miezi mitatu iliyopita .

Bilali alisema mashahidi watano waliitwa mbele ya Mahakama na kukiri kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo. Alisema baada ya uchunguzi wa vinasaba ( DNA), uliofanywa Tanzania Bara ulionesha kwamba kwa asilimia 96 mtuhumiwa ndiye aliyempa ujauzito mwanafunzi huyo.

Hakimu Abdalla alisema ameridhishwa na ushahidi wote, ikiwemo ule wa kitaalamu wa vinasaba wa DNA, uliofanywa na wataalamu kutoka Tanzania Bara, unaoonesha kwamba ni kweli mtuhumiwa alitenda kosa hilo.

Alisema mtuhumiwa atatumikia chuo cha mafunzo jela miaka saba, na atakapotoka atalazimika kulipa fidia ya sh.milioni moja ikiwa ni fundisho kwa wengine kuacha kufanya vitendo hivyo vya udhalilishaji wa wanafunzi wa vyuo vya madrasa.

“Nimeridhishwa na mazingira ya makosa haya kwa mtuhumiwa na kubaini kwamba ni kweli amempa ujauzito mwanafunzi wake wa chuo, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema Adalla.

Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea, alikana kosa hilo na kusema anahisi kwamba alipitiwa na kurubuniwa na adui shetani, ambaye ndiye aliyemshawishi kufanya hivyo.

Hivi karibuni, akizindua kampeni ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alikemea tabia ya baadhi ya walimu wa vyuo vya madrasa kuwafanyia ukatili wa kijinsia wanafunzi wao na wengine kuwapa ujauzito.

CHANZO: HABARILEO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni