Jumatano, 31 Januari 2018

UDANGANYIFU WATAWALA VYUMBA VYA MITIHANI


Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne  uliofanyika mwaka 2017 ambapo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 7.22 huku vitendo vya udanganyifu vikiongezeka ukilinganisha na mwaka 2016.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Charles Msonde ametangaza matokeo hayo leo jijini Dar es Salaam ambapo amesema ufaulu wa mtihani huo ni asilimia 77.09 ukilinganishwa na asilimia 70.68 ya mwaka 2016.

“Jumla ya watahiniwa 287,713 ambao ni sawa na asilimia 77.09 wamefaulu mitihani ya kidato cha nne 2017 (Wanafunzi wa shule na kujitegemea) ambao katika hao wasichana wapo 143,728 sawa na 75.21% wakati wavulana wapo 143,985 sawa na asilimia 79.06%. 

"Mwaka jana wanafunzi waliofaulu mtihani ya kidato cha nne walikuwa 277,283 ambao ni sawa na 70.09% hivyo ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 7.22”, amesema Dkt. Msonde.

Watahiniwa waliojiandikisha kufanya mtihani huo walikuwa 385,767 huku 323,332 walikuwa watahiniwa shule na 62,435 wa kujitegemea. Watahiniwa  wa shule 317,177 ambao ni sawa 98.28% ndio waliofanikiwa kufanya mtihani na wale wa kujitegeme 57,133 ambao sawa na 91.57% walifanya mtihani huo.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa shule zinazomilikiwa na watu binafsi zimefanya vizuri na kushika nafasi 10 za mwanzo na kuzipita kwa mbali shule za serikali. 

Shule ya kwanza ni St. Francis Girls ya mkoani Mbeya, Feza Boys (Dar es Salaam), Kemebos (Kagera), Bethel Sabs Girls (Iringa), Anwarite (Kilimanjaro), Marian Girls (Pwani), Canossa (Dar es Salaam), Feza Girls (Dar es Salaam), Marian Boys (Pwani), Shamsiye (Dar es Salaam).

Shule kumi za mwisho ni Kusini (Kusini Unguja),  Pwani Mchangani  (Kaskazini Unguja), Mwenge SMZ, Langoni (Mjini Magharibi), Furaha (Dar es Salaam), Mbesa (Ruvuma), Kabugaro (Kagera), Chokocho (Kusini Pemba), Nyeburu (Dar es Salaam) na Mtule (Kusini Unguja).

Mwanafunzi Ferson Mdee kutoka shule ya sekondari ya Marian Boys  ameongoza kwa ufaulu na kushika nafasi ya kwanza kitaifa.


Vitendo vya udanganyifu vyatawala

Licha ya ufaulu kuongezeka kwa mwaka 2017 lakini ulitawaliwa na vitendo vya udangajifu vilivyofanywa na baadhi ya wanafunzi  katika mtihani huo ikiwemo kuingia na simu kwenye vyumba vya mitihani, majibu,

Dkt. Msonde anasema, “Watahiniwa wetu 265 walibainika pasi na shaka kufanya udangajifu katika mitihani hii.  Wapo watahiniwa 123 waliokamatwa na simu, notes, vitabu ama kwa ujumla wake vitu visivyohitajika ndani  ya vyumba vya mitihani wakati akiendelea”,

“Wako pia watahiniwa 62 ambao walikuwa wanabadilishana script, walikuwa wanabadilishana namba na wengine kubainika kuwa na miandiko tofauti kwenye script zao. Watahiniwa 73 waliobainika kuwa na majibu ya kukosa yasiyo ya kawaida yenye mfanano usio wa kawaida”.

Amesema walikuwepo watahiniwa wengine ambao walifanyiwa mitihani na watu wengine ambao hawakuandikishwa kufanya mtihani, lakini walikamatwa kwa sababu kila mtahiniwa ana picha inayomtambulisha.

“Tulikuwa na watahiniwa wengine saba waliokuwa wakifanyiwa mitihani na watu wengine mamluki wengine wako nyumbani lakini wamekodi watu wakafanyie mitihani yao. 

Watahiniwa wanapofanya mitahani kuna picha zao ziko pale kwa hiyo ukimleta mtu mwingine ambaye hafananii, hawa walikamatwa na wasimamizi”, amesema Dkt. Msonde.

Akitoa mfano wa udanganyifu uliofanyika katika baadhi ya vituo amesema, “Katika shule ya Alfarik Seminary hiki ni kituo kiko Dar es Salaam mtu anayejiita Zuberi Mabula alikamatwa na msimamizi ndani ya chumba cha mtihani akimfanyia mtahiniwa Silvanus Prince Mjengwa”.

Anabainisha kuwa yapo baadhi ya matukio yamejitokeza mwaka huu hayajawahi kujitokeza wakati mwingine wowote ambapo ameshangazwa na ujasiri wa watuhumiwa hao.

“Watahiniwa mwaka huu walianzisha kitu ambacho sio cha kawaida watu wanapanga utaratibu wa kwenda kuwafanyia mitihani watu wengine lakini wanajiorodhesha na wenyewe kwenda kufanya mitihani”,

“ Kwa hiyo tumefikia hapo, tulikuwa na kundi la watahiniwa 27 wa kituo cha Mwalasi walijiandikisha kufanya mitihani katika jozi na walipoingia kwenye chumba cha mtihani mmoja anaandika namba ya mwenzie anayemfanyia mitihani na yule anayefanyiwa mtihani anaandika ya mwingine”, amesema Dkt. Msonde.

Baraza hilo limewafutia matokeo 265 kwa udangajifu huo ambapo 136 ni wale wa kujitegemea na 129 wa shule.

Jumanne, 23 Januari 2018

'SCORPION' ALIYEMTOBOA MACHO SAID MRISHO,JELA MIAKA SABA NA KULIPA FAINI MILIONI 30



Mahakama ya Wilaya ya  Ilala imemhukumu Salum Njwete maarufu kwa jina la ‘Scorpion’ kifungo cha miaka saba na kulipa fidia ya milioni 30 kwa kosa la kujeruhi na wizi wa kutumia silaha. 

Hukumu hiyo imesomwa mbele ya Hakimu, Flora Haule ambapo imemkuta na hatia ya kujeruhi ikiwemo kumtoboa macho kinyozi Said Mrisho na unyang’anyi wa kutumia silaha.

 Hapo awali mahakama ilimfutia Salum kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya upande wa mashtaka kuomba shtaka hilo liondolewe mahakamani kwasababu hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo. 

Kutokana na maombi hayo, Hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, Adelf Sachore alikubaliana na ombi hilo kwa kuzingatia kifungu namba 91 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ambacho kinampa Mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuondoa shtaka mahakamani muda wowote ili mradi kama kesi hiyo haijatolewa hukumu. 

Kifungu hicho pia kinampa Mamlaka DPP kumshtaki upya mshtakiwa huyo kama ana nia ya kuendesha shtaka hilo. 

Upande wa mashtaka ulifungua kesi mpya  yenye mashtaka mawili ambapo kesi hiyo ilihamishiwa kwa Hakimu Flora Haule ambaye leo ametoa huku hiyo ya kifungo cha miaka saba na faini ya milioni 30 kwa mshtakiwa ambapo anapaswa kulipa haraka iwezekanavyo. 

Kesi hiyo iliipata umaarufu ikizingatiwa kuwa mshtakiwa ‘Scorpion’ ni mwalimu wa Sanaa ya kujihami, 'Martial arts', msanii wa filamu za maagizo na mshindi wa shindano la Dume Challenge mwaka 2012. 

Katika kesi hiyo, Njwete alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni unyang’anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi Said Mrisho kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili zikiwemo, tumboni na mabegani na kisha kumtoboa macho na kumsababishia upofu, kitendo anachodaiwa kutenda Septemba 6, mwaka 2016 katika eneo la Buguruni Sheli, jijini Dar es Salaam. 

Pia anadaiwa alifanya tukio la unyang’anyi ambapo aliiba cheni ya Silva yenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, simu ya mkononi na fedha taslimu Shilingi 330,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh 474,000 mali ya Said Mrisho.
 Kufuatia tukio hilo  Said Mrisho ambaye mpaka sasa hana uwezo wa kuona baada ya kutobolewa macho yake yote mawili ameamriwa na mahakama kulipwa faini ya milioni 30  kama namna ya fidia.  

Hakimu Haule amesema katika hukumu hiyo Mahakama ilijikita sehemu kuu tatu ikiwemo kama mlalamikaji, Said Mrisho  amepata majeraha ya hatari pamoja na kama Scorpion alitumia unyang’anyi wa kutumia silaha. 

Pia Hakimu alitoa ruhusa kwa mtu yoyete ambaye hajaridhika na hukumu hiyo kukata rufaa. 

“Faini ilipwe wakati unatumikia kifungo, pia ni ruksa kukata rufaa kwa upande wowote kama haujaridhika,” amesema, Hakimu  Flora Haule. 

Hata hivyo Said Mrisho ameonekana kutoridhishwa na hukumu hiyo ya miaka 7 na kusema ni ndogo hivyo atapeleka ombi lake kwa Rais John Magufuli. 

“Hiyo milioni 30 ni ndogo sana, na kwahiyo miaka saba ni hukumu ndogo sana. Yaani inaniumiza sana na watoto wangu sifikirii nitafanya nini kwasababu sina ubunifu wa kufanya chochote nikiwa katika mazingira haya”, amesema Said Mrisho wakati akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya hukumu hiyo kusomwa.

 
“Kwa hili sidhani kama nitaishia hapa, nitafika kwa Mhe. Rais, nitafika kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa nitawaeleza kwa hili siwezi kukubaliana nao wameniharibia maisha sana".
 Salum Njwete,maarufu kwa jina la  "Scorpion" akiwa mokononi mwa dola


Jumamosi, 13 Januari 2018

UTAFITI: WANAOJIPIGA 'SELFIE' HATARINI KUPATA MAGONJWA YA AKILI



Imeelezwa kuwa tabia ya kujipiga picha mwenyewe (selfie) na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ni ugonjwa wa akili ujulikanao kitaalamu ‘Selfitis’ ambapo mgonjwa wa tatizo hili hugunduliwa kwa idadi ya picha alizopiga na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham Trent na Shule Kuu ya Utawala iliyopo nchini India ndio waliogundua ugonjwa huo wa ‘Selfitis’ baada ya taarifa kulipotiwa na vyombo vya habari mwaka 2014 ambazo zilitolewa na Chama Cha Marekani cha Tiba ya Akili kuwa kujipiga picha mara kwa mara ni moja ya dalili za kupata ugonjwa wa akili.

Watafiti hao walipoiona habari hiyo walifanya utafiti zaidi na kuthibitisha kuwa watu wengi wanaopenda kujipiga picha wana maradhi hayo.

 Walitumia njia ya kupima tabia ijulikanayo kama ‘Selfitis Behaviour Scale’ ambayo inaweza kupima dalili za ugonjwa huo kama upo kwa mtu.

Kipimo hicho cha tabia kilitokana na sampuli ya watu 400 ambapo waligawanywa kwenye makundi matatu ili kuangalia tabia zao za upigaji picha kwa kutumia simu za mkononi.    

Washiriki wote walitoka nchi ya India ambako kuna matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na idadi kubwa ya watu wanaofariki kutokana na kujipiga picha ‘Selfie’ kwenye maeneo hatarishi kama majengo marefu, kwenye madaraja na mito.

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa kwenye Jalida la  International Journal of Mental Health and Addiction ambapo limebaini makundi 3 ya watu wenye dalili za ugonjwa wa akili wa ‘Selfitis’.

 Ugonjwa huo hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine kulingana idadi ya picha anazojipiga na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii. Makundi hayo ni:

 •Kundi la 1- Hawa hujipiga picha mara tatu kwa siku lakini hawaziweki kwenye mitandao ya kijamii.

•Kundi la 2- Hawa hujipiga picha mara tatu kwa siku na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii.

•Kundi la 3- Hawa hawawezi kujizuia na hujipiga picha wakati wote na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii zaidi ya mara sita kwa siku.

Tabia ya kujipiga picha huanza taratibu kutoka hatua ya kwanza na mazoea yakizidi mtu hufika hatua ya tatu ambayo huathirika kisaikolojia na hujipiga picha kwa wingi na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ili kupata faraja kwa wanaomzunguka kwa sababu anaamini hawezi tena kuishi bila kujipiga picha.
 
                       Wanafamilia wakijipiga picha 'selfie'

Sababu zinazowasukuma watu kujipiga picha

Ziko sababu sita zinazowashawishi watu ambao wameathirika na ugonjwa wa akili wa selfitis ambapo hutafuta; kuongeza kujiamini, kukubalika na kusikilizwa, kuboresha msawazo wa mawazo, kutengeneza kumbukumbu ya eneo alilotembelea, kuongeza ukaribu na ushindani kwa watu wanamfuatilia kwenye mitandao ya kijamii.

Dk. Mark Griffiths, Mtaalamu wa tabia za binadamu Idara ya Saikolojia Chuo Kikuu cha Nottingham Trent, ambaye alishiriki katika utafiti huo anasema katika ripoti yake kuwa “Miaka michache iliyopita habari ilikuwa inasambaa kwenye vyombo vya habari ikitaka maradhi ya selfitis yaorodheshwe miongoni mwa magonjwa ya akili.

Haikumaanisha kuwa selfitis haikuwepo. Tumethibitisha kuwa maradhi hayo yapo kwa kutumia kipimo cha tabia kubaini dalili za selfitis”.

Mtafiti mwingine, Dk. Jonarthanan Balakrishnan anasema; “Watu wenye maradhi hayo wanakosa ujasiri, wanajitahidi kuwa sehemu ya watu wanaowazunguka na wanaonyesha tabia za urahibu kama watu wengine".
 
Ni matumaini kuwa tafiti nyingine zitafanyika ili kuelewa jinsi watu wanavyoingia kwenye hizo tabia na nini kifanyike kuwasaidia wale ambao wameathirika zaidi”

Hata hivyo, kuna maradhi mengine ya akili ambayo yanahusishwa na watu kuogopa kuwa karibu na simu ‘normophobia’. 

Wataalamu wa mawasiliano wanaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kukabiliana na changamoto za kukuwa kwa teknolojia duniani.

Jumatatu, 8 Januari 2018

UHABA WA MIUNDOMBINU YA MAJITAKA UNAVYOCHANGIA MAGONJWA YA MLIPUKO KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM



Licha ya idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mitandao ya majitaka katika miji mikuu kuongezeka, ni asilimia 20 tu ya wananchi katika miji hiyo wanafikiwa na huduma hiyo nchini na kuwaweka katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

Miji mikuu 10 ambayo imeunganishwa kwenye mitandao wa majitaka ni Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Tabora, Moshi, Tanga, Songea na Iringa ambapo serikali imeendelea kufanya maboresho ya miundombinu ili kuhakikisha wateja wengi zaidi wanaunganishwa kwenye huduma hiyo.

Kulingana na hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa wakati huo Eng. Gerson Lwenge aliyoitoa kwenye bunge la bajeti ya mwaka 2017/2018 alisema “Idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mitandao ya majitaka katika miji hiyo imeongezeka kutoka 25,361 mwezi Machi, 2016 hadi kufikia wateja 26,636 mwezi Machi, 2017 na kuweza kupunguza kero ya majitaka kutiririka hovyo katika miji hiyo”. 

Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mtandao wa majitaka imeongezeka kutoka 18,436 mwezi Machi, 2016 hadi kufikia wateja 19,034 mwezi Machi, 2017. 

Kwa muktadha huo huduma ya uondoaji majitaka katika miji hiyo ikijumuisha Jiji la Dar es Salaam imefikia asilimia 20.

Matarajio ya wizara ya Maji na Umwagiliaji ni kuongeza huduma ya uondoaji majitaka kutoka asilimia 20 ya sasa hadi kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020. 
  Mabomba yakimwaga majitaka kwenye mto

Licha ya juhudi hizo za serikali, changamoto inabaki kwa jiji la Dar es Salaam ambalo idadi ya wakazi wake inaongezeka kwa kasi na kwamba lina uhitaji mkubwa wa huduma hiyo ili kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama dhidi ya majitaka yanayotiririka katika mitaa mbalimbali.

Kulingana na  Mamlaka ya Maji Dar es Salaam (DAWASCO) inaeleza kuwa mfumo wa majitaka katika jiji la Dar es Salaam ni mkusanyiko wa mifereji  ambayo hukusanya maji kutoka katika maeneo mbalimbali kwa kutumia  pampu zilizofungwa katika vituo 15 ambazo huyaelekeza maji hayo katika mabwawa.

Eneo linalopata huduma hiyo ni kilomita 170 ambalo limetandazwa mabomba yenye kipenyo cha milimita 100 hadi 100 ambapo maeneo ya katikati ya jiji, Kariakoo, Upanga na Muhimbili humwaga maji yake moja kwa moja katika bahari ya Hindi.

Eneo linalopata huduma hiyo ni dogo ikilinganishwa na ukubwa wa jiji hilo ambalo unafikia kilomita za mraba 1,393. 

Ni dhahiri kuwa eneo kubwa lililobaki limezungukwa na majitaka ambayo huchanganyika na maji ya visima yanayotumiwa na wananchi wengi wa jiji hilo na kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.  

Moja ya njia kubwa ambayo inaweza kueneza magonjwa kama kipindupindu ni matumizi ya maji machafu. Maji machafu yanaweza kuwa ya visima au bomba ikiwa hayawekwi dawa kuua vijidudu au kuchemshwa kabla ya kutumika.

Dar es Salaam inatajwa kuongoza kukumbwa na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu kuliko maeneo mengine nchini. 

Hali hiyo inatokana na jiji hilo kuwa na idadi kubwa ya visima vyenye vimelea ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa ya milipuko hasa kipindupindu na homa za matumbo.

Kipindupindu ni ugonjwa unaoambukizwa kupitia maji au chakula chenye vimelea ambavyo kitaalamu hujulikana kwa jina la ‘Vibrio Cholerae.’  Vimelea hivi huishi katika maji yaliyochafuliwa hasa yenye kinyesi.

Maeneo ambayo huathirika zaidi na majitaka ni Buguruni, Kigogo, Tandale, Kariakoo, Manzese na Yombo ambayo hutegemea zaidi maji ya visima virefu kama mbadala wa huduma za Dawasco, lakini visima hivyo havina maji salama.

Hili linathibitishwa na kauli ya Waziri wa Maji na Umwagilia wa wakati huo,  Mhandisi Gerson Lwenge wakati wa bunge la bajeti 2016/2017 alipoelezea kuhusu uchunguzi wa visima 108 ambapo visima 66 vilikuwa sio salama na maji yake yalikuwa na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu. Visima virefu vilikuwa 40 na vifupi ni 26.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Ardhi, unaonesha maji ya visima vingi sio salama na kushauri wachimba visima kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepusha jamii na magonjwa kwa kutumia maji yasiyokuwa salama.

Kufikia Septemba 2016, Dar Es Salaam ilikuwa na visima virefu 676 huku Wilaya za Temeke na Ilala zikiongoza kutokana na kutofikiwa na maji ya DAWASCO. Kinondoni, kwa kuwa na mtandao mkubwa wa maji ya Dawasco, hali ya kipindupindu sio mbaya.

Ni dhahiri kuwa mamlaka husika zinapaswa kutazama upya mfumo wa majitaka na kuboresha miundombinu iliyopo ili kuwafikia watu wengi zaidi katika nyumba zao. 

Pia elimu iendelee kutolewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutumia mfumo rasmi wa kutibu majitaka ili kujiepusha na athari za kiafya.