Jumanne, 17 Aprili 2018

MASHITAKA YA WATUHUMIWA WA UFISADI TCCCo YAIVA

NA CHARLES NDAGULLA,MOSHI

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini(Takukuru) mkoani Kilimanjaro,imekamilisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi wa zaidi ya shilingi Bilioni mbili zinazowakabili vigogo wa Kiwanda cha kukoboa kahawa cha Tanganyika Coffee Curing(TCCCo).

Ufisadi huo unahusisha ununuzi wa mtambo unaodaiwa kuwa ni chakavu wa kukoboa kahawa katika kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa aslimia 54 na Chama Kikuu cha ushirika(KNCU)mkoani Kilimanjaro.

Miongoni mwa wanaochunguzwa na Takukuru ni aliyekuwa  mwenyekiti  wa (KNCU),Maynard Swai ambaye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kiwamda hicho pamoja na aliyekuwa meneja mkuu wa kiwanda hicho,Andrew Kleruu .

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita,kaimu mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro,Moses Uguda amesema tayari majalada sita yanayohusu tuhuma za vigogo hao yamepelekwa kwa mkurugenzi wa mashitaka nchini(DPP) kwa ajili ya kupata kibali cha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao.

Oguda alisema kiwanda hicho ni mali ya wanaushirika na si mali ya mtu binafsi kama ambavyo baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakijaribu kuipotosha jamii na kwamba  takukuru kama chombo cha uchunguzi kinao wajibu wa kuchunguza ufisadi wa mali hizo za wanaushirika.

Mkutano huo na waandishi wa habari ulikuwa mahususi kwa ajili ya kutoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia januari hadi machi mwaka huu.

Wanahisa wengine wa kiwanda hicho ni pamoja na Chama cha   wamiliki mashamba makubwa (TCGA)kikiwa na  asilimia 36 ya hisa,Vyama vingine vinne vikuu vya ushirika   vinavyomiliki hisa kwenye kiwanda hicho ni ACU,USAMBARA,MOFACU,RIVACU na KANYOVU ambavyo vinamiliki asilimia 10 ya hisa zilizobaki.

Mtambo huo unadaiwa kununuliwa nchini Brazil  kutoka Kampuni ya Pinhalense baada ya serikali kuridhia bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho kuuza mali zake ili kununua mtambo  huo mpya.

Hata hivyo,pamoja na kiasi  hicho kikubwa cha fedha kutumika kununua mtambo huo,hadi sasa umeshindwa kuanza kutumika tofauti na matarajio ya wengi huku mtambo unaotajwa kuwa ni mbovu na haufai  ukiwa unaendelea kukoboa kahawa.
 
Uchunguzi uliofanywa na Ndagullablog umebaini kuwa  baadhi ya vifaa vimekuwa vikinyofolewa kutoka mtambo wa zamani  na kufungwa kwenye mtambo huo mpya hatua ambao imeibua maswali mengi kuliko majibu.


Sababu za kuuzwa kwa mali hizo zikiwamo nyumba  ilikuwa ni  kununua mtambo huo  mpya  ili kukiwezesha kiwanda hicho  kujiendesha kwa ufanisi na kulipa madeni ya kisheria ya zaidi ya  sh,Milioni 800 ambayo kiwanda hicho kinadaiwa ikiwamo TRA,NSSF,Manispaa ya moshi na madeni ya manunuzi.


Katika  mkutano wake na waandishi wa habari Machi 17 mwaka 2013,Maynard Swai akiwa mwenyekiti wa bodi ya kiwanda hicho,alitaja madeni hayo ya kisheria kwa  upande wa TRA ni sh,Milioni 377,541,680,NSSF(Milioni 163,391,438),Manispaa ya Moshi(Milioni 78,188,287),Astra insurance(Milioni 44,064,038),madeni ya watumishi yakiwamo mafao ya kustaafu(Milioni 59,877,236).


Pia kiwanda hicho kinadaiwa ada ya ukaguzi wa mahesabu kutoka shirika la kukagua mahesabu ya vyama vya ushirika la COASCO wanaodai sh,Milioni 10,000,000,wakati SACCOs ya kiwanda hicho ikidai sh,Milioni 2.800,000 huku madeni ya manunuzi yakiwa ni sh,Milioni 75,509,612,madeni haya ni kufikia mwaka 2013. 

Taarifa ya mwenyekiti huyo kwa  wanahabari ambayo nakala yake tunayo,ilieleza kuwa  athari zinazosababishwa na uchakavu wa mitambo hiyo iliyojengwa miaka 60 iliyopita chini ya mjerumani  Heins Bueb ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha ukoboaji kutoka tani 65,736 msimu wa 1980/81 hadi kufikia tani 3,487 msimu wa 2012/2013.


Athari nyingine ni kushuka kwa ubora wa ukoboaji kunakochangiwa na kupondwa,punje kuvunjwa vunjwa hatua ambayo alisema inasababisha hasara kwenye madaraja na kupanda kwa kiwango cha hasara kwa mkulima.

Mwenyekiti huyo  wa zamani wa bodi alisema katika kujikwamua na janga hilo,kiwanda kililazimika kupunguza wafanyakazi wake kutoka 660 hadi wafanyakazi 65 zoezi ambalo lilifanywa kwa awamu nne kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2003 .

Pamoja na upunguzaji huo wa wafanyakazi,Swai alisema bado gharama za uendeshaji ziko juu kutokana na uchakavu mkubwa  wa mitambo ambayo ina umri wa miaka 40 na kushuka kwa kiwango cha mapokezi ya kahawa.


“Bodi ilitafakari kwa kina hali ya kiwanda na  kuona umhimu wa kununua mtambo mmoja wa kisasa ili kunusuru kiwanda,mtambo unaotegemewa kununuliwa una uwezo wa kupunguza gharama ikilinganishwa na mtambo uliopo”,inasema taarifa hiyo.

Mwenyekiti huyo aliusifia sana mtambo huo  katika taarifa yake kuwa una uwezo wa kukoboa tani sita za kahawa kwa saa moja badala ya mitambo minne chakavu ya sasa inayokoboa kahawa chini ya tani tatu kwa saa  moja.

Kwamba mtambo huo mpya ungepunguza gharama za umeme kwa zaidi ya nusu ya gharama za sasa kutokana na mtambo huo mpya kuwa na “installed capacity” ya 165KW dhidi ya 431KW kwa  mtambo wa zamani.   


Jumatatu, 9 Aprili 2018

WANUNUZI BINAFSI WA KAHAWA MARUFUKU KWENDA VIJIJINI- SERIKALI



 
 JENGO LA MAKAO MAKUU YA BODI YA KAHAWA NCHINI(TCB)LILILOPO MJINI MOSHI

 NA CHARLES NDAGULLA,MOSHI

WAKULIMA  wa zao la kahawa nchini hawana budi kufurahia mabadiliko ya taratibu mpya  za usimamizi wa sekta ndogo ya kahawa baada ya kupitishwa kwa maamuzi magumu ambayo yatachangia kuleta ufanisi katika uzalishaji wa zao hilo.

Miongoni mwa maamuzi hayo magumu ni pamoja na wanunuzi binafsi kupigwa marufuku kwenda vijijini kunuua kahawa ya wakulima ambako sasa jukumu hilo linaachwa kwa vyama vya msingi ya ushrika na vyama vikuu  vya ushirika.

Kabla ya uamuzi huo,makampuni ya watu binafsi yalikuwa yakinunua kahawa kwa wakulima na hivyo kuwafanya baadhi ya wakulima kuuza kahawa yao ikiwa mbichi kwa lengo la kupata fedha za chap chap hatua ambayo ilikuwa inachangia kuwepo na kahawa chafu na isyokuwa na ubora.

Uamuzi huo ulitangazwa hivi  karibuni mjini Dodoma na Waziri wa Kilimo,Dk.Charles Tizeba katika mkutano wa tisa wa wadau wa kahawa  ulioandaliwa na Bodi ya kahawa nchini(TCB) kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.

Mkutano huo pia ulihudhuliwa na wawakirishi wa vyama vya ushirika nchini,wawakirishi wa halmashauri za wilaya zinazolima kahawa,wadau wa kahawa na wawakirishi kutoka taasisi za fedha,Benki ya ushirika(KCBL) pamoja na Bodi ya stakabadhi ghalani.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo,vyama vya msingi vya ushirika  vitakuwa na jukumu la kukusanya kahawa hiyo kutoka kwa wakulima,kuipeleka  kwenye viwanda kwa ajili ya kukoboa na baadaye kuipeleka mnadani.

Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo amesema katika taarifa yake kuwa kuanzia sasa wanunuzi wote wa kahawa sharti wawe na cheti cha ulipaji kodi
.
Aidha amesema bei atayolipwa mkulima itapatikana pale kahawa itakapouzwa mnadani na  kwamba vyama vya ushirika vitalipwa ili navyo viwalipe wakulima fedha zao kulingana na kahawa waliyokusanya.

Katika mabadiliko hayo ya uendeshaji mpya wa minada,kwa sasa wauzaji wa kahawa mnadani hawataruhusiwa kupeleka bei ya akiba na badala yake jukumu hilo litaachwa kwa dalali atakayekuwa na wajibu wa kuandaa bei ya akiba kulingana na bei ya  soko la kahawa.

Vyama vikuu vya ushirika navyo vimeonywa kutokupeleka kahawa mnadani ikiwa imechanganywa na ya vyama vingine lengo ni kulinda ubora wa kahawa na bei ya vyama vitakavyoweka juhudi katika kuzingatia ubora wa kahawa na kahawa ya kila chama cha msingi itaonekana kwenye katalogi.

“Bodi ya kahawa itatoa bei elekezi ya kahawa kwa vyama vya msingi vya ushirika  na vyama vikuu vya ushirika zitakazofaa kulipwa kama malipo ya awali”,amesema Kimaryo. 
 KAHAWA NI MALI,ITUNZE IKUTUNZE

Kuhusu wenye mashamba makubwa ya kahawa,kaimu mkurugenzi huyo amesema kuwa,nao watatakiwa kwenda kuuza kahawa yao mnadani tofauti na zamani ambako walikuwa wakiuza kahawa yao moja kwa moja nje ya nchi.

Hata    hivyo alisema wale ambao wanayo mikataba ya mauzo ya muda mrefu na wateja wao wa nje,bodi ya kahawa itaandaa utaratibu kupitia minada ili kutoathiri mikataba yao.

Akizungumzia ugharamiaji wa mikakati,Kimaryo amesema shughuli zote ambazo hapo awali zilikuwa zipo chini ya mfuko wa  wakfu wa kahawa(TCDF) ambao ulivunjwa na Waziri Mkuu hivi karibuni,zitafanywa na bodi ya kahawa.

Shughuli hizo ni pamoja na kuhamasisha uzalishaji wa miche bora ya kahawa,kugharamia mikutano ya wadau wa kahawa na kuwezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Katika hatua nyingine,mkoa wa kagera ,bado umeendelea kuwa kinara wa uzalishaji ambako katika msimu wa 2017/18 umezalisha tani 12,131 ukifuatiwa na Ruvuma iliyozalisha tani 11,914.

Mkoa wa Songwe unashika nafasi ya tatu ukizalisha tani 8,690  huku mkoa wa Kilimanjaro ukikamata nafasi ya nne kwa kuzalisha tani 2,968 na Arusha ikifunga tano bora ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji baada ya kuzalisha tani 2,312.
 WAZIRI WA KILIMO,DK CHARLES TIZEBA(kulia)AKIPATA MAELEZO KUTOKA KWA MTAAALAM WA KAHAWA(kushoto)ALIPOTEMBELEA SHAMBA LA KAHAWA LA KPL HIVI KARIBINI MKOANI KILIMANJARO(katikati) NI KAIMU MKURUGENZI WA BODI YA KAHAWA NCHINI,PRIMUS KIMARYO.

Katika uzalishaji wa kahawa duniani,Uganda na Ethiopia bado zimeng’ang’ania kwenye kumi bora ya nchi zinazozalisha kahawa kwa wingi dunia ambako Ethiopia ipo  ipo nafsi ya tano na Uganda ikiwa nafasi ya tisa.

Brazil inakamata nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Vietnam wakati Colombia inakamata nafasi ya tatu na nafasi ya nne ipo Indonesia,Honduras inakamata nafasi ya sita na India ikikamata nafasi ya saba,Peru nafasi ya nane na Guantemala ikikamata nafasi ya kumi nyuma ya Uganda.

Nchi hizo kumi ndizo zilizoshikilia roho ya kahawa duniani kwani zinazalisha aslimia 88 ya kahawa yote inayozalishwa duniani na aslimia 12 inaachwa kwa nchi nyingine ikiwamo Tanzania.

Kuhusu hali ya bei ya kahawa nchini,kaimu mkurugenzi huyo wa bodi ya kahawa, anasema kuwa,katika msimu wa 2016/2017 wakulima waliouza kahawa yao wakati bei ikiwa nzuri sokoni walipata wastani wa shilingi 5,000.

Alisema wastani wa bei kwa msimu ni shilingi 4,000 kwa kahawa ya Arabika huku wakulima wanaozalisha kahawa aina ya Robusta walilipwa wastani wa shilingi 1,200 hadi 1,400 kwak ilo ya maganda.

“Msimu huu 2017/2018 bei ya kahawa imeshuka kutokana na kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia,bei ya mkulima imekuwa ni ya wastani kutokana na ushindani unaotokana na kiwango kidogo cha uzalishaji “,alisema.
 

Uchunguzi wetu umebaini kuwa,katika misimu saba iliyopita uzalishaji wa zao la kahawa nchini umekuwa ukipanda na kushuka huku baadhi ya wakulima wakidaiwa kulipa kisogo zao hilo na kugeukia mazao mseto kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na bei ndogo.

Katika msimu wa 2010/2011 uzalishaji wa kahawa ulikuwa tani 56,790.0 lakini msimu uliofuata wa 2011/2012 uzalishaji ulishuka kwa kasi ya kutisha na kufikia tani 33,086.7 na ulipanda tena msimu wa 2012/2013 na kufikia tani 71,319.1.

Msimu wa 2013/2014 tani 48,761.9 zilizalishwa na tani hizo zilishuka tena msimu wa 2014/2015 na kufikia 42,768.0 na kupanda tena katika msimu wa 2015/2016 hadi tani 60,188.0 kabla ya kuporomoka msimu wa 2016/2017 hadi tani 46,963.0.


Amesema changamoto nyingine inayochangia kushuka kwa uzalishaji ni pamoja uwekezaji kidogo kwenye uzalishaji kutoka taasisi za fedha na wakulima wengi kutotumia kikamilifu mashine za kati (CPU)za kumenyea kahawa.


Kuhusu soko la nje amesema Italia imezipiku nchini za Japan,Ujerumani,Marekani na Ubeligiji kutokana na kuongoza kununua kahawa ya Tanzania kwa aslimia 25.18 ikifuatiwa na Japan(16.89%),Ujeruman(11.32%),Marekani(10.86%) huku Ubeligiji ikishika nafasi ya tano kwa aslimia 9.41.

 WAZIRI WA KILIMO,DK.CHARLES TIZEBA AKIONJA KAHAWA KATIKA SHAMBA LA KAHAWA LA KPL MKOANI KILIMANJARO ALIPOFANYA ZIARA YA SIKU MOJA HIVI KARIBUNI.

Alhamisi, 5 Aprili 2018

UNAHITAJI MOYO WA UVUMILIVU PAMOJA NA UTIMAMU WA MWILI KUKIFIKIA KILELE CHA UHURU,SISI TULIWEZA HATA WEWE UNAWEZA

ILIKUWA MWAKA JUZI NIKIWA KILELE CHA UHURU CHA MLIMA KILIMANJARO,MLIMA MREFU KULIKO YOTE BARANI AFRIKA.

 MWANDISHI CHIPUKIZI MKOANI ARUSHA NAYE ALITOBOA.

 VIJANA KUTOKA JESHI LA WANANCHI TANZANIA(JWTZ)WAKIWA KILELE CHA UHURU.

 NI SAFARI YA DAMU NA JASHO KUKIFIKIA KILELE CHA UHURU,MAKAMANDA HAWA WANAHABARI KUTOKA A-TOWN NAO WALITOBOA.


 MKUU WA MAJESHI MSTAAFU,JENERALI GEORGE MWITA WAITARA AMBAYE KWA SASA NI MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI YA SHIRIKA LA HIFADHI ZA TAIFA NCHINI(TANAPA) AKIWA KWENYE PICHA YA PAMOJA NA MWANAHABARI CHIPUKIZI KUTOKA ARUSHA MWAKA JUZI KATIKA KITUO CHA HOROMBO .


JENERALI WAITARA AMEKUWA AKIPANDA MLIMA KILIMANJARO TANGU MWAKA 2008 AKIRITHI MIKOBA HIYO KUTOKA KWA MKUU WA MAJESHI MSTAAFU JENERALI MRISHO SARAKIKYA.



USIKOSE PICHA MOTOMOTO ZA MATUKIO YA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO DESEMBA MWAKA JANA ALHAMISI WIKI IJAYO

Jumanne, 3 Aprili 2018

KILIMO,UVUVI HARAMU VINAVYOHATARISHA UHAI BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU


 
 Bwawa la Nyumba ya Mungu linaounguanisha wilaya za Mwanga mkoani Kilimanjaro na Simanjiro Mkoani Manyara

Bwawa la Nyumba ya Mungu ni chanzo kikubwa cha maji yanayotumika kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu, kilimo cha umwagiliaji,  mifugo na uzalishaji wa umeme, lakini shughuli hizo zinaweza kuhatarisha uzalishaji wa umeme unaosambazwa na Gridi ya Taifa. 

Bwawa la Nyumba ya Mungu  linapatikana wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro ambapo lilitengenezwa ili kuhifadhi maji yanayotiririka kutoka Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuzuia mafuriko kwenye makazi ya watu na mashamba na baadaye yatumike kuzalisha umeme na kwenye kilimo.

Lakini ongezeko la shughuli za kilimo kupitia mito ya asili ikiwemo Kikuletwa na Ruvu pembezoni mwa bwawa hilo kumechangia upotevu mkubwa wa maji kwenye vituo vya kuzalisha umeme.

Inaelezwa kuwa vituo hivyo ni Nyumba ya Mungu kilichopo Wilaya ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, New Pangani Falls, wilaya ya Muheza na Hale kilichopo wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambavyo vyote vina uwezo wa kuzalisha megawati 97.

Akizungumza na wanahabari Meneja wa vituo hivyo, Mhandisi  Mahenda Mahenda alisema kwenye  Bwawa la Nyumba ya Mungu kuna mitambo miwili inayozalisha umeme iliyoanza kazi 1969 ambapo mitambo hiyo inafanya kazi vizuri na imekuwa ikifanyiwa matengenezo mara kwa mara.

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji yanayotumiwa na wakazi wa wilaya zinazozunguka bwawa hilo yamechangia kupungua kwa kina cha maji.
 Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu(katikati)akipokea maelezo mafupi ya shughuli za uzalishaji umeme katika kituo cha kupozea umeme cha Bwawa la Nyumba ya Mungu alipotembelea bwawa hilo hivi karibini.

 “Bwawa linapokuwa na kiwango kidogo cha maji uzalishaji umeme hupungua, kuna wakati maji hupungua zaidi hivyo taratibu haziruhusu tuendelee kuzalisha umeme”,anasema.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kituo cha Nyumba ya Mungu, Mhandishi, Clarence Mahunda alisema kituo chake kina uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 8 ambao huingizwa kwenye Gridi ya Taifa kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani na viwandani.

Mhandisi Mahunda alisema hadi kufikia mwishoni mwa Januari mwaka huu kituo hicho klikuwa kinazalisha megawati 3.5 hadi 4 tofauti na uwezo wake wa kuzalisha megawati 8 kwa saa 24.

“Shughuli za binadamu zikiwemo kulima, kuchunga ng’ombe na uvuvi kumepelekea uzalishaji wa umeme katika kituo hiki kuwa hafifu, kitu ambacho kinasababisha ukosefu wa maji ya kutosha hivyo uzalishaji umeme pungufu”, alisema Mhandisi Mahunda.

Alibainisha kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo  wameendelea kuzuia athari za kimazingira pembezoni mwa bwawa la Nyumba ya Mungu lakini bado uwezo wa uzalishaji umeme haujaongezeka kwasababu kina cha maji kiko chini.

Mkazi wa kijiji  cha Kagongo kilichopo wilaya ya Mwanga  mkoani Kilimanjaro, Charles John Waziri  alisema kuwa kuna hujuma katika matumizi ya rasilimali maji ambapo imebainika kuwa wakulima wanaotumia kilimo cha umwagiliaji wamekua wakitumia maji kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu katika bwawa.

Naye, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alizitaka serikali za mitaa na Mkoa kwa kushirikiana na wananchi wanaozunguka vituo hivyo kuhakikisha wanatunza mazingira ya Bwawa la Nyumba ya Mungu ili kupata maji kwa ajili ya uzalishaji umem

“Nimeelezwa kuwa kina cha maji hakiruhusu mashine zote kuzalisha umeme, na hii ni kwasababu ya shughuli za binadamu ambazo zinaendelea pembezoni mwa Bwawa la maji yanayotumika kuzalisha umeme huo”, alisema Naibu Waziri.

Wadau wa mazingira wamezishauri mamlaka zinazohusika na bwawa hilo ziwajibike kuhamasisha uboreshaji mifereji kwa kuisakafia ili kuokoa upotevu mkubwa wa maji na kuachana na mifereji ya asili ambayo inapoteza maji mengi yanayoingia kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu.
 

 Pichani ni Boti iliyonunuliwa na Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani manyara kwa ajili ya kufanya dori kukabiliana na uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu,boti hiyo sasa haifanyi kazi.

Nyumba ya Mungu

Bwawa la nyumba ya Mungu lilijengwa na kukamilika mwaka 1965 Kaskazini mwa Tanzania. Mwaka 1970 lilianza kutumiwa zaidi kwa uvuvi wa samaki lakini mabadiliko ya hali ya hewa yamepunguza upatikanaji wa samaki na uzalishaji umeme katika bwawa hilo. 

Bwawa hilo lilijengwa karibu na maporomoko ya Neogene Kilomita 80 kutoka Kusini mwa mlima Kilimanjaro ambapo urefu wake unafikia Kilomita 180 na kina cha maji cha mita 6 kwenda chini. Bwawa hilo linapokea maji kutoka vyanzo mbalimbali lakini chanzo kikubwa ni mlima Kilimanjaro.

Maji yanayotoka kwenye bwawa hilo hutumika kuzalisha umeme katika vituo vya Pangani, Nyumba ya Mungu na Hale. Lakini bwawa hilo limeathiriwa mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za binadamu.