TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini(Takukuru) mkoani Kilimanjaro,imekamilisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi wa zaidi ya shilingi Bilioni mbili zinazowakabili vigogo wa Kiwanda cha kukoboa kahawa cha Tanganyika Coffee Curing(TCCCo).
Ufisadi huo unahusisha ununuzi wa
mtambo unaodaiwa kuwa ni chakavu wa kukoboa kahawa katika kiwanda hicho
kinachomilikiwa kwa aslimia 54 na Chama Kikuu cha ushirika(KNCU)mkoani
Kilimanjaro.
Miongoni mwa wanaochunguzwa na
Takukuru ni aliyekuwa mwenyekiti wa (KNCU),Maynard Swai ambaye
alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kiwamda hicho pamoja na aliyekuwa
meneja mkuu wa kiwanda hicho,Andrew Kleruu .
Akizungumza na waandishi wa habari
wiki iliyopita,kaimu mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro,Moses Uguda amesema
tayari majalada sita yanayohusu tuhuma za vigogo hao yamepelekwa kwa mkurugenzi
wa mashitaka nchini(DPP) kwa ajili ya kupata kibali cha kuwafikisha mahakamani
watuhumiwa hao.
Oguda alisema kiwanda hicho ni mali
ya wanaushirika na si mali ya mtu binafsi kama ambavyo baadhi ya watuhumiwa
wamekuwa wakijaribu kuipotosha jamii na kwamba takukuru kama chombo cha
uchunguzi kinao wajibu wa kuchunguza ufisadi wa mali hizo za wanaushirika.
Mkutano huo na waandishi wa habari
ulikuwa mahususi kwa ajili ya kutoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo
katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia januari hadi machi mwaka huu.
Wanahisa wengine wa kiwanda hicho ni
pamoja na Chama cha wamiliki mashamba makubwa (TCGA)kikiwa na
asilimia 36 ya hisa,Vyama vingine vinne vikuu vya ushirika
vinavyomiliki hisa kwenye kiwanda hicho ni ACU,USAMBARA,MOFACU,RIVACU na
KANYOVU ambavyo vinamiliki asilimia 10 ya hisa zilizobaki.
Mtambo huo unadaiwa kununuliwa
nchini Brazil kutoka Kampuni ya Pinhalense baada ya serikali kuridhia
bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho kuuza mali zake ili kununua mtambo
huo mpya.
Hata hivyo,pamoja na kiasi
hicho kikubwa cha fedha kutumika kununua mtambo huo,hadi sasa umeshindwa kuanza
kutumika tofauti na matarajio ya wengi huku mtambo unaotajwa kuwa ni mbovu na
haufai ukiwa unaendelea kukoboa kahawa.
Uchunguzi uliofanywa na Ndagullablog umebaini kuwa baadhi ya vifaa vimekuwa vikinyofolewa kutoka mtambo wa
zamani na kufungwa kwenye mtambo huo mpya hatua ambao imeibua maswali
mengi kuliko majibu.
Sababu za kuuzwa kwa mali hizo
zikiwamo nyumba ilikuwa ni kununua mtambo huo mpya ili
kukiwezesha kiwanda hicho kujiendesha kwa ufanisi na kulipa madeni ya
kisheria ya zaidi ya sh,Milioni 800 ambayo kiwanda hicho kinadaiwa
ikiwamo TRA,NSSF,Manispaa ya moshi na madeni ya manunuzi.
Katika mkutano wake na
waandishi wa habari Machi 17 mwaka 2013,Maynard Swai akiwa mwenyekiti wa bodi
ya kiwanda hicho,alitaja madeni hayo ya kisheria kwa upande wa TRA ni
sh,Milioni 377,541,680,NSSF(Milioni 163,391,438),Manispaa ya Moshi(Milioni
78,188,287),Astra insurance(Milioni 44,064,038),madeni ya watumishi yakiwamo
mafao ya kustaafu(Milioni 59,877,236).
Pia kiwanda hicho kinadaiwa ada ya
ukaguzi wa mahesabu kutoka shirika la kukagua mahesabu ya vyama vya ushirika la
COASCO wanaodai sh,Milioni 10,000,000,wakati SACCOs ya kiwanda hicho ikidai
sh,Milioni 2.800,000 huku madeni ya manunuzi yakiwa ni sh,Milioni 75,509,612,madeni
haya ni kufikia mwaka 2013.
Taarifa ya mwenyekiti huyo kwa
wanahabari ambayo nakala yake tunayo,ilieleza kuwa athari
zinazosababishwa na uchakavu wa mitambo hiyo iliyojengwa miaka 60 iliyopita
chini ya mjerumani Heins Bueb ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha
ukoboaji kutoka tani 65,736 msimu wa 1980/81 hadi kufikia tani 3,487 msimu wa
2012/2013.
Athari nyingine ni kushuka kwa ubora
wa ukoboaji kunakochangiwa na kupondwa,punje kuvunjwa vunjwa hatua ambayo
alisema inasababisha hasara kwenye madaraja na kupanda kwa kiwango cha hasara
kwa mkulima.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa
bodi alisema katika kujikwamua na janga hilo,kiwanda kililazimika kupunguza
wafanyakazi wake kutoka 660 hadi wafanyakazi 65 zoezi ambalo lilifanywa kwa
awamu nne kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2003 .
Pamoja na upunguzaji huo wa
wafanyakazi,Swai alisema bado gharama za uendeshaji ziko juu kutokana na
uchakavu mkubwa wa mitambo ambayo ina umri wa miaka 40 na kushuka kwa
kiwango cha mapokezi ya kahawa.
“Bodi ilitafakari kwa kina hali ya
kiwanda na kuona umhimu wa kununua mtambo mmoja wa kisasa ili kunusuru
kiwanda,mtambo unaotegemewa kununuliwa una uwezo wa kupunguza gharama
ikilinganishwa na mtambo uliopo”,inasema taarifa hiyo.
Mwenyekiti huyo aliusifia sana
mtambo huo katika taarifa yake kuwa una uwezo wa kukoboa tani sita za
kahawa kwa saa moja badala ya mitambo minne chakavu ya sasa inayokoboa kahawa
chini ya tani tatu kwa saa moja.
Kwamba mtambo huo mpya ungepunguza
gharama za umeme kwa zaidi ya nusu ya gharama za sasa kutokana na mtambo huo
mpya kuwa na “installed capacity” ya 165KW dhidi ya 431KW kwa mtambo wa
zamani.