JENGO LA MAKAO MAKUU YA BODI YA KAHAWA NCHINI(TCB)LILILOPO MJINI MOSHI
WAKULIMA wa zao la kahawa
nchini hawana budi kufurahia mabadiliko ya taratibu mpya za usimamizi wa
sekta ndogo ya kahawa baada ya kupitishwa kwa maamuzi magumu ambayo yatachangia
kuleta ufanisi katika uzalishaji wa zao hilo.
Miongoni mwa maamuzi hayo magumu ni
pamoja na wanunuzi binafsi kupigwa marufuku kwenda vijijini kunuua kahawa ya
wakulima ambako sasa jukumu hilo linaachwa kwa vyama vya msingi ya ushrika na
vyama vikuu vya ushirika.
Kabla ya uamuzi huo,makampuni ya
watu binafsi yalikuwa yakinunua kahawa kwa wakulima na hivyo kuwafanya baadhi
ya wakulima kuuza kahawa yao ikiwa mbichi kwa lengo la kupata fedha za chap
chap hatua ambayo ilikuwa inachangia kuwepo na kahawa chafu na isyokuwa na
ubora.
Uamuzi huo ulitangazwa hivi
karibuni mjini Dodoma na Waziri wa Kilimo,Dk.Charles Tizeba katika mkutano wa
tisa wa wadau wa kahawa ulioandaliwa na Bodi ya kahawa nchini(TCB) kwa
kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.
Mkutano huo pia ulihudhuliwa na
wawakirishi wa vyama vya ushirika nchini,wawakirishi wa halmashauri za wilaya
zinazolima kahawa,wadau wa kahawa na wawakirishi kutoka taasisi za fedha,Benki
ya ushirika(KCBL) pamoja na Bodi ya stakabadhi ghalani.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo,vyama
vya msingi vya ushirika vitakuwa na jukumu la kukusanya kahawa hiyo
kutoka kwa wakulima,kuipeleka kwenye viwanda kwa ajili ya kukoboa na
baadaye kuipeleka mnadani.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa
Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo amesema katika taarifa yake kuwa
kuanzia sasa wanunuzi wote wa kahawa sharti wawe na cheti cha ulipaji kodi
.
Aidha amesema bei atayolipwa mkulima
itapatikana pale kahawa itakapouzwa mnadani na kwamba vyama vya ushirika
vitalipwa ili navyo viwalipe wakulima fedha zao kulingana na kahawa
waliyokusanya.
Katika mabadiliko hayo ya uendeshaji
mpya wa minada,kwa sasa wauzaji wa kahawa mnadani hawataruhusiwa kupeleka bei
ya akiba na badala yake jukumu hilo litaachwa kwa dalali atakayekuwa na wajibu
wa kuandaa bei ya akiba kulingana na bei ya soko la kahawa.
Vyama vikuu vya ushirika navyo
vimeonywa kutokupeleka kahawa mnadani ikiwa imechanganywa na ya vyama vingine
lengo ni kulinda ubora wa kahawa na bei ya vyama vitakavyoweka juhudi katika
kuzingatia ubora wa kahawa na kahawa ya kila chama cha msingi itaonekana kwenye
katalogi.
“Bodi ya kahawa itatoa bei elekezi
ya kahawa kwa vyama vya msingi vya ushirika na vyama vikuu vya ushirika
zitakazofaa kulipwa kama malipo ya awali”,amesema Kimaryo.
KAHAWA NI MALI,ITUNZE IKUTUNZE
Kuhusu wenye mashamba makubwa ya
kahawa,kaimu mkurugenzi huyo amesema kuwa,nao watatakiwa kwenda kuuza kahawa
yao mnadani tofauti na zamani ambako walikuwa wakiuza kahawa yao moja kwa moja
nje ya nchi.
Hata hivyo alisema wale
ambao wanayo mikataba ya mauzo ya muda mrefu na wateja wao wa nje,bodi ya
kahawa itaandaa utaratibu kupitia minada ili kutoathiri mikataba yao.
Akizungumzia ugharamiaji wa
mikakati,Kimaryo amesema shughuli zote ambazo hapo awali zilikuwa zipo chini ya
mfuko wa wakfu wa kahawa(TCDF) ambao ulivunjwa na Waziri Mkuu hivi
karibuni,zitafanywa na bodi ya kahawa.
Shughuli hizo ni pamoja na
kuhamasisha uzalishaji wa miche bora ya kahawa,kugharamia mikutano ya wadau wa
kahawa na kuwezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Katika hatua nyingine,mkoa wa kagera
,bado umeendelea kuwa kinara wa uzalishaji ambako katika msimu wa 2017/18
umezalisha tani 12,131 ukifuatiwa na Ruvuma iliyozalisha tani 11,914.
Mkoa wa Songwe unashika nafasi ya
tatu ukizalisha tani 8,690 huku mkoa wa Kilimanjaro ukikamata nafasi ya nne
kwa kuzalisha tani 2,968 na Arusha ikifunga tano bora ya mikoa inayoongoza kwa
uzalishaji baada ya kuzalisha tani 2,312.
WAZIRI WA KILIMO,DK CHARLES TIZEBA(kulia)AKIPATA MAELEZO KUTOKA KWA MTAAALAM WA KAHAWA(kushoto)ALIPOTEMBELEA SHAMBA LA KAHAWA LA KPL HIVI KARIBINI MKOANI KILIMANJARO(katikati) NI KAIMU MKURUGENZI WA BODI YA KAHAWA NCHINI,PRIMUS KIMARYO.
Katika uzalishaji wa kahawa
duniani,Uganda na Ethiopia bado zimeng’ang’ania kwenye kumi bora ya nchi
zinazozalisha kahawa kwa wingi dunia ambako Ethiopia ipo ipo nafsi ya
tano na Uganda ikiwa nafasi ya tisa.
Brazil inakamata nafasi ya kwanza
ikifuatiwa na Vietnam wakati Colombia inakamata nafasi ya tatu na nafasi ya nne
ipo Indonesia,Honduras inakamata nafasi ya sita na India ikikamata nafasi ya
saba,Peru nafasi ya nane na Guantemala ikikamata nafasi ya kumi nyuma ya
Uganda.
Nchi hizo kumi ndizo zilizoshikilia
roho ya kahawa duniani kwani zinazalisha aslimia 88 ya kahawa yote
inayozalishwa duniani na aslimia 12 inaachwa kwa nchi nyingine ikiwamo
Tanzania.
Kuhusu hali ya bei ya kahawa
nchini,kaimu mkurugenzi huyo wa bodi ya kahawa, anasema kuwa,katika msimu wa
2016/2017 wakulima waliouza kahawa yao wakati bei ikiwa nzuri sokoni walipata
wastani wa shilingi 5,000.
Alisema wastani wa bei kwa msimu ni
shilingi 4,000 kwa kahawa ya Arabika huku wakulima wanaozalisha kahawa aina ya
Robusta walilipwa wastani wa shilingi 1,200 hadi 1,400 kwak ilo ya maganda.
“Msimu huu 2017/2018 bei ya kahawa
imeshuka kutokana na kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia,bei ya
mkulima imekuwa ni ya wastani kutokana na ushindani unaotokana na kiwango
kidogo cha uzalishaji “,alisema.
Uchunguzi wetu umebaini
kuwa,katika misimu saba iliyopita uzalishaji wa zao la kahawa nchini umekuwa
ukipanda na kushuka huku baadhi ya wakulima wakidaiwa kulipa kisogo zao hilo na
kugeukia mazao mseto kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na bei
ndogo.
Katika msimu wa 2010/2011 uzalishaji
wa kahawa ulikuwa tani 56,790.0 lakini msimu uliofuata wa 2011/2012 uzalishaji
ulishuka kwa kasi ya kutisha na kufikia tani 33,086.7 na ulipanda tena msimu wa
2012/2013 na kufikia tani 71,319.1.
Msimu wa 2013/2014 tani 48,761.9
zilizalishwa na tani hizo zilishuka tena msimu wa 2014/2015 na kufikia 42,768.0
na kupanda tena katika msimu wa 2015/2016 hadi tani 60,188.0 kabla ya
kuporomoka msimu wa 2016/2017 hadi tani 46,963.0.
Amesema changamoto nyingine
inayochangia kushuka kwa uzalishaji ni pamoja uwekezaji kidogo kwenye
uzalishaji kutoka taasisi za fedha na wakulima wengi kutotumia kikamilifu
mashine za kati (CPU)za kumenyea kahawa.
Kuhusu soko la nje amesema Italia
imezipiku nchini za Japan,Ujerumani,Marekani na Ubeligiji kutokana na kuongoza
kununua kahawa ya Tanzania kwa aslimia 25.18 ikifuatiwa na Japan(16.89%),Ujeruman(11.32%),Marekani(10.86%)
huku Ubeligiji ikishika nafasi ya tano kwa aslimia 9.41.
WAZIRI WA KILIMO,DK.CHARLES TIZEBA AKIONJA KAHAWA KATIKA SHAMBA LA KAHAWA LA KPL MKOANI KILIMANJARO ALIPOFANYA ZIARA YA SIKU MOJA HIVI KARIBUNI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni