Jumanne, 20 Februari 2018

TAJIRI MOSHI AKAMATWA NA MAPIPA KUMI YA KEMILAKI ZA HATARI,NI WIFRED LUCAS TARIMO


JESHI  la polisi mkoani Kilimanjaro,limemtia mbaroni mfanyabiashara  maarufu katika miji ya Moshi na Arusha,Wilfred  Lucas Tarimo  kwa kutuhuma za kukutwa na mapipa kumi yaliyosheheni kemikali bashirifu zilizopigwa marufuku na serikali.

Tarimo ambaye pia ni mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Derrick Global Trading(D.G.T) ya mjini Moshi  watengenezaji wa pombe aina ya banana kupitia kinywaji chake cha Budget,alikamatwa hivi karibuni na polisi pamoja na mkewe aliyetajwa kwa jina moja la Irene.

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro,Koka Moita alidhibitisha kukamatwa kwa mfanyabaishara huyo alipozungumza na mtandao huu na kwamba upelelezi juu ya tuhuma hizo unaendelea.

Kwa mujibu wa kamanda Koka,tayari ofisi ya Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa(RCO) imemwandikia barua mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara kemmikali hizo na kubaini aina ya kemikali husika pamoja na thamani yake.

“Ni kweli hilo tukio la Wilfred Tarimo lipo,amekamatwa na mapipa kumi ya kemikali na nimezungumza na  RCO amesema tayari wameshamwandikia barua mkemia mkuu wa serikali li waje kuzifanyia uchunguzi wa kimaabara hizo kemikali na hapo ndipo tutajua aina ya kemikali na thamani yake kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa”,alisema Koka.

Mtandao huu  umezungumza na mkemia mwandamizi wa serikali kanda ya Kaskazini,Christphera Anyango kutaka kujua namna wanavyopokea sampuri kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.

Kwa mujibu wa Anyango,ofisi yao hupokea sampuli mbali mbali kutoka polisi na kuzifanyia uchunguzi na kwamba pia wanaweza kuchukua sampuli wenyewe kulingana na mahitaji ya wahusika.

“Polisi wanaweza wakaleta sampuli wenyewe na kama kuna kitu kinahitaji utaalamu zaidi wanatuandikia barua na sisi tunakwenda kuchukua wenyewe na kuzifanyia uchunguzi”,alisema.

Alipoulizwa kama wameshapokea barua kutoka ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai(RCO) mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kwenda kuchukua sampuli za kemikali zilizokamatwa kwa mfanyabiashara huyo,ofisa huyo alisema yupo nje ya ofisi.

Hata hivyo aliomba atafutwe ofisa mwenzake  aliyemwachia ofisi aliyetajwa kwa jina la Joyce Njisya ambaye amekiri kupokea barua hiyo kutoka polisi Kilimanjaro alipozungumza na Jamhuri.

Akizungumza na mtanao huu  kwa nija ya simu,Joyce amesema kuwa yatari wameshachukua sampuli za kemikali hizo na kuzituma makao makuu ya ofisi ya mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.

“Ni kweli hiyo barua tumeshaipokea na tumeshachukua sampuli na kuzipeleka makao makuu yetu kwa ajili  ya uchunguzi,tukikamilisha uchunguzi wetu tutarejesha majibu ya uchunguzi kwa polisi,wao ndo watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuyatolea majibu”,alisema.


Hata hivyo mfanyabiashara huyo hakukiri wala kukanusha kukamatwa na shehena ya kemikali zilizopigwa  marufuku na serikali kwani baada ya kupigiwa simu alidai yupo kwenye kikao na aliahidi kuwasiliana na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kikao hicho lakini hakufanya hivyo.

Na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake ya kiganjani,bado mfanyabiashara huyo hakuweza kujibu maswali aliyoulizwa na mwandishi wa habari hizi.

“Mr.Wilfred Tarimo habari za leo?,naitwa Charles Ndagulla mwandishi wa habari gazeti la Jamhuri,unazungumziaje tuhuma za wewe na mke wako Irene kukamatwa na polisi mkituhumiwa kukutwa na mapipa kumi yenye kemikali bashirifu zilizopigwa marufuku na serikali?,unasomeka ujumbe huo.

Kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kunakuja siku chache baada ya maofisa wa Mamlaka ya  Chakula la Dawa(TFDA)Kanda ya kaskazini,kukifunga kiwanda hicho cha kutengeneza pombe aina ya Banana cha Derrick Global Trading(D.G.T ) baada ya  kubainika kuwa na kasoro .

Kiwanda hicho kilifungwa chini ya kifungu cha 181 sura ya 209 ya sheria ya chakula na dawa ya mwaka 2003 kutokana na tuhuma za kutumia nembo ya kiwanda kingine cha kutengeneza pombe kali kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari kiwandani hapo hivi karibuni,Mkaguzi wa chakula mwandamizi kutoka TFDA Kanda ya kaskazini,William Mhina,alisema sababu nyingine za  kufungwa kwa kiwanda hicho ni mazingira yasiyoridhisha ya kiwanda hicho.

Alitaja sababu zingine ni wafanyakazi kutokuwa na vyeti vya kuonyesha afya zao huku wafanyakazi hasa wa kike kutokuvaa kofia kichwani.

Alisema uchunguzi wao umebaini kuwa,eneo la kuoshea chupa ni chafu na kwamba chupa hizo zimekuwa zikioshwa katika mazingira yasiyoridhisha.

Alisema wamiliki wa kiwanda hicho wamepewa muda wa kurekebisha kasoro hizo na baada ya kufanya hivyo TFDA itafanya ukaguzi tena kujiridhisha kama kasoro hizo zimefanyiwa kazi,

Mbali na kufungwa kwa kiwanda hicho,jeshi la polisi kwa kushirikiana na maofisa wa mamlaka ya mapato Tanzania(TRA),walifanikiwa kukamata shehena ya vifungashio  vinavyotumiwa na kampuni moja mkoani Shinyanga  ya Canon General Supply inayojihusisha na utengenezaji wa pombe kali aina ya Shujaa.

Vifungashio hivyo vilikamatwa ndani ya kiwanda hicho kilichopo eneo la Kwa Alphone kata ya Kibolironi  huku baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho wakishikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi.

Akizungumzia tukio hilo,ofisa huyo kutoka TFDA alisema hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria inayosimamia usajili wa bidhaa na kuongeza kuwa,vifungashio vilivyokamatwa ndani ya kiwanda hicho havimo kwenye orodha ya usajili wa bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro,Hamisi Issah alisema jeshi hilo linamshikilia meneja wa Kiwanda hicho aliyemtaja kwa jina la Boniface Damas(56) pamoja na wafanyakazi watatu wa kiwanda hicho.

Kamanda Issah aliwataja wafanyakazi hao kuwani Severine Pantaleo(37),Riziki Fabian (28) na Daniel Japhet(18) ambao wanadaiwa kukutwa na pombve kali iliyofungashwa kwenye viroba iana ya Zed inayodaiwa kutengenezwa kienyeji.

“Viroba hivyo vina alama zake,lakini watuhumiwa hawa walikuwa wakitengeneza katika mfumo wanaoujua wenyewe,utengenezaji wa pombe usiozingatia taratibu ni hatari na unaweza kuleta madhara makubwa kwa wanywaji”,alisema kama Issah.

Kuhusu vifungashio vilivyokamatwa ndani ya kiwanda cha D.G.T,kamanda Issah alisema kuwa,wamiliki wa kiwanda hicho hawakuwa na haki stahiki ya kutengeneza pombe hizo kutokana na kutengeneza pombe hizo pasipo kuzungitia tararibu za kisheria.

Kamanda Issah amesema polisi kwa kushirikiana na TFDA wanafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo ikiwamo matumizi ya malighafi isiyo ya kiwanda hicho na uchunguzi ukikamilika sheria itachukua mkondo wake kwa watakaobainika kutenda makosa.

Hata hivyo tangu kukamatwa kwa watuhumiwa hao  uchunguzi wa Jamhuri umebaini kuwa mpaka sasa hawafikishwa mahakamani.





MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni