Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limemtia mbaroni mkazi wa
wilaya ya Mwanga, aliyekuwa akisakwa kwa udi na uvumba kwa kutumia majina ya
viongozi kutapeli fedha kwa njia ya mtandao.
Kamanda wa Polisi mkoa
Kilimanjaro, Koka Moita, alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa
kutumia jina la aliyekuwa mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Said Mecki Sadick kutapeli
fedha.
Kaimu kamanda huyo
alisema ingawa mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 28 kwa tuhuma za kuiba shehena
ya viazi huko Tarakea wilayani Rombo, lakini alikuwa akitafutwa kwa tuhuma za
utapeli.
“Anatuhumiwa kuiba
viazi funzo nzima huko Tarakea Rombo lakini tulikuwa tunamtafuta kwa
impersonation (kujifanya) yeye ni Said Mecki Sadick aliyekuwa mkuu wa mkoa
wakati siye,”alisema.
Moita alisema mtuhumiwa
huyo, Hassan Omary Kashingo, anashikiliwa kituo kikuu cha polisi Moshi na
kuwataka wananchi ambao walifungua taarifa juu yake, wafike ofisi ya RCO
Kilimanjaro.
Desemba 15,2015,
aliwahi kukamatwa na Polisi kwa tuhuma za kutumia jina la aliyekuwa Katibu Mkuu
Kiongozi , sasa ni mwenyekiti wa bodi ya chuo cha Diplomasia, Balozi Ombeni
Sefue kutapeli.
Wakati akikamatwa,
tayari kulikuwa na majalada zaidi ya nane ya utapeli katika kituo cha kati
mjini Moshi, na haijulikani ilikuwaje hakurejeshwa Moshi kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Kumbukumbu za Polisi, zinaonyesha kuwa mtuhumiwa huyo anatumia
majina tofauti tofauti ya Hassan Abdalah au “Golota”, Yusuph Mjema au
“Kashingo”, na majina mengi ambayo hayajabainika.
Novemba mwaka jana
mtuhumiwa huyo anadaiwa kutumia jina Sadick kutapeli
fedha kutoka kwa viongozi mbalimbali wa umma, dini na wananchi wa kawaida,
akijitambulisha kuwa ni Sadick.
Aliyekuwa Kamanda wa
Polisi mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alitangaza Jeshi hilo kumsaka kwa
udi na uvumba mtuhumiwa huyo kwa tuhuma mbalimbali za utapeli akisajili laini
ya Sadick.
Kwa upande wake, mkuu
wa mkoa Kilimanjaro, Said Mecki Sadick
alilithibitishia gazeti hili mwaka jana, kupokea taarifa za kuwepo kwa
mtu anayetumia jina lake kutapeli na kwamba tayari ameripoti polisi.
Mtuhumiwa huyo ndiye
ambaye Desemba 4, 2015, alimpigia mhadhiri mmoja wa chuo kikuu cha St. John cha
mjini, na kujifanya yeye
ni Balozi Sefue, na kwamba ana shida.
Katika maongezo hayo,
mtuhumiwa huyo ambaye ni mhitimu wa darasa la saba, alimuomba Profesa huyo amtumie
mtoto wake Sh500,000 ambaye amepata dharura akiwa mkoani Singida.
Hata hivyo ilibainika
baadae kuwa mtu huyo hakuwa Balozi Ombeni Sefue na ndipo DCI alipounda kikosi
kazi kilichopiga kambi mkoani Kilimanjaro na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumia
huyo.
Mtuhumiwa huyo ndiye
anayetuhumiwa kati ya mwaka 2013 na 2015, alitapeli viongozi
mbalimbali kwa kutumia jina la mwandishi mwandamizi wa habari wa mkoa wa
Kilimanjaro, Daniel Mjema.
Chanzo:Mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni