Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
imewaburuza kortini watumishi wawili wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi mkoani
Kilimanjaro kwa tuhuma za ufisadi.
Waliofikishwa
mbele ya Hakimu Mkazi wa Moshi, Pamela Mazengo ni Nicodemus Nyaki ambaye ni
karani idara ya fedha na Dk Lucas Kawishe aliyekuwa Kaimu Mganga mkuu wa
Halmashauri hiyo.
Washitakiwa
hao walifikishwa kortini hivi karibuni na kusomewa mashitaka manne yanayohusu kughushi
nyaraka zinazohusu malipo ya Sh4.6 milioni, na mwendesha mashitaka wa Takukuru
Susan Kimaro.
Mwendesha
mashitaka huyo wa Takukuru alidai Novemba 4,2012, katika ofisi za kiwanda cha
sukari cha TPC, washitakiwa waligushi barua wakitaka waidhinishiwe kiasi hicho
cha fedha.
Fedha
hizo walidai ni kwa ajili ya kuwalipa madaktari bingwa na dereva ambao
walishiriki katika kliniki maalumu katika hospitali ya TPC, huku wakifahamu
kuwa taarifa hizo zilikuwa ni uongo.
Katika
shitaka lingine, ilidaiwa kuwa kati ya Desemba 8 na 17,2012 katika eneo hilo
hilo, washitakiwa walighushi hati ya malipo namba PV001579 kuonyesha kiasi hicho
cha fedha kingelipwa madaktari hao.
Halikadhalika
ilidaiwa kuwa Desemba 14 mwaka huo huo, washitakiwa waligushi orodha yenye
majina ambayo ilionyesha wamelipwa jumla ya Sh4.6 milioni, wakati wakifahamu
orodha hiyo ni ya uongo.
Mbali
na kosa hilo, lakini wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 8 hadi 17,2012, wakiwa
watumishi wa Halmashauri ya Moshi, walitumia vocha namba PV001579 ambayo
ilikuwa na maelezo ya uongo.
Maelezo
katika vocha hiyo yaliyoonyesha Sh4.6 milioni zililipwa kwa madaktari bingwa na
dereva ambao walihudhuria klini maalum, yanadaiwa kuwa ya uongo kwa lengo la
kumpotosha mwajiri.
Washitakiwa
walikana mashitaka hayo na kuachiwa kwa dhamana hadi Februari 22, wakati kesi
yao itakapotajwa kwa kuwa upelelezi wa makosa yao ulikuwa bado haujakamilika.
Chanzo. Mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni