Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka 2017 ambapo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 7.22 huku vitendo vya udanganyifu vikiongezeka ukilinganisha na mwaka 2016.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Charles Msonde ametangaza matokeo hayo leo jijini Dar es Salaam ambapo amesema ufaulu wa mtihani huo ni asilimia 77.09 ukilinganishwa na asilimia 70.68 ya mwaka 2016.
“Jumla ya watahiniwa 287,713 ambao ni sawa na asilimia 77.09 wamefaulu mitihani ya kidato cha nne 2017 (Wanafunzi wa shule na kujitegemea) ambao katika hao wasichana wapo 143,728 sawa na 75.21% wakati wavulana wapo 143,985 sawa na asilimia 79.06%.
"Mwaka jana wanafunzi waliofaulu mtihani ya kidato cha nne walikuwa 277,283 ambao ni sawa na 70.09% hivyo ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 7.22”, amesema Dkt. Msonde.
Watahiniwa waliojiandikisha kufanya mtihani huo walikuwa 385,767 huku 323,332 walikuwa watahiniwa shule na 62,435 wa kujitegemea. Watahiniwa wa shule 317,177 ambao ni sawa 98.28% ndio waliofanikiwa kufanya mtihani na wale wa kujitegeme 57,133 ambao sawa na 91.57% walifanya mtihani huo.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa shule zinazomilikiwa na watu binafsi zimefanya vizuri na kushika nafasi 10 za mwanzo na kuzipita kwa mbali shule za serikali.
Shule ya kwanza ni St. Francis Girls ya mkoani Mbeya, Feza Boys (Dar es Salaam), Kemebos (Kagera), Bethel Sabs Girls (Iringa), Anwarite (Kilimanjaro), Marian Girls (Pwani), Canossa (Dar es Salaam), Feza Girls (Dar es Salaam), Marian Boys (Pwani), Shamsiye (Dar es Salaam).
Shule kumi za mwisho ni Kusini (Kusini Unguja), Pwani Mchangani (Kaskazini Unguja), Mwenge SMZ, Langoni (Mjini Magharibi), Furaha (Dar es Salaam), Mbesa (Ruvuma), Kabugaro (Kagera), Chokocho (Kusini Pemba), Nyeburu (Dar es Salaam) na Mtule (Kusini Unguja).
Mwanafunzi Ferson Mdee kutoka shule ya sekondari ya Marian Boys ameongoza kwa ufaulu na kushika nafasi ya kwanza kitaifa.
Vitendo vya udanganyifu vyatawala
Licha ya ufaulu kuongezeka kwa mwaka 2017 lakini ulitawaliwa na vitendo vya udangajifu vilivyofanywa na baadhi ya wanafunzi katika mtihani huo ikiwemo kuingia na simu kwenye vyumba vya mitihani, majibu,
Dkt. Msonde anasema, “Watahiniwa wetu 265 walibainika pasi na shaka kufanya udangajifu katika mitihani hii. Wapo watahiniwa 123 waliokamatwa na simu, notes, vitabu ama kwa ujumla wake vitu visivyohitajika ndani ya vyumba vya mitihani wakati akiendelea”,
“Wako pia watahiniwa 62 ambao walikuwa wanabadilishana script, walikuwa wanabadilishana namba na wengine kubainika kuwa na miandiko tofauti kwenye script zao. Watahiniwa 73 waliobainika kuwa na majibu ya kukosa yasiyo ya kawaida yenye mfanano usio wa kawaida”.
Amesema walikuwepo watahiniwa wengine ambao walifanyiwa mitihani na watu wengine ambao hawakuandikishwa kufanya mtihani, lakini walikamatwa kwa sababu kila mtahiniwa ana picha inayomtambulisha.
“Tulikuwa na watahiniwa wengine saba waliokuwa wakifanyiwa mitihani na watu wengine mamluki wengine wako nyumbani lakini wamekodi watu wakafanyie mitihani yao.
Watahiniwa wanapofanya mitahani kuna picha zao ziko pale kwa hiyo ukimleta mtu mwingine ambaye hafananii, hawa walikamatwa na wasimamizi”, amesema Dkt. Msonde.
Akitoa mfano wa udanganyifu uliofanyika katika baadhi ya vituo amesema, “Katika shule ya Alfarik Seminary hiki ni kituo kiko Dar es Salaam mtu anayejiita Zuberi Mabula alikamatwa na msimamizi ndani ya chumba cha mtihani akimfanyia mtahiniwa Silvanus Prince Mjengwa”.
Anabainisha kuwa yapo baadhi ya matukio yamejitokeza mwaka huu hayajawahi kujitokeza wakati mwingine wowote ambapo ameshangazwa na ujasiri wa watuhumiwa hao.
“Watahiniwa mwaka huu walianzisha kitu ambacho sio cha kawaida watu wanapanga utaratibu wa kwenda kuwafanyia mitihani watu wengine lakini wanajiorodhesha na wenyewe kwenda kufanya mitihani”,
“ Kwa hiyo tumefikia hapo, tulikuwa na kundi la watahiniwa 27 wa kituo cha Mwalasi walijiandikisha kufanya mitihani katika jozi na walipoingia kwenye chumba cha mtihani mmoja anaandika namba ya mwenzie anayemfanyia mitihani na yule anayefanyiwa mtihani anaandika ya mwingine”, amesema Dkt. Msonde.
Baraza hilo limewafutia matokeo 265 kwa udangajifu huo ambapo 136 ni wale wa kujitegemea na 129 wa shule.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni