Licha ya idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mitandao ya majitaka katika miji mikuu kuongezeka, ni asilimia 20 tu ya wananchi katika miji hiyo wanafikiwa na huduma hiyo nchini na kuwaweka katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.
Miji mikuu 10 ambayo imeunganishwa kwenye mitandao wa majitaka ni Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Tabora, Moshi, Tanga, Songea na Iringa ambapo serikali imeendelea kufanya maboresho ya miundombinu ili kuhakikisha wateja wengi zaidi wanaunganishwa kwenye huduma hiyo.
Kulingana na hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa wakati huo Eng. Gerson Lwenge aliyoitoa kwenye bunge la bajeti ya mwaka 2017/2018 alisema “Idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mitandao ya majitaka katika miji hiyo imeongezeka kutoka 25,361 mwezi Machi, 2016 hadi kufikia wateja 26,636 mwezi Machi, 2017 na kuweza kupunguza kero ya majitaka kutiririka hovyo katika miji hiyo”.
Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mtandao wa majitaka imeongezeka kutoka 18,436 mwezi Machi, 2016 hadi kufikia wateja 19,034 mwezi Machi, 2017.
Kwa muktadha huo huduma ya uondoaji majitaka katika miji hiyo ikijumuisha Jiji la Dar es Salaam imefikia asilimia 20.
Matarajio ya wizara ya Maji na Umwagiliaji ni kuongeza huduma ya uondoaji majitaka kutoka asilimia 20 ya sasa hadi kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020.
Mabomba yakimwaga majitaka kwenye mto
Licha ya juhudi hizo za serikali,
changamoto inabaki kwa jiji la Dar es Salaam ambalo idadi ya wakazi wake
inaongezeka kwa kasi na kwamba lina uhitaji mkubwa wa huduma hiyo ili
kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama dhidi ya majitaka yanayotiririka
katika mitaa mbalimbali.
Kulingana na Mamlaka ya Maji
Dar es Salaam (DAWASCO) inaeleza kuwa mfumo
wa majitaka katika jiji la Dar es Salaam ni mkusanyiko wa
mifereji ambayo hukusanya maji kutoka katika maeneo mbalimbali kwa
kutumia pampu zilizofungwa katika vituo 15 ambazo huyaelekeza maji hayo
katika mabwawa.
Eneo linalopata huduma hiyo ni kilomita
170 ambalo limetandazwa mabomba yenye kipenyo cha milimita 100 hadi 100 ambapo
maeneo ya katikati ya jiji, Kariakoo, Upanga na Muhimbili humwaga maji yake
moja kwa moja katika bahari ya Hindi.
Eneo linalopata huduma hiyo ni dogo
ikilinganishwa na ukubwa wa jiji hilo ambalo unafikia kilomita za mraba 1,393.
Ni dhahiri kuwa eneo kubwa lililobaki limezungukwa na majitaka ambayo
huchanganyika na maji ya visima yanayotumiwa na wananchi wengi wa jiji hilo na
kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Moja ya njia kubwa ambayo inaweza
kueneza magonjwa kama kipindupindu ni matumizi ya maji machafu. Maji machafu
yanaweza kuwa ya visima au bomba ikiwa hayawekwi dawa kuua vijidudu au
kuchemshwa kabla ya kutumika.
Dar es Salaam inatajwa kuongoza
kukumbwa na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu kuliko maeneo
mengine nchini.
Hali hiyo inatokana na jiji hilo kuwa na idadi kubwa ya visima
vyenye vimelea ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa ya milipuko hasa
kipindupindu na homa za matumbo.
Kipindupindu ni ugonjwa
unaoambukizwa kupitia maji au chakula chenye vimelea ambavyo kitaalamu
hujulikana kwa jina la ‘Vibrio Cholerae.’ Vimelea hivi huishi katika maji
yaliyochafuliwa hasa yenye kinyesi.
Maeneo ambayo huathirika zaidi na
majitaka ni Buguruni, Kigogo, Tandale, Kariakoo, Manzese na Yombo ambayo
hutegemea zaidi maji ya visima virefu kama mbadala wa huduma za Dawasco, lakini
visima hivyo havina maji salama.
Hili linathibitishwa na kauli ya
Waziri wa Maji na Umwagilia wa wakati huo, Mhandisi
Gerson Lwenge wakati wa bunge la
bajeti 2016/2017 alipoelezea kuhusu uchunguzi wa visima 108
ambapo visima 66 vilikuwa sio salama na maji yake yalikuwa na vimelea vya
ugonjwa wa kipindupindu. Visima virefu vilikuwa 40 na vifupi ni 26.
Utafiti wa Chuo Kikuu cha Ardhi,
unaonesha maji ya visima vingi sio salama na kushauri wachimba visima kupata
ushauri wa kitaalamu ili kuepusha jamii na magonjwa kwa kutumia maji yasiyokuwa
salama.
Kufikia Septemba 2016, Dar Es Salaam
ilikuwa na visima virefu 676 huku Wilaya za Temeke na Ilala zikiongoza kutokana
na kutofikiwa na maji ya DAWASCO. Kinondoni, kwa kuwa na mtandao mkubwa wa maji
ya Dawasco, hali ya kipindupindu sio mbaya.
Ni dhahiri kuwa mamlaka husika
zinapaswa kutazama upya mfumo wa majitaka na kuboresha miundombinu iliyopo ili
kuwafikia watu wengi zaidi katika nyumba zao.
Pia elimu iendelee kutolewa kwa
wananchi juu ya umuhimu wa kutumia mfumo rasmi wa kutibu majitaka ili
kujiepusha na athari za kiafya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni