Na Charles Ndagulla,Moshi.
HAYAWI HAYAWI YAMEKUWA,baada ya
kusota mahabusu kwa siku 17,hatimaye mtumishi wa mfuko wa Pensheni kwa
watumishi wa (PPF),Anitha Osward Ichwekeleza(32),anayetuhumiwa kujihusisha na
usafrishaji wa dawa za kulevya,amefikishwa mahakamani mjini moshi.
Mtumishi huyo wa umma,alikamatwa
desemba 19 mwaka jana akiwa na shehena ya madawa ya kulevya aina ya mirungi
aliyokuwa akiisafrisha kwa kutumia gari lake dogo aina ya Toyota Sienta lenye
namba za usjaili T674DLB.
Anitha alifikishwa katika makahama
ya hakimu mkazi mjini Moshi chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za
moto akitokea kituo cha polisi Majengo mjini hapa ambako kwa muda wote tangu
akamatwe alikuwa akishikiliwa huko.
Baada ya kufikishwa hapo
alishikiliwa kwa muda nje ya mahakama kabla ya kupandishwa kizimbani na kusomewa shitaka moja la uhujumu
uchumi mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi,Aidan Mwilapwa.
Alisomewa shitaka hilo na wakili wa serikali
Agatha Pima na kutokana na shitaka hilo kuwa ni la uhujumu uchumi na mahakama
hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya aina hiyo hadi mahakama kuu,mshitakiwa huyo
hakutakiwa kujibu chochote.
Mshitakiwa huyo ambaye kwenye hati
ya mashitaka ametambulishwa kama mtumishi wa umma,ameshitakiwa kwa kosa moja la
kusafrisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 15(b) cha sheria namba 5 ya
mwaka 2015 ya udhibiti wa usafrishaji wa
dawa za kulevya kama ilivyofanyiwa marejeo madogo na sheria namba 23 ya mwaka
2016.
Kwa mujibu wa hati ya
mashitaka,mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa,mnamo desemba 19 mwaka jana huku Majengo
kwa Mtei Manispaa ya Moshi,mshitakiwa alikutwa akisafrisha kilo 216.37 za dawa
za kulevya.
Baada
ya kusomewa shitaka hilo,mshitakiwa huyo alipelekwa mahabusu katika Gereza Kuu
la Mkoa,la Karanga ambako sasa ameenda kuanza maisha mapya ya gerezani,shauri
hilo litakuja kwa ajili ya kutajwa tena mahakamani hapo Januari 19 mwaka huu. 

HIVI
NDIVYO ALIVYONASWA NA SHEHENA YA DAWA ZA KULEVYA
Anitha alikamatwa na askari wa jeshi la polisi
waliokuwa doria baada ya kupenyezewa taarifa na raia wema kuwa mtumishi huyo wa
umma alikuwa amebeba ‘mzigo’ akitumia gari lake binafsi ambalo kulingana na
sheria,kama atapatikana na hatia,gari hilo litataifishwa na serikali .
“Askari wakiwa doria walimkamata
Anitha Oswald, ambaye ni mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa
anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370”, alisema
kamanda Issa.
Kamanda Issa alisema Anitha Oswald
alikamatwa eneo la Majengo kwa Mtei Disemba 19, mwaka jana, akiwa anatokea Njia
Panda ya Himo kuchukua mzigo huo.
Aidha kamanda Issa alisema kwamba
usafirishaji wa dawa za kulevya bado ni changamoto kubwa ambapo alielezea
kusikitishwa na tabia ya baadhi ya watumishi wa Umma kujihusisha na
usafirishaji huo.
“Jeshi la polisi mkoani hapa liko
makini, operesheni inaendelea na hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kujihusisha
na biashara hii”, alisema.
Hata hivyo kamanda aliongeza kusema
kwamba jeshi hilo la polisi mkoani kilimanjaro, bado linaendelea kumtafuta
dereva wa gari hilo, ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza gari alilokuwa
akiliendesha baada ya kugonga mti katika jitihada za kuwakimbia polisi.
PICHA MBALI MBALI ZIKIMUONYESHA ANITHA OSWARD ALIVYONASWA NA DAWA ZA KULEVYA
Mtuhumiwa wa dawa za kulevya,Anitha Osward(32)akiwa chini ya ulinzi wa polisi huku akiwa amesimama mbele ya gari lake aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674DLB huku shehena ya dawa za kulevya ikiwa ndani ya gari lake.
Shehena ya dawa za kulevya iliyokamatwa na polisi mjini moshi ikisafrishwa na mtumishi wa mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma(PPF),Anitha Osward,tayari mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani .
Gari la mtuhumiwa wa dawa za kulevya Anitha Osward aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB likivutwa baada ya kugonga mti katika jitihada za mtuhumiwa huyo kuwakimbia polisi.
gari aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB linalomilikiwa na mtumishi wa mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma(PPF)Anitha Osward likiwa limesheheni shehena ya dawa za kulevya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni