Ijumaa, 2 Februari 2018

NABII TITO AMWIMBUA ASKOFU SHOO, AKUMBUSHIA YA KIBWETERE


Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo, ameonya kuwa watu wakichanganyikiwa kwa mambo ya kiroho, madhara yake ni makubwa.

Askofu Shoo ametolea mfano wa mwaka 2000 ambapo Askofu Joseph Kibwetere wa Uganda, aliwaangamiza wafuasi wake 1,000 kwa moto baada ya kuwaaminisha kuwa mwisho wa dunia umefika.

Mkuu huyo wa kanisa ametoa kauli hiyo kufuatia kile alichosema kuongeza kwa mafundisho potofu ya dini ya kikristo, na kuipongeza Serikali kwa kumdhibiti aliyejiita Nabii Tito mkoani Dodoma.

Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo, alitaka taratibu za usajili wa makanisa na taasisi za dini utizamwe upya, ili kuepusha jamii kupokea mafundisho potofu.
 “Ndio maana kwa muda mrefu tumesisitiza (Serikali) watafute maoni ya mabaraza ya makanisa kabla ya kuruhusu kila mtu anayejisikia kuanzisha kanisa lake anafanya hivyo,”alisema na kuongeza;-

“Watu wakichanganyikiwa kwa mambo ya kiroho madhara yake sio kwa kanisa tu bali ni kwa jamii nzima inayopokea mafundisho hayo potofu. Chukua mfano wa Kibwetere wa Uganda”.

Kauli ya Askofu Shoo imekuja wakati polisi mkoani Dodoma wakiendelea kumshikilia Tito Machibya maarufu kwa jina la Nabii Tito, kwa madai ya kujenga chuki dhidi ya dini za watu wengine.

Kabla ya kukamatwa kwake “Nabii Tito”, alionekana katika mitandao ya kijamii, akitoa mafundisho ya dini ya kikristo, ambayo baadhi ya watu na Serikali wameyatafsiri kuwa amfundisho potofu ya kidini.

Polisi kupitia kwa kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroro wanadai daktari wa hospitali ya Mirembe mkoani humo, wamethibitisha kuwa “Nabii Tito” ana matatizo ya kiakili.

Lakini wakati polisi wakishughulika na Nabii Tito, kumeibuka wimbo kubwa la uanzishaji wa makanisa, ambapo baadhi ya wanayoyaanzisha hujivika vyeo vya Utume au Unabii wao na wenza wao.

Mbali na kujikita katika mafundisho ya ajabu ajabu, baadhi ya makanisa hayo yanadaiwa kujiendesha kibiashara badala ya kuhibiri Injili, huku mengine yakienda mbali na kupanga viwango vya sadaka.

Hivi karibuni, Naibu Askofu wa kanisa katoliki Jimbo la Moshi, Padre Deogratius Matiika aliliambia gazeti hili  kuwa, ujio wa makanisa mapya na wanaojiita Mitume, umekuja na changamoto na kero.
 “Baadhi wanaishi maisha ya anasa na wana utajiri mkubwa wakati miongoni mwa washirika wao kuna watu hawajui hata watakula nini baada ya kutoka ibadani na hawafahamu watasaidiwa vipi,”alisema.

Padre Matiika alisema kuwa yapo baadhi ya makanisa mengi yanatumia nguvu za giza kuwatapeli waumini wao kuwa wanaponya na kufufua watu waliokufa,hali ambayo inawagharimu waumini.

“Unakuta muumini anaambiwa alete picha ya marehemu iombewe ili afufuke na anapoileta ni lazima iambatanishwe na fedha. Huo ni utapeli mkubwa na haukubaliki,”alisema Matiika.

“Kumtolea Mungu sadaka hupangiwi unatoa kile ambacho mfukoni mwako unaoana ni chenye kumpendeza Mungu na sio kupangiwa kutoa sadaka,”alisisitiza Padre Matiika.

Padre Matiika aliiomba Serikali kuweka mwongozo na mikakati maalumu kwa makanisa ili kuepukana na kuongezeka kwa makanisa mengi ya uongo ambayo yanapotosha waumini wa leo.


Chanzo:Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni