Rais wa Ujerumani, Joachim
Gauck, anaendelea na ziara yake nchini Tanzania, ambapo leo atatembelea
visiwani Zanzibar, na kufanya mazungumzo na Rais Ali Mohamed Shein.
Katika kukamilisha siku ya
kwanza ya ziara hiyo jana usiku, Rais Gauck alikula chakula cha jioni
alichoandaliwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika Ikulu ya Dar
es Salaam.
Gauck ameyasifu maendeleo ya
kisiasa na kiuchumi ya Tanzania, ingawa amesema bado mengi yanapaswa kufanyika
ili kuwawezesha wananchi wa kawaida.
Amerejelea mtazamo wa Ujerumani
kwa Tanzania kama taifa la Afrika Mashariki linaloinukia kwa kasi kiuchumi,
hatua ambayo amesema inachangiwa na uwepo wa amani na utulivu wa kisiasa.
Aidha, Rais Kikwete ameitaka
Ujerumani kuimarisha uwekezaji wake kwenye sekta kadhaa zinazokuwa nchini
Tanzania, hasa katika soko la utalii ambalo tayari Ujerumani imeonyesha
muelekeo mzuri.
Ziara hiyo itamfikisha Gauck hadi mkoani Arusha.