Jumatatu, 5 Februari 2018

TAPELI ANAYEISHI KWA KUTUMIA MAJINA YA VIONGOZI MBARONI


Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limemtia mbaroni mkazi wa wilaya ya Mwanga, aliyekuwa akisakwa kwa udi na uvumba kwa kutumia majina ya viongozi kutapeli fedha kwa njia ya mtandao.
Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Koka Moita, alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa kutumia jina la aliyekuwa mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Said Mecki Sadick kutapeli fedha.
Kaimu kamanda huyo alisema ingawa mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 28 kwa tuhuma za kuiba shehena ya viazi huko Tarakea wilayani Rombo, lakini alikuwa akitafutwa kwa tuhuma za utapeli.
“Anatuhumiwa kuiba viazi funzo nzima huko Tarakea Rombo lakini tulikuwa tunamtafuta kwa impersonation (kujifanya) yeye ni Said Mecki Sadick aliyekuwa mkuu wa mkoa wakati siye,”alisema.
Moita alisema mtuhumiwa huyo, Hassan Omary Kashingo, anashikiliwa kituo kikuu cha polisi Moshi na kuwataka wananchi ambao walifungua taarifa juu yake, wafike ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Desemba 15,2015, aliwahi kukamatwa na Polisi kwa tuhuma za kutumia jina la aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi , sasa ni mwenyekiti wa bodi ya chuo cha Diplomasia, Balozi Ombeni Sefue kutapeli.
Wakati akikamatwa, tayari kulikuwa na majalada zaidi ya nane ya utapeli katika kituo cha kati mjini Moshi, na haijulikani ilikuwaje hakurejeshwa Moshi kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kumbukumbu za Polisi, zinaonyesha kuwa mtuhumiwa huyo anatumia majina tofauti tofauti ya Hassan Abdalah au “Golota”, Yusuph Mjema au “Kashingo”, na majina mengi ambayo hayajabainika.
Novemba mwaka jana mtuhumiwa huyo anadaiwa kutumia jina Sadick kutapeli fedha kutoka kwa viongozi mbalimbali wa umma, dini na wananchi wa kawaida, akijitambulisha kuwa ni Sadick.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alitangaza Jeshi hilo kumsaka kwa udi na uvumba mtuhumiwa huyo kwa tuhuma mbalimbali za utapeli akisajili laini ya Sadick.
Kwa upande wake, mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Said Mecki Sadick  alilithibitishia gazeti hili mwaka jana, kupokea taarifa za kuwepo kwa mtu anayetumia jina lake kutapeli na kwamba tayari ameripoti polisi.
Mtuhumiwa huyo ndiye ambaye Desemba 4, 2015, alimpigia mhadhiri mmoja wa chuo kikuu cha St. John cha mjini, na kujifanya yeye ni Balozi Sefue, na kwamba ana shida.
Katika maongezo hayo, mtuhumiwa huyo ambaye ni mhitimu wa darasa la saba, alimuomba Profesa huyo  amtumie mtoto wake Sh500,000 ambaye amepata dharura akiwa mkoani Singida.
Hata hivyo ilibainika baadae kuwa mtu huyo hakuwa Balozi Ombeni Sefue na ndipo DCI alipounda kikosi kazi kilichopiga kambi mkoani Kilimanjaro na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumia huyo.
Mtuhumiwa huyo ndiye anayetuhumiwa  kati ya mwaka 2013 na 2015, alitapeli viongozi mbalimbali kwa kutumia jina la mwandishi mwandamizi wa habari wa mkoa wa Kilimanjaro, Daniel Mjema.
 Chanzo:Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni