Jumamosi, 19 Mei 2018

RUSHWA YA NGONO YATIKISA ARUSHA SERENA HOTEL Arusha Serena Hotel,Resort and Spa
 

 NA CHARLES NDAGULLA,ARUSHA

RUSHWA  ya ngono ni moja ya vitendo ambavyo vimekuwa vikiwakwaza wanawake katika  kupata ajira maeneo mbali mbali duniani hatua ambayo inatajwa kama moja ya changamoto kubwa katika mafanikio yao.

Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo,wapo baadhi yao ambao licha ya kuwa na sifa za kuajiliwa wamejikutaka wakikosa fursa hizo kutokana na kushindwa kutoa rushwa ya ngono kwa wanaosimamia mamlaka za ajira.

Pamoja na  kelele ninyi kupigwa kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu yakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali  juu ya kukithiri kwa vitendo hivyo,mambo bado yahajabadilika katika baadhi ya maeneo ya kazi hapa nchini.

Wafanyakazi wa kike katika Hotel ya kitalii ya Arusha Serena Hotel and Resort iliyopo kilometa 4.5 kutoka eneo la Tengeru nje ya Jiji la Arusha ni moja ya wahanga wa matukio hayo ya unyanyasaji wa kingono.

Wafanyakazi hao walioomba kutotajwa majina yao kwa sababu maalumu,wamezungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha na kuelezea kilio chao juu ya vitendo hivyo ambavyo wanadai vinawakwaza katika utendaji kazi wao.

  
Kwa mujibu wa wafanyakazi hao,wamedai wengi wa wanaonyanyasika ni wafanyakazi wa kitanzania huku wafanyakazi kutoka nchini Kenya wakipewa huduma nzuri ikiwamo mishahara minono na maslahi mengine.
 Ndagullablog imezungumza na meneja Raslimali watu wa hotel hiyo John mwamakula juu ya malalamiko ya wafanyakazi hao kunyanyaswa kingono na baadhi ya maofisa wa hotel hiyo akiwamo meneja wake Filex Ongembo.

Katika mahojiano na Ndagullablog ofisini kwake wiki hii,Mwamakula hakukiri wala kukanusha malalamiko hayo huku akisisitiza vitendo hivyo ni kinyume na sera ya hotel hizo.

Amesema sera ya hotel hizo zilizopo maeneo mbali mbali nchini inakataza vitendo hivyo na kwamba anayebainika kufanya hivyo anakuwa katika hatari ya kufukuzwa kazi.

Mwamakula amesema kuwa hawajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi hao kunyanyaswa kingoni lakini akadai zipo njia tatu kwa wafanyakazi hao kuwasilisha malalamiko yao kwa uongozi.

Ametaja njia hizo kuwa ni pamoja na utoaji taarifa kwa njia ya siri(wisow blower),mfanyakazi kwenda moja kwa moja ofisini kwake na kupitia mikutano ya wafanyakazi(Staff General Meeting) ambayo amedai hufanyika kila baada ya miezi mitatu.

“Kwa ujumla hatukubaliani na hivyo vitendo na hata ukiangalia sera yetu inakataza vitendo hivyo na adhabu yake ni kali sana kama ikibainika mtu amehusika na vitendo hivyo tunamfukuza kazi”,amesema.

Hata hivyo meneja huyo alipoulizwa alipo Ongembo amesema hajui alipo zaidi ya kusema hayupo na taarifa ambazo jamhuri limezipata ni kwamba meneja huyo amerejeshwa nchini kwao Kenya.

Malalamiko mengine ya wafanyakazi hao ni kupunguzwa kwa mishahara yao kwa aslimia tano tangu mwaka jana na meneja huyo amekiri kuwepo na punguzo hilo la mishahara kwa wafanyakazi hao.

Akijibu malalamiko hayo,Mwamakula amesema kuwa,makato hayo yalitokana na kuyumba kwa biashara ya utalii mwaka jana madai ambayo wafanyakazi hayo wameyapinga.

 Huduma ya matibabu ni moja ya malalamiko mengine kwa watumishi ambako wanadai mwajili wao kuwaondoa kwenye huduma ya matibabu kupitia bima ya Afya(NHIF) huku wakitibiwa kupitia bima ya Jubilee ambayo wamedai haiwapi nafasi ya kwenda kutibiwa katika hospital za rufaa.

Wametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kutopewa usafiri wa kutoka nyumbani kwenda kazini na kurudi majumbani hali ambayo imewalazimu kutumia zaidi ya shilingi 10,000 kwa siku kama gharama za usafiri fedha ambazo wanadai zinazotoka kwenye sehemu ya mishahara yao.

Licha ya kutopewa usafiri,wafanyakazi hao wamedai kuwa usalama wao uko shakani kutokana na kutumia usafiri wa boda boda usiku wa manane wakati wa kutoka kazini kutokana na boda boda wengi kutowafahamu.

“Tunaomba mtusaidie kwa kweli hali ni mbaya,wafanyakazi wa kitanzania tunanyanyasika sana tofauti na wenzetu wakenya ambao wanaishi vizuri licha ya baadhi yao kutokuwa na hadhi ya kufanyakazi ambazo tunauwezo nazo”,wamesema.

Hata hivyo wafanyakazi hao wamedai  kuwa,wamekuwa katika tishio la kufukuzwa kazi pindi wanapodai kuboreshewa mazingira ya kazi hatua ambayo imewafanya baadhi yao kukaa kimya kwa hofu ya kufukuzwa kazi.

Wafanyakazi hao wameitaka wizara ya kazi,ajira na vijana  pamoja na idara ya uhamiaji Jijini Arusha kufanya uchunguzi wa kina kwa baadhi ya wafanyakazi wa hotel hiyo kutoka nchini Kenya kwani baadhi yao hawana sifa za kufanyakazi hapa nchini.

“Ukienda pale ofisi kuu utawakuta wakenya wamejazana pale wengine hawana sifa za kuwa hapa nchini kwa sababu baadhi ya kazi wanazofanya hazihitaji watu kutoka nje ya nchi,wapo wanafanyakazi kama makatibu mhitasi,je kazi hiyo inahitaji mtu kutoka Kenya?,wamehoji.

  Kuhusu suala la matibabu,Mwamakula amesema kuwa si kweli bima ya Jubilee inawanyima fursa ya kutibiwa katika Hospital za rufaa huku akikiri kujiondoa katika Bima ya Afya ya NHIF.

“Mpango wetu wa matibabu unagusa mfanyakazi na mwenza wake kama ameoa ama kuolewa na watoto wasiozidi wanne wenye umri chini ya miaka 18”,amesema.

Amesema wafanyakazi hao pia ni wanachama wa mfuko wa hifadhi ya Jamii (NSSF) ambako kuna  mpango wa matibabu kupitia fao la matibabu ambako mwanachama anaweza kujiandikisha bila kuathiri michango yake na akachagua Hosptil anayoitaka.

Mbali na huduma hizo,meneja huyo amesema wafanyakazi hao wanayo bima nyingine ambako matibabu yakishindikana hapa nchini wanaweza kupelekewa nchini Kenya kwa matibabu zaidi.

Jumatatu, 14 Mei 2018

HAKUNA UGONJWA WA EBORA NCHINI,ASEMA MKUU WA MKOA WA SONGWE,CHIKU GALLAWA


Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa  amewatoa wasiwasi wananchi wa mkoa huo kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao umeuikumba nchi ya jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC).

Mkuu  wa Mkoa huyo amesema hakuna tukio lolote la kuwepo kwa ugonjwa huo katika mkoa wake lililoripotiwa lakini amewataka wananchi hao kuchukua tahadhari za kiafya ili kujikinga na maambukizi yoyote yanayoweza kutokea.

Mkoa wa Songwe unapatikana Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania na unapakana na nchi ya Zambia ambayo ina muingiliano wa karibu na wananchi wa Congo DRC.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe magufuli,akimwapisha mkuu wa mkoa wa Songwe,Chiku Gallawa Ikulu Dar es salaam mwezi machi mwaka 2016.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa mkoa wa Songwe umeimarisha ukaguzi katika kituo chake cha mpakani cha Tunduma kilichopo wilaya ya Momba.

“Tunaimarisha kituo cha kupokea wageni mpakani mwa Tunduma na Zambia, watakaogulika kuwa na tatizo hilo watahifadhiwa eneo maalum  kwaajili ya uangalizi na tiba,” amesema Galawa.

Kwa mujibu wa Galawa akinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema ugonjwa huo uliolipuka Congo DRC umeua watu 17 na mpaka sasa kuna wagonjwa 21 katika vituo maalum vya matibabu.

Hata hivyo, Kamati ya ulinzi na usalama katika wilaya ya Momba inakutana na uongozi wa Wilaya ya Nakonde ya nchi jirani ya Zambia ili kuweka mikakati ya ukaguzi mpakani mwa nchi hizo mbili na kuhakikisha wageni wanaoingia na kutoka hawasambazi virusi vya ugonjwa huo.

Tanzania inachukua tahadhari ya ugonjwa huo ikizingatiwa kuwa imekuwa na mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara ya muda mrefu na Congo DRC ambayo yanaunganishwa zaidi na usafiri wa bandari ya Dar es Salaam, Reli ya TAZARA  na mtandao wa barabara.

Miundombinu hiyo ya usafiri imekuwa kiungo muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa kutoka bandari ya Dar es Salaam ambazo zimekuwa zikisafirishwa kwa malori ambayo yanapita nchi ya Zambia na kuingia Congo DRC. 

Pia DRC imekuwa ikisafirisha madini yake kwenda nchi za ng’ambo kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Kutokana na mahusiano hayo ya karibu ni rahisi  kwa virusi vya ebola kusambaa kwa haraka katika nchi za jirani ikiwemo Tanzania.

Kinachoendelea Congo DRC

Kwa taarifa zilizopo, tayari watu 17 wamefariki kutokana na ugonjwa wa virusi vya Ebola katika mji wa Bikoro uliopo  Kaskazini Magharibi mwa Congo DRC. Ebola ni ugonjwa unaotokea katika kipindi fulani na kuua watu wengi kwa muda mfupi.

Ni hatua gani ambazo Congo DRC inapaswa kuchukua wakati huu?

Mamlaka za afya nchini humo tayari zimejifunza masomo ya msingi kutokana na  milipuko ya ugonjwa huo iliyowahi kutokea mwaka 2014 hasa katika nchi za Afrika Magharibi ambapo zaidi ya watu 11,000 walikufa.

Kwa sababu Congo RDC imekumbana na milipuko ya ugonjwa huo siku za nyuma imeimarisha uwezo wake wa kukabiliana na maambukizi mapya.

Lakini kama ilivyo kwa magonjwa mengine ambayo yanatishia afya ya dunia, ni muhimu kwa nchi za jirani kushirikiana kuhakikisha mlipuko huo unadhibitiwa mapema kabla haujasambaa katika eneo kubwa.

 Mgonjwa mwenye maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Ebora akipatiwa tiba.

Kwanza, mamlaka za afya zinatakiwa kubaini ukubwa wa tatizo. Pili wanatakiwa kuingilia kati na kuvunja mnyororo wa maambukizi haraka iwezekanavyo.

Taarifa za mtandao wa Quartz Afrika zinaeleza kuwa tayari wametuma wataalamu ili kufahamu lini na wapi ambako watu wameathirika zaidi, wapi walipotoka au kusafiri tangu waathirike.

 Uchambuzi huo utasaidia kuelewa kiasi cha maambukizi kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Baada ya zoezi hilo kukamilika, serikali itachukua hatua stahiki. Hatua mbalimbali za kudhibiti zitaanzishwa haraka ikiwemo kuzuia na matibabu. Katika mtazamo wa kuzuia ni vema serikali ikashirikiana na jamii ili watu waelewe mlipuko wenyewe  na jinsi unavyosambaa.

Kwa mtazamo wa matibabu, mamlaka za afya zinatakiwa kujenga vituo vya matibabu na upatikanaji wa maabara za vipimo. 

Kulingana na kiwango cha vifo, wataalamu watafanya uchunguzi wa kina ili kubaini chimbuko la mlipuko wa Ebola.

 Hii ndiyo njia pekee ya kuvunja mnyororo wa maambukizi.

Changamoto zinazokwamisha udhibiti wa virusi vya ugonjwa huo nchini Congo DRC

DRC imekuwa na milipuko mingi  ya Ebola kuliko nchi yoyote duniani. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kumekuwa na milipuko 5: 2007, 2008 hadi 2009, 2012, 2014 na 2017.

Matokea yake nchi hiyo imepata uzoefu wa kutosha  jinsi ya kudhibiti ugonjwa huo.  Lakini bado kuna sintofahamu. Moja ya pengo kubwa ni kuelewa mabadiliko ya maambukizi ya virusi kutoka kwa wanyama walioathirika hadi kwa binadamu.

Nchi hiyo ina mfumo mzuri wa kushughulika na ugonjwa huo-maabara zake zilikuwa na uwezo wa kupima na kuthibitisha kesi za virusi ndani ya saa 24. 

Lakini mifumo yake ya uchunguzi na ufuatiliaji  ni dhaifu,mifumo imara ya uchunguzi ingehakikisha kesi zinaripotiwa mapema na mamlaka husika zinakuwa tayari kukabiliana nazo.

Chanzo:FikraPevu

Jumatatu, 7 Mei 2018

BASTOLA ILIYOPORWA MOSHI YATUMIKA KUUA MLINZI SHAMBA LA MKONGE KOROGWE


 JESHI  la polisi mkoani  Tanga limefanikiwa kuwatia mbaroni watu wanne akiwamo mwanamke mmoja mkazi wa Kigogo Jijini Dar es salaam wakituhumiwa kuhusika ma mauaji ya mlinzi wa shamba la Mkonge la Kwa Mduru lililopo wilaya ya Korogwe .

Katika tukio hilo,mlinzi wa shamba hilo,Omar Athuman aliuawa kwa kupigwa risasi huku meneja mkuu wa Shamba hilo ambaye ni raia wa Kigeni,Mathias Hendrik akijeruhiwa vibaya sehemu mbali mbali za mwili wake.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga,Kamishna Msaidizi  Mwandamizi wa polisi(SACP),Edward Bukombe,amezungumza na Ndagullablog na kueleza  kuwa katika tukio hilo,majambazi hao mbali na kuua,kujeruhi,pia walipora vitu mbali mbali zikiwamo,pesa,simu .

Waliokamatwa kuhusiana na tukio hjilo ni Ebeni Venance Mwaipopo(27)mkazi wa Ngarenairobi mkoani Arusha,Fredrick Menadi(46) mkazi wa Chekereni ya Bonite mjini Moshi,Diana Godliving(24)na Dismas Venance Mwaipopo,wote wakazi wa Dar es salaam.

“Katika tukio hilo,watuhumiwa hao walitumia silaha ya moto kufanikisha uporaji huo ambako walimuua mlinzi wa shamba hilo,wakamjeruhi mwenzake lakini meneja mkuu wa shamba hilo naye alijeruhiwa vibaya”,amesema kamanda Bukombe.

Habari kutoka wilayani Korogwe zinadai kuwa,kutokana na meneja huyo kupata majereha makubwa sehemu mbali mbali za mwili ,kwa sasa yuko nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi.

Akizungumza na Ndagullablog ofisini  kwake hivi karibuni,kamanda Bukombe alisema uchunguzi wa polisi umebaini kuwa silaha iliyotumika katika tukio hilo la mauaji ya mlinzi huyo iliibwa mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa kamanda Bukombe,Bastola hiyo aina ya Norinco Star,ni mali ya mfanyabiashara Denis Swai mkazi wa Soweto katika Manispaa ya Moshi  mkoani Kilimanjaro.

Ndagullablog imezungumza na Swai ambaye amekiri kuwa Bastola hiyo ni mali yake na kwamba tayari ameshaitwa na ofisi ni Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai(RCO) mkoa wa Tanga kwa ajili ya utambuzi.

“Kama ulivyopata taarifa kwa RPC wa Tanga ni kweli hiyo bastola ni mali yangu na hivi karibuni niliitwa na RCO kwenda kuitambua na nimejiridhisha kuwa ni mali yangu japo imefutwa namba”,amesema Swai.

Mfanyabiashara huyo amesema kuwa,bastola hiyo iliibwa na watu wanaaminika kuwa ni majambazi baada ya kuvamia nyumbani kwake eneo la Soweto mwezi julai mwaka jana ambako licha ya kuiba bastola hiyo waliiba na vitu vingine.

Kwa mujibu wa Swai,majambazi hao wakiwa na silaha za moto waliiba pia seti moja ya TV aina ya Sony yenye ukubwa wa inchi 40 ikiwa na thamani ya shilingi milioni 1.2,pete ya ndoa ya mke wake na pesa taslimu zaidi ya paundi 20,000 za Uingereza.

Hata hivyo mfanyabiashara huyo amsema kuwa wakati tukio hilo linatokea yeye hakuwepo nyumbani kutokana na kuwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) ambako alikuwa akipokea wageni wake kutoka nchini Marekani.

“Kama ningekuwa nyumbani siku hiyo basi lolote ningeweza kutokea nap engine leo nisingekuwa hai maana kwa jinsi walivyoingia nyumbani ni  hakika walikuwa wamejipanga kwa lolote”.amesema.

Wakati bastola yake ikipatikana baada ya kuhusika katika tukio la mauaji huko Korogwe mkoani Tanga,seti yake ya TV ilipatikana kwa mmoja wa watuhumiwa hao wa mauaji ,Fredrick Menadi eneo la Chekereni ya Bonite mjini Moshi.

WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MAUAJI YA MLINZI

Wakati huo huo,watuhumiwa hao wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mfawidhi wa wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wakikabiliwa na shitaka moja la mauaji ya mlinzi wa shamba hilo la Mkonge la Kwa Mduru.

Waliofikishwa mahakamani mbele ya hakimu mfawidhi Kassim Kwawa ni,Ebeni Venance Mwaipopo(27)fundi na mkazi wa Ngarenairobi mkoani Arusha na Fredrick Menadi (46) boda boda mkazi wa Chekereni ya Bonite mjini Moshi.

Wengine ni Diana Godliving binti wa miaka 24 na mkazi wa Kigogo Jijini Dar es salaam pamoja na Dismas Venance Mwaipopo pia mkazi wa Dar es salaam anayetajwa kuwa ni baba mzazi wa mshitakiwa wa kwanza.

Washitakiwa hao  walisomewa shitaka moja la mauaji na mwendesha mashitaka mkaguzi wa polisi,Richard Rweyemamu ambako wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 23 mwaka jana saa 3.20 usiku.

Hata hivyo washitakiwa hao baada ya kusomewa shitaka hilo hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo ya wilaya kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji na kurejeshwa  rumande katika gereza la wilaya la Korogwe lililopo Korogwe mjini.

  

Jumatano, 2 Mei 2018

GOD'SLOVE MAPHIE: MDAU WA MAENDELEO ALIYEVUTIWA NA MPANGO WA MAGUFULI KUIFUFUA ATCL


TANGU aingie madarakani,Rais wa awamu ya Tano,Dk.John Pombe Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa serikali yake inafanya mapinduzi makubwa katika kuelekea uchumi wa kati.

Rais  Magufuli amekuwa muumini wa Tanzania ya Viwanda akiamini kuwa ili Taifa lipige hatua kimaendeleo kufikia uchumi wa kati sharti sekta ya viwanda iimarishwe.

Katika kufanikisha Tanzania ya viwanda,hivi karibinu serikali ilitangaza  zabuni ya ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la kuzalisha umeme katika  maporomoko ya maji yam to Rufiji yanayofahamika kama Stiegler’s  Gorge yanyopatikana ndani ya pori tengefu la Selous . 

Kwa mujibu wa Waziri wa madini,Dk.Medadi  Kalemani,mradi huo  utazalisha umeme wa kiasi cha megawati 2,100 na na utagharimu kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 2 ambazo zitatolewa na Serikali ya Tanzania.

Dkt. Kalemani amesema malengo ya Serikali ni kuzalisha umeme kiasi cha megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 kama Sera ya Nishati ya mwaka 2015 inavyoelekeza.

"Tunataka kujenga Tanzania ya Viwanda. Tunataka ifikapo mwaka 2019-20 tufike megawati 5,000. Tanzania ya Viwanda inahitaji umeme, mradi kama huu na pia ya Kinyerezi I Extension, MW 185 Kinyerezi II MW 240 na miradi mingine itawezesha kufikia lengo letu," alisema Dkt. Kalemani.

Mbali na mkakati wa Rais Magufuli kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda,pia amekuwa katika harakati za kuhakikisha shirika la Ndege Tanzania(ATCL)linafufuliwa kwa kiwango cha juu pamoja na ununuzi wa ndege mpya.

Lengo la serikali ya Rais Magufuli ni kuhakikisha shirika hilo la umma linarejea katika hali yake ili kuinua usafiri wa anga na kuwawezesha watanzania kuendelea kunufaika na raslimali za Taifa lao.

Hadi sasa Rais Magufuli amefanikisha ununuzi wa ndege nne zikiwamo mbili aina ya Dash8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na Dash8-Q300 moja yenye uwezo wa kubeba  abiria 50.

Tayari safari za ndege za shirika hilo ambazo kwa muda mrefu zilisitishwa,zimeanza ikiwamo safari za Dar es salaam- Mbeya,Dar es salaam-Dodoma na kwingineko kwa lengo la kuwapatia huduma bora na kwa bei nafuu watanzania.
 Mdau wa maendeleo Jijini Arusha,God'slove Maphie


God’slove Maphie ni mmoja wa wadau wa maendeleo katika Jiji la Arusha ambaye ameguswa na harakati za Rais Dk.John Pombe magufuli za kulifufua shirika hilo la ndege ikiwamo ununuzi wa ndege mpya.

Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya jijini Arusha,Maphie anasema hatua ya Rais Magufuli kulifufua shirika hilo ni ya kupongezwa na watanzania wote wapenda maendeleo.

“Mimi sitafuti ajira kwa mheshimiwa Rais,lakini ni ukweli uliowazi kuwa kitendo cha kulifufua shirika letu la ndege ni kitendo cha kupongezwa sana hasa katika kuelekea uchumi wa kati”,anasema.

Maphie anasema ilikuwa ni aibu kubwa kwa nchi kubwa kama Tanzania kutokuwa na shirika lake la ndege linalojiendesha kwa ufanisi  huku nchi ndogo kama Rwanda yenye watu wachache ikilinganishwa na Tanzania zikiwa na shirika la ndege.

Mbali na hilo pia amepongeza hatua ya serikali ya Tanzania kuzindua ujenzi wa mradi wa  rada nne ambazo zitakuwa mahususi katika kuhakikisha anga la Tanzania linakuwa salama .

“Unapokuwa huna rada za kuongoza ndege maana yake ni kwamba anga lako linakuwa haliko salama lakini kwa hatua hii ya serikali kuanza ujenzi wa rada nne ni hatua nzuri sana kwetu sisi kama taifa”,anasema.

Pamoja na kupongeza jitihada hizo za serikali ya Dk.John Pombe Magufuli kulifufua shirika la ndege na ujenzi wa rada,akashauri usimamizi mzuri wa raslimali hizo za taifa.

Anasema kama hapatakuwa na usimamizi nzuri katika uendeshaji wa ATCL,basi watanzania watarajie kurejea kule ambako shirika limetoka baada ya kukosa usimamizi mzuri .

Maphie anasema ni wajibu wa bodi ya wakurugenzi ya ATCL kuhakikisha shirika hilo halifi kwa kulisimamia vizuri ili juhudi za Rais Magufuli za kulifufua shirika hilo zilete  matunda mazuri.

“Hata wewe mwandishi wa habari ili ufanye kazi yako kwa ufanisi ni sharti uzingatie miiko ya taaluma yako na hicho ndicho watanzania wanataka kuona shirika linaendeshwa na watu wanaofuata misingi na maadili ya taaluma zao”,anasema.

Anasema kuwa,anaamini Rais magufuli akiuungwa mkono katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo watanzania miaka michache ijayo Tanzania itapiga hatua kubwa kiuchumi na kuondokana na hali ya kuwa tegemezi.
 Moja ya Ndege za Shirika la Ndege Tanzania(ATCL) ikiwa angani.