Jumatano, 30 Mei 2018

MMILIKI SHULE YA SCOLASTICA KUENDELEA KUSOTA RUMANDE,UPELEZI KESI YAKE BADO NGOMA NZITO


 Edward Shayo,mmiliki wa shule binafsi ya sekondari ya Scolastica iliyopo mji mdogo wa Himo mkoani Kilimanjaro,anakabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo,Humphrey Makundi aliyeuawa Novemba 6 mwaka jana,pichani akiwa na pingu mikononi akipelekwa kizimbani.


NA CHARLES NDAGULLA,MOSHI

MMILIKI wa shule binafsi ya sekondari ya Scolastica iliyopo katika Mji Mdogo wa Himo mkoani Kilimanjaro,Edward Shayo ataendelea kusota rumande katika Gereza kuu la mkoa la Karanga kutokana na upelelezi wa kesi  ya mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo kutokukamilika.

Shayo na wenzake wawili wanashitakiwa na Jamhuri kwa mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo,Humphrey Makundi(16)anyedaiwa kuuawa Novemba 6 mwaka jana.

Washitakiwa hao wamerejeshwa tena rumande leo May 30 baada ya upande wa Jamhuri kuieleza mahakama ya hakimu mkazi iliyoketi chini ya Hakimu Julieth Mawole kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

 Kesi hiyo sasa itatajwa tena mahakamani hapo Juni 13 mwaka huu huku ndugu wa washitakiwa hao akiwamo mke wa mmiliki wa shule hiyo Mama Scolastica Shayo wakiondoka makahamani hapo kwa unyonge.

Shayo ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo amekuwa haamini kilichotokea kwani tangu  aliposomewa shitaka la mauaji ya kukusidia kwa mara ya kwanza Novemba 27 mwaka huu,amekuwa katika hali ya majonzi huku akitoa raia kwa ndugu zake kumwombea.

Mbali na Shayo,washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ni Hamis Chacha ambaye ni mlinzi wa shule hiyo pamoja na Makamu mkuu wa shule hiyo,Laban Nabiswa .


Walisomewa shitaka hilo kwa mara ya kwanza na wakili wa serikali Cassim Nasri akisaidiwa na wakili mwenzake wa Serikali Faygrace Sadallah mbele ya hakimu  Julieth Mawole .

Akisoma hati ya mashitaka,wakili Nasri alidai kuwa,mnamo Novemba 6 mwaka jana huko maeneo ya  Himo wilaya ya Moshi,washitakiwa kwa pamoja walimuua kwa makusudi mtu mmoja aitwaye Humphrey Makundi.

Baada ya kusomewa shitaka hilo,washitakiwa hao hawakautakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji hadi mahakama kuu.

 
HUMPHREY MAKUNDI ALIVYOUAWA KIKATIRI



1.Novemba 6 mwaka jana mwanafunzi huyo alidaiwa kutoweka shuleni hapo

2.Novemba 10 mwaka jana mwili wake uliokotwa ndani ya Mto Wona na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa,Mawenzi

3.Novemba 12 mwili wa marehemu ulizikwa na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga baada ya kutojitokeza ndugu wa kuutambua 

4.Novemba 17 mwaka jana mahakama ya hakimu mkazi mjini moshi ilitoa kibali cha mwili huo kufukuliwa baada ya ndugu wa marehemu kubaini kuwa mwili uliozikwa katika makaburi hayo ni wa mtoto wao.

MWILI  ULIVYOFANYIWA  UCHUNGUZI


Mwili wa marehemu Humphrey ulifanyiwa uchunguzi na madaktari katika Hospital ya rufaa ya KCMC na kushuhudiwa na Baba mzazi wa marehemu na katika uchunguzi huo,ikibainika marehemu alikatwa na kitu chenye ncha kali kiunoni,mgongoni,kwenye mapaja na mbavu mbili zilivunjika.

Baba mzazi huyo akawaeleza wanahabari kuwa kulingana na majibu ya uchunguzi huo ni ukweli ulio wazi kuwa,mwanaye aliuawa na kwamba kifo chake kinatia shaka na kuvitaka vyombo vya uchunguzi kuwasaka wahusika wa mauaji ya mtoto wake mpendwa.

SHULE WALIVYOSUSIA MAZISHI YAKE


Katika  hali ya kusikitisha na kushangaza,uongozi wa shule hiyo,ulisusia mazishi ya marehemu Humphrey  yaliyofanyika DEesemba 2 mwaka jana katika Kijiji cha Komakundi wilaya ya Moshi Vijijini.

Uongozi wa shule hiyo haukuweza kutuma mwakilishi katika mazishi hayo ambayo yaliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira huku ibaada ya mazishi ikiongozwa na msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma ,Mchungaji Samwel Mshana.

 Edward Shayo wa pili kutoka kushoto(hajafungwa pingu) akiwa na washitakiwa wenzake wakipelekwa kizimbani,Shayo  na wenzake waanakabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya Scolastica,Humphrey Makundi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni