Jumatano, 26 Novemba 2014

ZAMBI ATENGUA ZUIO LA MRAJIS UUZWAJI SHAMBA LA GARARAGUA



Hatimaye Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,Godfrey Zambi,ametoa ruhusa ya kuuzwa mara moja  shamba kubwa la kahawa la Gararagua mali ya Chama Kikuu cha ushirika mkoani Kilimanjaro(KNCU).

Hatua hiyo imekuja siku chake baada ya ofisi ya Mrajis wa vyama vya ushirika nchini kuzuia uuzwaji wa shamba hilo ikishinikiza kuondolewa kwa Bodi ya wakurugenzi ya KNCU  hatua ambayo iliibua malumbano makali baina yake na bodi ya chama hicho.

Akizungumza wiki hii katika mkutano Mkuu maalumu,Zambi alisema ofisi ya mrajis haina mamlaka kisheria ya kuiondoa bodi ya KNCU na kwamba mwenye mamlaka hayo ni wanachama ambao oktoba 22 mwaka huu walipiga kura na kuridhia bodi hiyo kuendelea kuwapo madarakani.

Waziri Zambi alisema kuwa,shamba hilo litauzwa kwa uwazi baada ya kufanyika kwa tathimini ya thamani halisi ya shamba hilo na kwamba kitaundwa chombo kitakachosimamia uuzwaji huo ili kukiwezesha kuondokana na mzigo wa madeni unaokiandama likiwamo deni kubwa la benki ya CRDB .

Awali ofisi ya  mrajis wa vyama vya ushirika nchini,licha ya kuchelewa kutoa kibali cha kuuzwa kwa shamba hilo,ilitoa masharti ikitaka bodi ya sasa ya KNCU iondoke madarakani na shamba hilo liuzwe chini ya bodi mpya hatua ambayo ilisababisha malumbano makali.

Kutokana na masharti hayo, KNCU iliandika barua ya malalamiko kwa waziri mwenye dhamana na ushirika  wakidai kuwa masharti hayo yanaendelea kukiumiza chama hicho kwa kuendelea kulipa mamilioni ya fedha kwa CRDB kama riba.

Katika taarifa yake kwa wajumbe wa mkutano huo mkuu maalumu,mwenyekiti wa chama hicho,Maynard Swai alimweleza waziri Zambi kuwa,hatua hiyo ya mrajis kuzuia uuzwaji wa shamba hilo ni kuleta machafuko kwa chama hicho na kuua ushirika.

Chama hicho kinamiliki mashamba makubwa manne ambayo ni Gararagua, Lerongo,Lyamungo na Molomo na kati ya hayo matatu yamekodishwa kwa wawekezaji wazalendo huku moja likitarajiwa kutumika kwa shughuli za uzalishaji wa miche bora ya kahawa na  kuwa shamba darasa.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo,chama hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo kuyumba kwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia,mbinu chafu za kibiashara kutoka kwa wapinzani wake.

Aliainisha changamoto nyingine kuwa ni kuwapo kwa ushawishi mbaya wa kisiasa wenye nia ya kukivuruga chama hicho pamoja na mzigo mkubwa wa madeni kuanzia msimu wa 2003/2004 hadi hivi sasa.

UCHAMBUZI: KWA HILI MRAJIS VYAMA VYA USHIRIKA AMEPOTOKA



OKTOBA  22  mwaka huu ofisi ya Mrajis wa vyama vya ushirika nchini,iliitisha mkutano mkuu maalumu wa wanachama wa chama kikuu cha ushirika mkoani Kilimanjaro(KNCU)ambao pamoja na mambo mengine mkutano huo ulijadili hoja za ukaguzi.

Hatua ya kuitishwa kwa mkutano huo mkuu maalumu ni kutokana na madai ya ofisi ya mrajis kwamba KNCU  imeshindwa kujibu hoja za mkaguzi wa nje  katika misimu mitano ya 2008/2009 hadi 2012/2013 hivyo kushindwa kutoa huduma zake kikamilifu kwa wanachama wake.

Kabla ya hoja hizo hazijawasilishwa na kujadiliwa na wajumbe wa mkutano huo mkuu,mwenyekiti wa bodi ya uongozi ya  KNCU,Maynard Swai  alitoa taarifa ya utetezi  kwa wajumbe hao .

Katika utetezi huo,mwenyekiti huyo alishutumu vikali ofisi hiyo ya  mrajis wa vyama vya ushirika nchini na kudai ofisi hiyo ni kikwazo katika ustawi  wa ushirika kutokana na kuyumba katika utoaji wa  maamuzi..

Mwenyekiti huyo alidai kuwa,ofisi hiyo ya mrajis imekuwa ikitoa maamuzi tata ikiwamo kuzuia uuzwaji wa shamba kubwa la kahawa la Gararagua ambalo chama hicho kililenga kuliuza ili kuweza kulipa mkopo wa benki ya CRDB,madeni ya vyama vya msingi na kuimarisha hali ya kifedha ya chama hicho.

Akadia kuwa,pamoja na kuishirikisha ofisi hiyo katika mchakato mzima wa uuzwaji wa shamba hilo na ofisi hiyo ya mrajis kutoa ruhusa ya kuuzwa kwa shamba hilo kwa barua ya machi 27 mwaka huu,ofisi hiyo ilisitisha uuzwaji wa shama hilo .

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo,kitendo cha ofisi hiyo ya mrajis kuwa na maamuzi tata ni uvunjifu wa sheria namba 6  ya ushirika ya mwaka 2013 kifungu cha 132(3) kinachoweka bayana kuwa mtu yeyote anayekwaza au kuingilia shughuli za ushirika na kuisababishia hasara atawajibika kwa hasara hiyo.

“Kwa tafsiri hii ya sheria,kitendo cha kuchelewa kutoa maamuzi kwa mambo mbalimbali ambayo union ilikwishapeleka ofisini kwake,kimeendelea kuisababishia hasara union”,ilisema taarifa ya mwenyekiti huyo.

Kutokana na mkanganyiko huo wa maamuzi ,chama hicho kinadai  kuwa kitalazimika kulipa riba na marejesho  ya milioni 250 mapema mwezi huu baada ya mwezi mei  mwaka huu kulipa kiasi kama hicho .

Kuhusu hoja za ukaguzi ,mwenyekiti huyo alidai hoja hizo ni batili kwa mujibu wa kifungu cha 55(9) cha sheria namba 6 ya ushirika ya mwaka 2013 kinachoweka wazi kuwa,hesabu zikishawasilishwa na kujadiliwa na kisha kupitishwa na mkutano mkuu,uamuzi wao dhidi ya hesabu hizo ni wa mwisho.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo hoja hizo zilikuwa  batili kutokana na kuwasilishwa nje ya muda kama sheria inavyotamka kwa vile ziliwasilishwa  nje ya kipindi cha miezi sita kama sheria inavyoagiza.

Shutuma hizo za KNCU dhidi ya ofisi ya mrajis ni nzito na ambazo hazihitaji kufumbiwa macho na ofisi hiyo ambayo ndiyo mhimili mkuu katika ustawi wa vyama vya ushirika nchini.

Ofisi hii ya mrajis pia inalalamikiwa na KNCU kwa kushindwa kutatua mgogoro wa shamba la Lyamungo licha ya aliyekuwa waziri wa ushirika  ,George Kahama  kuridhia kwamba shamba hilo ni mali ya KNCU  katika barua yake ya Oktoba 21 mwaka 2005.

Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 112 limekaa kwa zaidi ya miaka kumi sasa tangu mwaka 2004 bila kuwekezwa baada yak uwekewa pingamizi na hivyo kukikosesha chama hicho mapato na licha ya kutolewa maamuzi na aliyekuwa mrajis wa vyama vya ushirika wakati huo,hadi sasa limegeuka kuwa pori.

Katika mkutano huo  mkuu maalum,kundi la wanachama lililojitenga kufanya biashara na KNCU lilipewa hadhi ya kutoa maamuzi ikiwamo kupiga kura kuamua kama uongozi wa bodi ya chama hicho uendelee kuwapo madaraka ama la.

Hii ni ajabu ya mwaka,kwamba  watu ambao wameshajiondoa kwenye umoja na kuanzisha umoja wao walioupa jina la G32 wanapewa hadhi ya kutoa maamuzi  ya kuondoa uongozi ambao hawakuuweka madarakani.

Kwa muda mrefu KNCU imekuwa ikilalamikia hatua ya mrajis kutochukua hatua za kulifuta kundi hili ambalo linafanya kazi kinyume na sheria ya ushirika inayokataza kuanzishwa kwa chombo kingine kinachofanya biashara inayofanana na chombo kilichopo katika eneo moja.

Kushindwa kwa ofisi ya  mrajis wa vyama vya ushirika kutoa maamuzi sahihi ikiwamo kufuta usajili wa kundi la G32 linaloendesha biashara kinyume na sheria ya ushirika ni kuzidi kuyapa nguvu malalamiko ya KNCU dhidi ya ofisi hiyo.

Haya ni baadhi tu ya malalamiko ya KNCU dhidi ya ofisi ya mrajis wa vyama vya ushirika nchini hatua ambayo inafifisha ile dhana ya ‘ushirika’ pamoja tunajenga uchumi.

Hakuna ubishi kwamba ushirika kwa sasa umegubikwa na changamoto nyingi ikiwamo ufujaji wa fedha za wakulima ambao umewafanya wakulima wengi kukata tama na kuamua kuachama na ushirika na kujikita katika shughuli nyingine.

Kwa hali hiyo bila kuwapo na jitihada kubwa za kuinua ushirika kwa msaada wa ofisi ya mrajis wa vyama vya ushirika,hatutarajii muujiza kuuinua ushirika na kuwawezesha wakulima kuboresha hali zao za maisha kupitia ushiika.

Kama ofisi ya mrajis itakuwa kikwazo katika ustawi wa ushirika,ile dhana ya ‘ushirika’ tunajenga uchumi haitaweza kufanikiwa na itabakia kuwa katika midomo ya watu pasipo vitendo.


ZILIZOPITA 

 

KADI 'HARAMU' ZAIVURUGA CCM, MWANGA



Hali  ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilayani Mwanga si shwari kutokana na kuibuka kwa kundi linalotoa kadi za chama hichokwa wanachama wapya bila utaratibu kwa misingi ya kujijenga kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao na chaguzi za viongozi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji mapema mwezi ujao.

Habari zilizopatikana hivi karibuni kutoka wilayani mwanga na kudhibitishwa na mbunge wa jimbo hilo,Profesa Jumanne Maghembe,zinadai kuwa tayari kadi haramu 3,000 zimeingizwa wilayani humo na kugawanywa kwa wanachama wapaya bila kufuata tararibu za kichama.

Akizungumza kutoka bungeni  mjini Dodoma, Maghembe amedai kuwa, wanaosambaza kadi hizo bado zinasambazwa kama njugu katika maeneo kadhaa ya jimbo hilo na kukitaka chama hicho kuchukua hatua kwa wanaoendesha mchezo huo mchafu .

Kadi zinatolewa kwa wingi katika maeneo ya Kighare,Kilomeni,Kirongwe ambako taarifa zinadai kuwa zinatolewa bila utaratibu ikiwamo wanachama kupewa bila kuomba na kutojadiliwa kwenye matawi .

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro,Juma Idd alisema kuwa tayari wameagiza uchunguzi kufanyika na kubaini kama kadi hizo zinatolewa nje ya utaratibu na kwamba watakaobainika kufanya hivyo watawajibishwa kwa mujibu wa taratibu.

Hata hivyo mwenyekiti huyo alikwepa kuweka wazi juu ya mpasuko uliopo ndani ya kamati ya siasa ya wilaya hiyo ambako taarifa zinadai kuwa baadhi ya wajumbe wake hawasalimiani hali ambayo inaelezwa kuibua makundi mawili .

Kundi moja ndani ya kamati hiyo ya siasa ni lile linalomuunga mkono mbunge wa sasa Profesa Jumanne Maghembe na jingine likimuunga mkono MNEC,Joseph Thadayo ambaye katika uchaguzi mkuu mwaka 2010,alibwagwa na Maghembe kwenye kura za maoni.

Kutokana na mpasuko huo,baadhi ya wanaccm  waliozungumza na blog wamekitaka chama hicho makao makuu kuunda tume ya kuchunguza sakata hilo  kwa kile walichodai kuwa kamati ya siasa ya wilaya imeparanganyika.

Wamedai kuwa,kamati hiyo haiwezi kutoa matokeo mazuri ya uchunguzi kutokana na mparanganyiko huo kwani hadi sasa wajumbe wa kamati hiyo hawashirikiani hata katika shughuli za maendeleo hata kufikia hatua ya kutozikana.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo,ndiye anayedaiwa kufadhili mpango huo wa kusambaza kadi harahamu kwa lengo la kupanua wingo wa kisiasa na kujiongezea wajumbe wengi wenye ushawishi mkubwa katika zoezi la upigaji wa kura za maoni.