Jumatatu, 3 Novemba 2014

VIJANA WAHANGA WAKUBWA TATIZO LA AJIRA NCHINI



Suala  la  ajira hapa nchini limeelezwa kuwa ndiyo tatizo kubwa  katika jamii  huku wahanga wakubwa  wakiwa ni vijana  kutokana na kundi hilo kuongoza kwa aslimia 61.7 ya watanzania wote.

MWANZILISHI/MTENDAJI MKUU WA TAASISI YA TANZANIA SME GROWTH CENTER, VICTOR TESHA

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mwanzilishi na mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Tanzania SME Growth Center,Victor Tesha wakati akitoa elimu ya ujasiriamali kwa makundi ya kina mama na vijana katika kata za Uru Kishumundu na Uru Kaskazini.

Alisema kuwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012  kundi la vijana ndilo linaloongoza  kwa wingi  kuliko makundi mengine ya Wazee na Watoto ambako inaonyesha vijana kati ya umri wa miaka 15 – 35 wanafikia asilimia 61.7 .

 Mtendaji huyo mkuu wa Taasisi hiyo alikuwa alitoa elimu hiyo ikiwa ni mpango wa taasisi yake kuwawezesha kina mama na vijana waliojiunga katika vikundi vya ujasiriamali kunufaika na mikopo itakayotolewa na taasisi yake katika wilaya za Moshi Vijijini na Mjini pamoja na mkoa wa Arusha.

Akitoa elimu hiyo,Tesha alisema ufumbuzi wa tatizo la ajira litapungua  na kufanikiwa pale jamii itakapobaini  kiini cha tatizo hilo na kiini hicho kimesambaa kwa kiasi kipi suala ambalo linahitaji wadua binafsi na serikali kuangalia namna ya kulitatua.
  
Katika kukabiliana na tatizo hilo  la ajira kwa vijana,mtendaji huyo alisema kuwa,vijana wanatakiwa kuwa na mlengo wa mabadiliko kwa kuamini kuwa ajira si lazima uajiliwe tu bali hata kwa kujiajiri kwa kufanya biashara ndogondogo na kuachana na kasumba ya kuchagua kazi.

 Alisema kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kazi dunia( ILO) ya mwaka 2011 inaonyesha kuwa  asilimia 78.8 ya vijana kote duniani  hawakuwa na ajira, viwango vya vijana waliokosa ajira ilifikia asilimia 12.6% mwaka 2013 na inategemewa kupanda hadi kufikia 12.8% ifikapo mwaka  2018.

Aliongeza kuwa ripoti hiyo imemzindua  na kuwa na wazo la kutatua tatizo la ajira kwa kutafuta taasisi ambazo zinaweza kutoa mikopo ya masharti nafuu kabisa ya  kuwawezesha vijana kujikwamua kimaisha kwa kujiajiri wenyewe.

Alisema watakaonufaika na mikopo hiyo yenye riba nafuu ni vijana na kina mama waliojiunga katika vikundi vya kuanzia watu kumi ambao watajiandikisha na vikundi vyao kutambulika kisheria.

Chini ya mpango huo kabla ya kunufaika na mikopo hiyo,vijana na kina mama  watapewa mafunzo ya kuwajengea uwezo kibiashara ili kupambana na matatizo yanayoweza kujitokeza, kujua njia za kifasaha za kuendesha biashara .

Kwa mujibu wa Tesha,mikopo hiyo itatolewa  kwa mfumo wa vifaa badala ya pesa ambako kila kikundi kitaainisha mahitaji yake  kulingana na biashara watakayofanya kwa pamoja ambako mikopo hiyo inatarajia kuanza kutolewa mwezi ujao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni