Jumatatu, 3 Novemba 2014

MUWSA: TATIZO LA MAJI MOSHI MJINI MWISHO DESEMBA



MAMLAKA  ya maji safi na Usafi wa Mazingira Moshi Mjini(MUWSA) inakamilisha utekelezaji wa miradi mitatu ya maji ambayo itaondoa kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi kwa wananchi ifikapo desemba mwaka huu.
 MKURUGENZI WA MUWSA, CYPRIAN LUHEMEJA

 

Hayo yamo kwenye taarifa ya hali ya huduma ya maji safi iliyotolewa jana na mkurugenzi wa mamlaka hiyo,Cyprian Luhemeja katika mkutano maalum na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo.

Miradi hiyo inahusisha visima viwili vya CCP na Kili Tank pamoja na chanzo cha maji kilichopo mto karanga ambacho maji yake yatazinufaisha kata za Pasua,Boma mbuzi,matindigana na mabogini na maeneo ya katikati ya mji ambapo wananchi wapatao 20,000 watanufaika na mradi huo.

MABOMBA YA MAJI KATIKA HIFADHI SALAMA YA MUWSA
Alisema mradi huo wa maji kutoka chemchem ya chanzo cha maji mto karanga unategemewa kuongeza mita za ujazo 2,592 kwa siku katika mfumo wa kusambazia maji pindi mradi utakapokamilika. 

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo,uzalishaji wa maji katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ni wastani wa mita za ujazo, 34,944 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji ya mita za ujazo 45,082 kwa siku.

Mamlaka hiyo pia imefanya ukarabati wa kilometa 11.8 za mabomba katika mkakati wa kuhakikisha maji yanayoongezwa kwenye mfumo wa kusambazia maji hayapotei kwa kupitia kwenye maomba chakavu na hivyo kuwafikia wateja wengi zaidi.

AIR VALVE KATIKA CHANZO CHA MAJI, KARANGA MJINI MOSHI
Mkurugenzi huyo alisema katika taarifa yake kuwa,matarajio ya mamlaka yake katika kipindi cha Oktoba 2014 na Juni 2015 ni kuanza ujenzi wa chemchem ya maji ya Ndesuo iliyopo Kibosho wilaya ya Moshi vijijini katika mpango wake wa kuboresha zaidi huduma ya maji safi.

Mpango mwingine wa mamlaka hiyo ni kumalizia uchimbaji wa visima viwili vya maji vilivyopo kata ya Longuo ambavyo mamlaka hiyo ilikabidhiwa na manispaa ya Moshi ikiwamo uwekaji wa umeme,pampu,motor na mabomba.

Chini ya mpango huo,mamlaka hiyo imelenga kufanyia ukarabati mtandao wa majisafi kwa  kilometa 14.9 pamoja na kufanyia upanuzi wa mtandao kwa kilometa 40.65 katika sehemu mbalimbali za mji ambazo bado hazijafikiwa na mtandao.
 WAANDISHI WA HABARI MJINI MOSHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni