Jumatano, 26 Novemba 2014

ZAMBI ATENGUA ZUIO LA MRAJIS UUZWAJI SHAMBA LA GARARAGUA



Hatimaye Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,Godfrey Zambi,ametoa ruhusa ya kuuzwa mara moja  shamba kubwa la kahawa la Gararagua mali ya Chama Kikuu cha ushirika mkoani Kilimanjaro(KNCU).

Hatua hiyo imekuja siku chake baada ya ofisi ya Mrajis wa vyama vya ushirika nchini kuzuia uuzwaji wa shamba hilo ikishinikiza kuondolewa kwa Bodi ya wakurugenzi ya KNCU  hatua ambayo iliibua malumbano makali baina yake na bodi ya chama hicho.

Akizungumza wiki hii katika mkutano Mkuu maalumu,Zambi alisema ofisi ya mrajis haina mamlaka kisheria ya kuiondoa bodi ya KNCU na kwamba mwenye mamlaka hayo ni wanachama ambao oktoba 22 mwaka huu walipiga kura na kuridhia bodi hiyo kuendelea kuwapo madarakani.

Waziri Zambi alisema kuwa,shamba hilo litauzwa kwa uwazi baada ya kufanyika kwa tathimini ya thamani halisi ya shamba hilo na kwamba kitaundwa chombo kitakachosimamia uuzwaji huo ili kukiwezesha kuondokana na mzigo wa madeni unaokiandama likiwamo deni kubwa la benki ya CRDB .

Awali ofisi ya  mrajis wa vyama vya ushirika nchini,licha ya kuchelewa kutoa kibali cha kuuzwa kwa shamba hilo,ilitoa masharti ikitaka bodi ya sasa ya KNCU iondoke madarakani na shamba hilo liuzwe chini ya bodi mpya hatua ambayo ilisababisha malumbano makali.

Kutokana na masharti hayo, KNCU iliandika barua ya malalamiko kwa waziri mwenye dhamana na ushirika  wakidai kuwa masharti hayo yanaendelea kukiumiza chama hicho kwa kuendelea kulipa mamilioni ya fedha kwa CRDB kama riba.

Katika taarifa yake kwa wajumbe wa mkutano huo mkuu maalumu,mwenyekiti wa chama hicho,Maynard Swai alimweleza waziri Zambi kuwa,hatua hiyo ya mrajis kuzuia uuzwaji wa shamba hilo ni kuleta machafuko kwa chama hicho na kuua ushirika.

Chama hicho kinamiliki mashamba makubwa manne ambayo ni Gararagua, Lerongo,Lyamungo na Molomo na kati ya hayo matatu yamekodishwa kwa wawekezaji wazalendo huku moja likitarajiwa kutumika kwa shughuli za uzalishaji wa miche bora ya kahawa na  kuwa shamba darasa.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo,chama hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo kuyumba kwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia,mbinu chafu za kibiashara kutoka kwa wapinzani wake.

Aliainisha changamoto nyingine kuwa ni kuwapo kwa ushawishi mbaya wa kisiasa wenye nia ya kukivuruga chama hicho pamoja na mzigo mkubwa wa madeni kuanzia msimu wa 2003/2004 hadi hivi sasa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni