Jumatano, 26 Novemba 2014

UCHAMBUZI: KWA HILI MRAJIS VYAMA VYA USHIRIKA AMEPOTOKA



OKTOBA  22  mwaka huu ofisi ya Mrajis wa vyama vya ushirika nchini,iliitisha mkutano mkuu maalumu wa wanachama wa chama kikuu cha ushirika mkoani Kilimanjaro(KNCU)ambao pamoja na mambo mengine mkutano huo ulijadili hoja za ukaguzi.

Hatua ya kuitishwa kwa mkutano huo mkuu maalumu ni kutokana na madai ya ofisi ya mrajis kwamba KNCU  imeshindwa kujibu hoja za mkaguzi wa nje  katika misimu mitano ya 2008/2009 hadi 2012/2013 hivyo kushindwa kutoa huduma zake kikamilifu kwa wanachama wake.

Kabla ya hoja hizo hazijawasilishwa na kujadiliwa na wajumbe wa mkutano huo mkuu,mwenyekiti wa bodi ya uongozi ya  KNCU,Maynard Swai  alitoa taarifa ya utetezi  kwa wajumbe hao .

Katika utetezi huo,mwenyekiti huyo alishutumu vikali ofisi hiyo ya  mrajis wa vyama vya ushirika nchini na kudai ofisi hiyo ni kikwazo katika ustawi  wa ushirika kutokana na kuyumba katika utoaji wa  maamuzi..

Mwenyekiti huyo alidai kuwa,ofisi hiyo ya mrajis imekuwa ikitoa maamuzi tata ikiwamo kuzuia uuzwaji wa shamba kubwa la kahawa la Gararagua ambalo chama hicho kililenga kuliuza ili kuweza kulipa mkopo wa benki ya CRDB,madeni ya vyama vya msingi na kuimarisha hali ya kifedha ya chama hicho.

Akadia kuwa,pamoja na kuishirikisha ofisi hiyo katika mchakato mzima wa uuzwaji wa shamba hilo na ofisi hiyo ya mrajis kutoa ruhusa ya kuuzwa kwa shamba hilo kwa barua ya machi 27 mwaka huu,ofisi hiyo ilisitisha uuzwaji wa shama hilo .

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo,kitendo cha ofisi hiyo ya mrajis kuwa na maamuzi tata ni uvunjifu wa sheria namba 6  ya ushirika ya mwaka 2013 kifungu cha 132(3) kinachoweka bayana kuwa mtu yeyote anayekwaza au kuingilia shughuli za ushirika na kuisababishia hasara atawajibika kwa hasara hiyo.

“Kwa tafsiri hii ya sheria,kitendo cha kuchelewa kutoa maamuzi kwa mambo mbalimbali ambayo union ilikwishapeleka ofisini kwake,kimeendelea kuisababishia hasara union”,ilisema taarifa ya mwenyekiti huyo.

Kutokana na mkanganyiko huo wa maamuzi ,chama hicho kinadai  kuwa kitalazimika kulipa riba na marejesho  ya milioni 250 mapema mwezi huu baada ya mwezi mei  mwaka huu kulipa kiasi kama hicho .

Kuhusu hoja za ukaguzi ,mwenyekiti huyo alidai hoja hizo ni batili kwa mujibu wa kifungu cha 55(9) cha sheria namba 6 ya ushirika ya mwaka 2013 kinachoweka wazi kuwa,hesabu zikishawasilishwa na kujadiliwa na kisha kupitishwa na mkutano mkuu,uamuzi wao dhidi ya hesabu hizo ni wa mwisho.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo hoja hizo zilikuwa  batili kutokana na kuwasilishwa nje ya muda kama sheria inavyotamka kwa vile ziliwasilishwa  nje ya kipindi cha miezi sita kama sheria inavyoagiza.

Shutuma hizo za KNCU dhidi ya ofisi ya mrajis ni nzito na ambazo hazihitaji kufumbiwa macho na ofisi hiyo ambayo ndiyo mhimili mkuu katika ustawi wa vyama vya ushirika nchini.

Ofisi hii ya mrajis pia inalalamikiwa na KNCU kwa kushindwa kutatua mgogoro wa shamba la Lyamungo licha ya aliyekuwa waziri wa ushirika  ,George Kahama  kuridhia kwamba shamba hilo ni mali ya KNCU  katika barua yake ya Oktoba 21 mwaka 2005.

Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 112 limekaa kwa zaidi ya miaka kumi sasa tangu mwaka 2004 bila kuwekezwa baada yak uwekewa pingamizi na hivyo kukikosesha chama hicho mapato na licha ya kutolewa maamuzi na aliyekuwa mrajis wa vyama vya ushirika wakati huo,hadi sasa limegeuka kuwa pori.

Katika mkutano huo  mkuu maalum,kundi la wanachama lililojitenga kufanya biashara na KNCU lilipewa hadhi ya kutoa maamuzi ikiwamo kupiga kura kuamua kama uongozi wa bodi ya chama hicho uendelee kuwapo madaraka ama la.

Hii ni ajabu ya mwaka,kwamba  watu ambao wameshajiondoa kwenye umoja na kuanzisha umoja wao walioupa jina la G32 wanapewa hadhi ya kutoa maamuzi  ya kuondoa uongozi ambao hawakuuweka madarakani.

Kwa muda mrefu KNCU imekuwa ikilalamikia hatua ya mrajis kutochukua hatua za kulifuta kundi hili ambalo linafanya kazi kinyume na sheria ya ushirika inayokataza kuanzishwa kwa chombo kingine kinachofanya biashara inayofanana na chombo kilichopo katika eneo moja.

Kushindwa kwa ofisi ya  mrajis wa vyama vya ushirika kutoa maamuzi sahihi ikiwamo kufuta usajili wa kundi la G32 linaloendesha biashara kinyume na sheria ya ushirika ni kuzidi kuyapa nguvu malalamiko ya KNCU dhidi ya ofisi hiyo.

Haya ni baadhi tu ya malalamiko ya KNCU dhidi ya ofisi ya mrajis wa vyama vya ushirika nchini hatua ambayo inafifisha ile dhana ya ‘ushirika’ pamoja tunajenga uchumi.

Hakuna ubishi kwamba ushirika kwa sasa umegubikwa na changamoto nyingi ikiwamo ufujaji wa fedha za wakulima ambao umewafanya wakulima wengi kukata tama na kuamua kuachama na ushirika na kujikita katika shughuli nyingine.

Kwa hali hiyo bila kuwapo na jitihada kubwa za kuinua ushirika kwa msaada wa ofisi ya mrajis wa vyama vya ushirika,hatutarajii muujiza kuuinua ushirika na kuwawezesha wakulima kuboresha hali zao za maisha kupitia ushiika.

Kama ofisi ya mrajis itakuwa kikwazo katika ustawi wa ushirika,ile dhana ya ‘ushirika’ tunajenga uchumi haitaweza kufanikiwa na itabakia kuwa katika midomo ya watu pasipo vitendo.


ZILIZOPITA 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni