Jumanne, 3 Aprili 2018

KILIMO,UVUVI HARAMU VINAVYOHATARISHA UHAI BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU


 
 Bwawa la Nyumba ya Mungu linaounguanisha wilaya za Mwanga mkoani Kilimanjaro na Simanjiro Mkoani Manyara

Bwawa la Nyumba ya Mungu ni chanzo kikubwa cha maji yanayotumika kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu, kilimo cha umwagiliaji,  mifugo na uzalishaji wa umeme, lakini shughuli hizo zinaweza kuhatarisha uzalishaji wa umeme unaosambazwa na Gridi ya Taifa. 

Bwawa la Nyumba ya Mungu  linapatikana wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro ambapo lilitengenezwa ili kuhifadhi maji yanayotiririka kutoka Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuzuia mafuriko kwenye makazi ya watu na mashamba na baadaye yatumike kuzalisha umeme na kwenye kilimo.

Lakini ongezeko la shughuli za kilimo kupitia mito ya asili ikiwemo Kikuletwa na Ruvu pembezoni mwa bwawa hilo kumechangia upotevu mkubwa wa maji kwenye vituo vya kuzalisha umeme.

Inaelezwa kuwa vituo hivyo ni Nyumba ya Mungu kilichopo Wilaya ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, New Pangani Falls, wilaya ya Muheza na Hale kilichopo wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambavyo vyote vina uwezo wa kuzalisha megawati 97.

Akizungumza na wanahabari Meneja wa vituo hivyo, Mhandisi  Mahenda Mahenda alisema kwenye  Bwawa la Nyumba ya Mungu kuna mitambo miwili inayozalisha umeme iliyoanza kazi 1969 ambapo mitambo hiyo inafanya kazi vizuri na imekuwa ikifanyiwa matengenezo mara kwa mara.

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji yanayotumiwa na wakazi wa wilaya zinazozunguka bwawa hilo yamechangia kupungua kwa kina cha maji.
 Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu(katikati)akipokea maelezo mafupi ya shughuli za uzalishaji umeme katika kituo cha kupozea umeme cha Bwawa la Nyumba ya Mungu alipotembelea bwawa hilo hivi karibini.

 “Bwawa linapokuwa na kiwango kidogo cha maji uzalishaji umeme hupungua, kuna wakati maji hupungua zaidi hivyo taratibu haziruhusu tuendelee kuzalisha umeme”,anasema.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kituo cha Nyumba ya Mungu, Mhandishi, Clarence Mahunda alisema kituo chake kina uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 8 ambao huingizwa kwenye Gridi ya Taifa kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani na viwandani.

Mhandisi Mahunda alisema hadi kufikia mwishoni mwa Januari mwaka huu kituo hicho klikuwa kinazalisha megawati 3.5 hadi 4 tofauti na uwezo wake wa kuzalisha megawati 8 kwa saa 24.

“Shughuli za binadamu zikiwemo kulima, kuchunga ng’ombe na uvuvi kumepelekea uzalishaji wa umeme katika kituo hiki kuwa hafifu, kitu ambacho kinasababisha ukosefu wa maji ya kutosha hivyo uzalishaji umeme pungufu”, alisema Mhandisi Mahunda.

Alibainisha kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo  wameendelea kuzuia athari za kimazingira pembezoni mwa bwawa la Nyumba ya Mungu lakini bado uwezo wa uzalishaji umeme haujaongezeka kwasababu kina cha maji kiko chini.

Mkazi wa kijiji  cha Kagongo kilichopo wilaya ya Mwanga  mkoani Kilimanjaro, Charles John Waziri  alisema kuwa kuna hujuma katika matumizi ya rasilimali maji ambapo imebainika kuwa wakulima wanaotumia kilimo cha umwagiliaji wamekua wakitumia maji kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu katika bwawa.

Naye, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alizitaka serikali za mitaa na Mkoa kwa kushirikiana na wananchi wanaozunguka vituo hivyo kuhakikisha wanatunza mazingira ya Bwawa la Nyumba ya Mungu ili kupata maji kwa ajili ya uzalishaji umem

“Nimeelezwa kuwa kina cha maji hakiruhusu mashine zote kuzalisha umeme, na hii ni kwasababu ya shughuli za binadamu ambazo zinaendelea pembezoni mwa Bwawa la maji yanayotumika kuzalisha umeme huo”, alisema Naibu Waziri.

Wadau wa mazingira wamezishauri mamlaka zinazohusika na bwawa hilo ziwajibike kuhamasisha uboreshaji mifereji kwa kuisakafia ili kuokoa upotevu mkubwa wa maji na kuachana na mifereji ya asili ambayo inapoteza maji mengi yanayoingia kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu.
 

 Pichani ni Boti iliyonunuliwa na Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani manyara kwa ajili ya kufanya dori kukabiliana na uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu,boti hiyo sasa haifanyi kazi.

Nyumba ya Mungu

Bwawa la nyumba ya Mungu lilijengwa na kukamilika mwaka 1965 Kaskazini mwa Tanzania. Mwaka 1970 lilianza kutumiwa zaidi kwa uvuvi wa samaki lakini mabadiliko ya hali ya hewa yamepunguza upatikanaji wa samaki na uzalishaji umeme katika bwawa hilo. 

Bwawa hilo lilijengwa karibu na maporomoko ya Neogene Kilomita 80 kutoka Kusini mwa mlima Kilimanjaro ambapo urefu wake unafikia Kilomita 180 na kina cha maji cha mita 6 kwenda chini. Bwawa hilo linapokea maji kutoka vyanzo mbalimbali lakini chanzo kikubwa ni mlima Kilimanjaro.

Maji yanayotoka kwenye bwawa hilo hutumika kuzalisha umeme katika vituo vya Pangani, Nyumba ya Mungu na Hale. Lakini bwawa hilo limeathiriwa mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za binadamu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni