Jumanne, 17 Aprili 2018

MASHITAKA YA WATUHUMIWA WA UFISADI TCCCo YAIVA

NA CHARLES NDAGULLA,MOSHI

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini(Takukuru) mkoani Kilimanjaro,imekamilisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi wa zaidi ya shilingi Bilioni mbili zinazowakabili vigogo wa Kiwanda cha kukoboa kahawa cha Tanganyika Coffee Curing(TCCCo).

Ufisadi huo unahusisha ununuzi wa mtambo unaodaiwa kuwa ni chakavu wa kukoboa kahawa katika kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa aslimia 54 na Chama Kikuu cha ushirika(KNCU)mkoani Kilimanjaro.

Miongoni mwa wanaochunguzwa na Takukuru ni aliyekuwa  mwenyekiti  wa (KNCU),Maynard Swai ambaye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kiwamda hicho pamoja na aliyekuwa meneja mkuu wa kiwanda hicho,Andrew Kleruu .

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita,kaimu mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro,Moses Uguda amesema tayari majalada sita yanayohusu tuhuma za vigogo hao yamepelekwa kwa mkurugenzi wa mashitaka nchini(DPP) kwa ajili ya kupata kibali cha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao.

Oguda alisema kiwanda hicho ni mali ya wanaushirika na si mali ya mtu binafsi kama ambavyo baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakijaribu kuipotosha jamii na kwamba  takukuru kama chombo cha uchunguzi kinao wajibu wa kuchunguza ufisadi wa mali hizo za wanaushirika.

Mkutano huo na waandishi wa habari ulikuwa mahususi kwa ajili ya kutoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia januari hadi machi mwaka huu.

Wanahisa wengine wa kiwanda hicho ni pamoja na Chama cha   wamiliki mashamba makubwa (TCGA)kikiwa na  asilimia 36 ya hisa,Vyama vingine vinne vikuu vya ushirika   vinavyomiliki hisa kwenye kiwanda hicho ni ACU,USAMBARA,MOFACU,RIVACU na KANYOVU ambavyo vinamiliki asilimia 10 ya hisa zilizobaki.

Mtambo huo unadaiwa kununuliwa nchini Brazil  kutoka Kampuni ya Pinhalense baada ya serikali kuridhia bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho kuuza mali zake ili kununua mtambo  huo mpya.

Hata hivyo,pamoja na kiasi  hicho kikubwa cha fedha kutumika kununua mtambo huo,hadi sasa umeshindwa kuanza kutumika tofauti na matarajio ya wengi huku mtambo unaotajwa kuwa ni mbovu na haufai  ukiwa unaendelea kukoboa kahawa.
 
Uchunguzi uliofanywa na Ndagullablog umebaini kuwa  baadhi ya vifaa vimekuwa vikinyofolewa kutoka mtambo wa zamani  na kufungwa kwenye mtambo huo mpya hatua ambao imeibua maswali mengi kuliko majibu.


Sababu za kuuzwa kwa mali hizo zikiwamo nyumba  ilikuwa ni  kununua mtambo huo  mpya  ili kukiwezesha kiwanda hicho  kujiendesha kwa ufanisi na kulipa madeni ya kisheria ya zaidi ya  sh,Milioni 800 ambayo kiwanda hicho kinadaiwa ikiwamo TRA,NSSF,Manispaa ya moshi na madeni ya manunuzi.


Katika  mkutano wake na waandishi wa habari Machi 17 mwaka 2013,Maynard Swai akiwa mwenyekiti wa bodi ya kiwanda hicho,alitaja madeni hayo ya kisheria kwa  upande wa TRA ni sh,Milioni 377,541,680,NSSF(Milioni 163,391,438),Manispaa ya Moshi(Milioni 78,188,287),Astra insurance(Milioni 44,064,038),madeni ya watumishi yakiwamo mafao ya kustaafu(Milioni 59,877,236).


Pia kiwanda hicho kinadaiwa ada ya ukaguzi wa mahesabu kutoka shirika la kukagua mahesabu ya vyama vya ushirika la COASCO wanaodai sh,Milioni 10,000,000,wakati SACCOs ya kiwanda hicho ikidai sh,Milioni 2.800,000 huku madeni ya manunuzi yakiwa ni sh,Milioni 75,509,612,madeni haya ni kufikia mwaka 2013. 

Taarifa ya mwenyekiti huyo kwa  wanahabari ambayo nakala yake tunayo,ilieleza kuwa  athari zinazosababishwa na uchakavu wa mitambo hiyo iliyojengwa miaka 60 iliyopita chini ya mjerumani  Heins Bueb ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha ukoboaji kutoka tani 65,736 msimu wa 1980/81 hadi kufikia tani 3,487 msimu wa 2012/2013.


Athari nyingine ni kushuka kwa ubora wa ukoboaji kunakochangiwa na kupondwa,punje kuvunjwa vunjwa hatua ambayo alisema inasababisha hasara kwenye madaraja na kupanda kwa kiwango cha hasara kwa mkulima.

Mwenyekiti huyo  wa zamani wa bodi alisema katika kujikwamua na janga hilo,kiwanda kililazimika kupunguza wafanyakazi wake kutoka 660 hadi wafanyakazi 65 zoezi ambalo lilifanywa kwa awamu nne kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2003 .

Pamoja na upunguzaji huo wa wafanyakazi,Swai alisema bado gharama za uendeshaji ziko juu kutokana na uchakavu mkubwa  wa mitambo ambayo ina umri wa miaka 40 na kushuka kwa kiwango cha mapokezi ya kahawa.


“Bodi ilitafakari kwa kina hali ya kiwanda na  kuona umhimu wa kununua mtambo mmoja wa kisasa ili kunusuru kiwanda,mtambo unaotegemewa kununuliwa una uwezo wa kupunguza gharama ikilinganishwa na mtambo uliopo”,inasema taarifa hiyo.

Mwenyekiti huyo aliusifia sana mtambo huo  katika taarifa yake kuwa una uwezo wa kukoboa tani sita za kahawa kwa saa moja badala ya mitambo minne chakavu ya sasa inayokoboa kahawa chini ya tani tatu kwa saa  moja.

Kwamba mtambo huo mpya ungepunguza gharama za umeme kwa zaidi ya nusu ya gharama za sasa kutokana na mtambo huo mpya kuwa na “installed capacity” ya 165KW dhidi ya 431KW kwa  mtambo wa zamani.   


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni