Alhamisi, 29 Machi 2018

LIPENI ANKRA ZA MAJI KWA WAKATI,DC KIPPI WARIOBA AWAASA WATEJA MUWSA


 
   Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na uondoshaji wa majitaka Moshi Mjini(MUWSA),Joyce Msiru akitoa taarifa ya utendaji kazi wa mamlaka hiyo katika uzinduzi wa wiki ya maji hvi karibini mjini moshi.                
  

MKUU wa Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Kippi Warioba amewataka Wananchi kulipa ankra za maji kwa wakati, ili huduma hiyo izidi kuwa endelevu, hali ambayo itawezesha pia kuwahudumia watu wengine kwa pamoja.

Warioba  alitoa kauli hiyo hivi karibuni  kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya  Maji ambayo kimkoa yalifanyika mjini moshi  katika viwanja vya Mamlaka ya Majisafi na Uondoshai wa maji taka moshi mjini (MUWSA).

Alisema kuwa ili MUWSA iweze kuendelea kutoa huduma bora ya maji kwa wananchi wa moshi ni vyema Wananchi wakawa na utayari wa kulipia ankra hizo kwa wakati.

“Niwaase Wananchi wenzangu kulipia ankra zenu za maji kwa wakati ili kuifanya huduma ya maji itolewayo na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira MUWSA, kuwa endelevu,”alisema Warioba.

Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwataka Wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji, ili maji hayo yaendelea kuwapo wakati wote kwenye vyanzo vya maji vilivyopo bila kupungua.

“Nachukua nafasi hii kuwaasa wale wote wanaofanya shughuli za uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji kuacha mara moja kufanya uharibifu huo,”alisema.
MKuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba(wa pili kutoka kulia)akikata utepe kuzindua huduma mpya ya kulipia ankara za maji ijulikanayo kama NMB Mobile katika uzinduzi wa wiki ya maji iliyofanyika hivi karibuni mjini Moshi.

Aliongeza kuwa “Naomba nitoe agizo kali kwa yeyote atakayepatikana anafanya shughuli za uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji, hatua kali zichukuliwe dhidi yake, na wale wote watakaokwenda kinyume na katazo la sheria hizi, waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria,”alisema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya sheria ya rasilimali za maji namba 11 ya mwaka 2009 kifungu cha 34, sambamba na sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 57, vyote kwa pamoja vinapinga  kufanyika kwa  shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kwenye vyanzo vya maji, mabwawa, mito, maziwa, chemichemi pamoja na kwenye visima.

Nae Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na ondoshaji wa majitaka(MUWSA) Joyce Msiru, alisema kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kuhamasisha na kuwaelimisha Wananchi kushiriki kikamilifu  katika matumizi ya majisafi na usafi wa mazingira, ikiambatana na kulipia ankra za matumizi ya majisafi na maji taka kwa wakati.

“Mamlaka inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya maji kuelimisha jamii juu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji na uendeshaji endelevu wa miradi ya maji, ili kuhakikisha kizazi kijacho kinapata rasilimali ya majisafi kwa uhakika na ubora unaotakiwa,”alisema Msiru. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni