Jumatano, 7 Machi 2018

WADAU MPIRA WA MAGONGO WALILIA VIWANJA MASHULENI ILI KUIBUA VIPAJI


Na Kija Elias,Moshi.
WADAU wa mchezo wa mpira wa Magongo hapa nchini, wameiomba serikali kupitia Wizara ya elimu kujenga viwanja vya mchezo huo kuanzia  shule za msingi na sekondari ili kuweza kuibua vipaji kwa wanafunzi kuanzia ngazi za awali.

Ombi hilo limetolewa na mjumbe wa chama cha mpira wa Magongo Tanzania (Hockey), Nitu Singh Rehal mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe kwenye  kikao cha wadau wa mchezo mkoa wa kilimanjaro, kilichofanyika hivi karibuni kwenye  ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya  mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema kujengwa kwa viwanja vya mpira wa magongo katika shule nyingi nchini kutawezesha kuibua vipaji lukuki vya mchezo huo hatua ambayo itawezesha kupata wachezaji bora ambao wataweza kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindani ya kimataifa.

“Mchezo wa magongo unakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa viwanja vya kuchezea mchezo huo, hususani kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, endapo vitajengwa viwanja vingi vya mchezo huu mashuleni tutaweza kupata wachezaji wazuri ambao wataitangaza nchi yetu kimataifa,”alisema.
 Mjumbe wa Chama cha mpira wa magongo Tanzania(Hockey).Nitu Singh Rehal akizungumza kwenye kikao cha wadau wa michezo klichoitishwa na Waziri mwenye dhamana na michezo,Dk.Harrison Mwakyembe hivi karibuni mjini Moshi.

Alisema kufundishwa kwa mchezo huo mashuleni kutawezesha kuibua vipaji na kuwapeleka wanafunzi hao kuwashindanisha na wanafunzi wenzao katika mikoa mbalimbali iliyopo hapa nchini.

Vile vile mjumbe huyo Nitu Singh Rehal aliiomba serikali kutazama upya gharama za kodi kwenye vifaa vya michezo vinavyoingizwa nchini kama msaada kutoka kwa wafadhili ili kuweza kuboresha michezo hapa nchini.

“Uwepo wa vifaa hivyo utawezesha kuzidi kuibua vipaji kwa mpira wa magongo, kwani vinauzwa ghali sana, tutashukuru serikali endapo itatupunguzia kodi ya uingizwaji wa vifaa vya michezo ili wanafunzi wetu waweze kupenda kucheza mchezo huo,”alisema.

Aliongeza kuwa ili mwanafunzi aweze kuupenda na kujiunga na mchezo huo wa magongo ni vyema serikali ikapunguza kodi ya vifaa hivyo na kuweza kusambazwa kwenye mashule mengi.

“Changamoto kubwa hapa inayosababisha wanafunzi kushindwa kuandaliwa katika mchezo wa magongo na kushindwa kuucheza mchezo huu wa magongo ni ukosefu wa vifaa hivyo pamoja na viwanja vya kuchezea mchezo huo”alisema Rehal.

Kwa upande wake Waziri wa habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe alisema kuwa serikali italifanyia kazi suala la kodi kwa vifaa vya michezo nchini.

“Kwa sasa tupo katika maongezi na wenzetu wa Wizara ya fedha ili kuhakikisha kwamba vifaa vya michezo vinaingia kwa gharama ndogo,”alisema Waziri Mwakyembe.

 Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo,Dkt.Harrison Mwakyembe(wa nne kutoka kushoto waliokaa)akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa michezo mara baada ya kikao chake na wadau hao hivi karibuni mjini Moshi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni