Jumanne, 27 Machi 2018

KICHAA CHA MBWA CHABISHA HODI K'NJARO,CHAUA WATATU,MAKUMI WAJERUHIWA


 NA CHARLES NDAGULLA,MOSHI

MKOA  wa Kilimanjaro,umekumbwa na tishio la ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambako mpaka sasa watu watatu wamekufa kutokana na kung’atwa na mbwa wanaoaminika kuwa na ugonjwa huo wakiwamo watoto wawili na mama mmoja .

Mbali na watu hao kufariki dunia katika halmashauri ya wilaya ya Moshi,watu 64 wameripotiwa kujeruhiwa na mbwa hao wenye ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika Vijiji vya TPC,Mawala,Oria,Mabogini na Ngasini.

Waliofariki dunia kwa kung’atwa na mbwa hao wametajwa kuwa ni Lulu Zephania(4),Grace Benny (5) mwanafunzi wa shule ya awali katika shule ya msingi Mawala na Naomi Mmanga(34) wote wakazi wa Kijiji cha Mawala.

Kwa mujibu wa Dk.Walter Marandu,daktari wa mifugo katika Halmashauri ya wilaya ya Moshi ,watu hao walishambuliwa na mbwa mmoja kati ya februari mosi na februari 5 mwaka huu na kukimbizwa katika Zanahati ya mawala kwa matibabu.

Akizungumza na Ndagullablog,Marandu  amesema kuwa baada ya hali zao kuendelea kuwa mbaya walihamishiwa katika  Hospitali ya TPC inayomilikiwa na Kiwanda cha sukari cha TPC kabla ya kupelekwa katika Hospital ya rufaa ya KCMC ambako mauti yaliwakuta.

Dk. Marandu amebainisha kuwa,tayari oparesheni kubwa ya kuwaangamiza mbwa hao inaendelea katika maeneo mbali mbali yaliyoripotiwa kukumbwa na ugonjwa huo.

Amesema mpaka sasa mbwa zaidi ya 100 wanaodaiwa kuwa na kichaa cha mbwa wameuawa katika oparesheni hiyo katika vijiji vya Mawala, Mikocheni, Msarikie na Mtakuja.

Kwa mujibu wa Dk.Marandu,watu 64 waliong’atwa na mbwa hao ni katika kipindi cha kuanzia januari hadi mwezi machi mwaka huu na kwamba tatizo hilo la kuwepo na mbwa wenye kichaa cha mbwa ni kubwa huku  wengi wa mbwa wenye ugonjwa huo  ni wale wanaozagaa mitaani .

Amesema tayari Halmashauri imeanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya kukabiliana na mbwa hao kwa kutoa gari la matangazo ambalo limekuwa likizunguka katika maeneo mbali mbali ya vijiji kutoa tahadhari hiyo.

“Timu yetu ya wataalamu ipo vijiji pamoja na gari la matangazo,tunatoa matangazo makanisani na misikitini juu ya kuwepo na mbwa wenye kichaa cha mbwa na namna ya wanachi kuchukua hatua”,amesema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji cha Mawala,David Laizer,amezungumza na Ndagullablog na kueleza kuwa tayari wamewaua mbwa 19 katika kijiji hicho tangu kuripotiwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo .


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi,Michael Kilawila amezungumza na Ndagullablog kuhusiana na kuibuka kwa ugonjwa huo na kueleza kuwa tayari zoezi la kuwapa chanjo mbwa hao limeanza.

Amesema lengo la chanjo hiyo ni kuhakikisha mbwa hao hawaendelei kuleta madhara kwa binadamu huku chanjo hiyo ikienda sanjari na kutolewa kwa elimu kwa wannchi juu ya kujilinda na mbwa hao.

“Tunawaomba wenye mbwa wao kuhakikisha kuwa mbwa wao wanapatiwa chanjo zinazositahili kuanzia chanjo ya kichaa cha mbwa, pamoja na magonjwa mengine ili kuepusha watu wasiendelee kupata madhara zaidi.

Moshi mjini nako hali tete.

Wakati hali ikiwa hivyo katika Halmshauri ya wilaya ya Moshi Vijijini,tatizo hilo pia limeripotiwa katika maeneo kadhaa ya mji wa Moshi ambako watu 13 wamelazwa katika Hospital teule ya St.Joseph ,Hospital ya Rufaa ya KCMC na kituo cha Afya cha Pasua baada ya kudaiwa kung’atwa na mbwa hao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,Michael Mwandezi amedhibitisha kuwepo na tishio la mbwa kung’ata watu katika manispaa hiyo alipozungumza na wanahabari ofisini kwake wiki iliyopita.

Amesema mbali na watu hao kulazwa kutokana na kushambuliwa na mbwa hao,hadi sasa zaidi ya watu 90 wameripotiwa kung’atwa na mbwa ndani ya manispaa ya Moshi katika kipindi cha kuanzia januari hadi machi mwaka huu.

“Ni kweli  manispaa yetu imekubwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa  na hivi ninavyozungumza tunao  wagonjwa ambao wameng’atwa na mbwa hao na baadhi yao  wamefariki dunia japo kwa sasa sina tawimu sahihi ya idadi ya waliokufa   na pia  wako wanaoendelea kupatiwa matibabu katika hosptali zetu”amesema

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo,Hospital teule ya Mtakatifu Joseph imepokea wagonjwa wanne wakati Hospital ya rufaa ya KCMC inayoendeshwa na Shirika la Msamalia Mwema(GSF)imepokea wagonjwa saba na kituo cha Afya cha pasua kinao wagonjwa wawili.

Amesema jitihada mbali mbali zimechukuliwa kukabilina na tishio la mbwa hao ikiwamo kuendesha oparesheni ya kuwaua mbwa wote wanaoonekana wakilanda landa mitaani.

  ”Tumeshaanza kutoa  matangazo kwa wananchi na tumewataka kutoa taarifa endapo watawaona mbwa  wakilanda landa mitaani na pia tumetoa maelekezo kwa wamiliki wa mbwa kuchukua tahadhari ikiwamo kuwapa chanjo mbwa  ”amesema

Mganga  Mkuu wa Manispaa hiyo,  Soka Mwakapalala amesema baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika  Hospitali za KCMC na Mtakatifu Joseph  hali zao ni mbaya  kutokana na baadhi yao kuripotiwa kupatwa na tatioz la kubweka kama mbwa.

Dk. Mwakapalala amesema kuwa mpaka sasa watu 91 wameripotiwak ung’atwa nam bwa kati ya januari na machi mwaka huu huku akieleza kuwa  virusi vya kichaa cha mbwa hushambulia sana mishipa ya fahamu na dalili kubwa ni mtu Kubweka kama mbwa  na  mwisho mtu  huyo hupoteza fahamu na kufariki.

“Asilimia 99 ya wagonjwa walioang’atwa na mbwa hufariki dunia hivyo kunahitajika tahadhari kubwa sana na tunawaomba wananchi pindi wanaposhambuliwa na mbwa ni mhimu kwenda haraka kupata matibabu ndani ya saa 24”amesema.

Mpaka sasa Manispaa ya Moshi imeendesha oparesheni na kuwaua mbwa 700 kwa kuwapiga risasi huku mbwa 709 wkaipatiwa chanjo.

Kwa mujibu wa Dk. Mwakapalala, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 watu zaidi ya 1,000 waling’atwa na mbwa  ambapo mwaka 2016 walikuwa 434, mwaka 2017 watu 564 na katika kipindi cha kuanzia January hadi Machi mwaka huu ni watu 91.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni