Jumamosi, 17 Machi 2018

PIERRE NKURUNZINZA KUTAWALA MILELE BURUNDI,HUU NI ULEVI MWINGINE WA MADARAKA KWA WATAWALA WA AFRIKA


Chama tawala nchini Burundi CNDD/FDD kimemtangaza Rais Pierre Nkurunziza kama kiongozi mkuu wa kudumu au kiongozi wa milele ndani ya chama hicho.

 Hatua hii ni mwendelezo wa 'ulevi' wa madaraka kwa watawala wa bara la Afrika ambao pindi wanapoingia madarakani huanzisha harakati za kuendelea kutawala ikiwamo kubadilisha katiba za nchi zao ili kuwaruhusu kuendelea kutawala .
 
 Rais wa Burundi,Pierre Nkurunzinza

Uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao vya siku tatu vya mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika eneo la Buye alikozaliwa Bwana Nkurunziza Kaskazini mwa nchi hiyo.

Uamuzi huo pia unachukuliwa wakati Burundi inajiandaa kufanya marekebisho ya katiba ili kumruhusu Rais Nkurunziza kuendelelea kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.

Taaarifa fupi ya chama cha CNDD/FDD imesema vikao hivyo vilinuwia kuimarisha chama tawala na taasisi zake,alinusurika kupinduliwa mwaka 2015
Lakini pia chama hicho kimechukua uamuzi wa kumuongezea hadhi na kumpa cheo cha juu Rais Nkurunziza na hivyo kumtangaza kuwa ni kiongozi mkuu wa kudumu ndani ya chama.

Kwenye hafla na makundi ya utamaduni ya chama tawala, katibu mkuu wa CNDD/FDD Bwana Evariste Ndayishimiye aliutangazia umati azimio hilo alolitamka kuwa ni muhimu mno katika uhai wa chama tawala.

Tangazo hili la chama tawala CNDD/FDD kumfanya Rais Nkurunziza kama Kiongozi Mkuu wa Kudumu linajiri wakati Burundi inajiandaa kwa kura ya maoni kuhusu Marekebisho ya Katiba baadae mwezi Mei. 

 Kati ya mambo mengi katiba hiyo ikipitishwa itamuwezesha Rais Nkurunziza kuweza kuwania Urais mpaka mwaka wa 2034.

Nkurunziza ni mcheza soka mashuhuri pia nchini Burundi
Wadadisi wengi wa siasa za Burundi wanaamini kuwa hatua hii ya chama tawala inanuwia kumalizia mapema mjadala wa mtetezi wa kiti cha Urais kwa niaba ya Chama hicho na kuonyesha mustakabali wa uongozi kabla hata uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2020.

Lakini pia uamuzi huo unapeleka ujumbe kwa wafuasi wa CNDD/FDD na haswa viongozi wenye nia pengine ya kuwania nafasi hiyo na hivyo kujaribu kukiepusha chama tawala na mpasuko kama ilivyotokea mwaka wa 2015 katika mzozo kuhusu muhula wa sasa wa Rais Nkurunziza.

Isitoshe kwa Wachambuzi wa siasa bado wanaiona hatua hii ya Rais Nkurunziza kutangazwa Kiongozi wa maisha kuwa dalili tosha ya jinsi kiongozi huyo alivyokidhibiti chama cha CNDD/FDD. 
 Rais wa Burundi,Pierre Nkurunzinza(kulia)akisakata soka mjini Bujumbura hivi karibuni.
Chanzo:BBC Swahili

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni