Mamlaka ya maji
safi na usafi wa mazingira Mjini Moshi(MUWSA) inahudumia wakazi wapatao 194,756
hii ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 pamoja na wakaazi
wengine 30,000 waliopo maeneo ya wilaya za Hai na Moshi Vijijini.
Kwa sasa Mamlaka hiyo
inao wateja wapatao 23,123 ambao wanapata huduma ya maji safi na salama kutoka
chemichemi nne na visima virefu vinne ambako uzalishaji wa maji safi na salama
unakadiliwa kuwa ni wastani wa mita za ujazo 34,944 kwa siku iikilinganishwa na
mahitaji ya mita za ujazo 45,082 kwa siku.
Hali ya upatikanaji wa
maji safi na salama kwa wakazi wa mji wa moshi kwa sasa ni wastani wa saa 18
hadi 24 kutegemea na eneo lilivyo ambapo mamlaka hiyo imeugawa mji wa moshi
katika kanda tisa ambazo ni Maili sita, Shanty Town, Soweto,City
Centre,Majengo,Bomambuzi,Chekereni na Himo.
Mamlaka hiyo ambayo ni
moja ya mamlaka kubwa hapa nchini,imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha
huduma kwa wakazi wa mji wa moshi ikiwamo utekelezaji wa miradi
mbalimbali yenye lengo la kuongeza maji na kuwafikia wateja wengi zaidi.
Miongoni mwa miradi hiyo
ni pamoja na ujenzi wa chanzo kipya cha maji ya Coffee Curing chenye
uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 700 kwa siku,ujenzi wa chemchem ya mto karanga
mradi utakaoongeza mita za ujazo 3,800 kwa siku.
Pamoja na jitihada hizo
nzuri za MUWSA katika kuwapatia huduma bora ya maji safi na salama wakazi wa
mji wa moshi na maeneo ya mji mdogo ya Himo,zipo changamoto kadhaa zinazoweza
kukwaza ndoto hizo.
Moja ya changamoto hizo
ni kuwapo na wateja wasiolipia ankara za maji kwa muda mwafaka na hivyo kuwapo
na malimbikizo makubwa ya madeni na hawa hatuna budi kuwaita wadaiwa sugu.
Miongoni mwa wadaiwa
hawa sugu ni taasisi za serikali ambazo zinadaiwa kiasi cha sh,Milioni
800,fedha hizi ni nyingi sana na endapo zitalipwa zinaweza kutumika kuboresha
miundombinu ya maji na wananchi wakapata maji ya uhakika bila ya mgao .
Deni hilo ambalo
linatajwa kuendelea kuongezeka limekuwa kikwazo kwa juhudi za Muwsa za kufikisha huduma bora ya maji safi na salama na uondoaji wa maji taka kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo.
Akitoa taarifa ya
utekelezaji wa shughuli za mamlaka hiyo hivi karibuni kwa Naibu Waziri wa maji
Amos Makalla,kaimu mwenyekiti wa Bodi hiyo,Elizabert Maro Minde,aliiomba wizara
ya maji kuingilia kati deni hilo kwa kuzibana taasisi hizo ili ziweze kulipa
madeni yake.
Minde alizitaja Taasisi
hizo kuwa ni pamoja na jeshi la polisi,Chuo cha mafunzo ya Taaluma ya jeshi la
polisi nchini(MPA) zamani kikiitwa CCP,jeshi la magereza na Idara ya Mahakama
na kuongeza kuwa licha ya mamlaka hiyo kujitahidi kukusanya madeni,imefika
pahala inashindwa.
Makalla alikuwa katika
ziara ya siku mbili mkoani Kilimanjaro ambako pamoja na mambo mengine alizindua
chanzo kipya cha maji kilichopo mto karanga ambacho kinazalisha mita za ujazo
3,800 kwa siku na kunufaisha maeneo ya Bomambuzi,Pasua,Matindigani,Kaloleni,Soweto
na Kiboriloni.
Mamlaka hiyo ililalamika
mbele ya Makalla kwamba Taasisi hizo za serikali hazitoi kipaumbele katika
kulipa madeni hayo licha ya ukweli kwamba kila mwaka zimekuwa zikipata fedha
kutoka kwenye bajeti za wizara zao kwa ajili ya kulipia huduma za maji na
mahitaji mengine.
Ni kweli kwamba taasisi
nyingi za serikali zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara na watoa huduma kwa
kushindwa kulipia huduma wanazopewa na taasisi mbalimbali licha ya kwamba
wizara zao hutenga kwenye majeti zake fedha kwa ajili ya taasisi zilizo chini
yake.
Malalamiko haya yamekuwa
ni ya siku nyingi na sasa yanaonekana kuwa sugu kutokana na taasisi husika
kutoona umhimu wa kulipia huduma hizo licha ya kuzihitaji kwa udi na uvumba na
hivyo kuibua malumbano baina ya watoa huduma na watumiaji wa huduma.
Pamoja na mamlaka hiyo
kuendelea kuzidai taasisi hizo,walimweleza Makalla kwamba bado wanaendelea
kuzipatia huduma ya maji bila kusitisha huduma hizo kwa kile walichodai ni
kutokana na mahitaji makubwa ya maji katika maeneo husika ya wadaiwa hao.
Kwanza ni jambo la
kuwapongeza MUWSA kwa kuonyesha moyo wa huruma wa taasisi hizo nyeti ambazo kwa
hakika zikisitishiwa huduma hiyo panaweza pakatokea mtikisiko mkubwa unaoweza
kuchafua hali ya hewa.
Wakati nikiwapongeza mamlaka
hiyo kwa kuonyesha uungwana kwa wadaiwa hao sugu,nashindwa kupata jibu la moja
kwa moja kwamba ni kweli taasisi hizo hazina uwezo wa kulipia ankara za maji
kiasi cha kuonewa huruma ya kutokusitishiwa huduma hiyo?
Swali hili haliwezi
kupata majibu kwa sababu wakati MUWSA wakiwaonea huruma wadaiwa hawa wa
mamilioni ya fedha,imekuwa mstari wa mbele kuwasitishia huduma wateja wake
ambao madeni yao hayafikii hata robo ya fedha wanazozidai taasisi hizi.
Napata wakati mguu
kuelewa ni mfumo upi unaotumiwa na mamlaka hiyo kuwasitishia huduma wateja wake
wadogo baada ya kuwatumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu zao za
kiganjani na kuwapa siku saba wawe wameshalipia ankara zao.
Kama MUWSA wameweza
kuwakabili wateja wadogo kwa kuwasitishia huduma za maji kwa kuwatumia ujumbe
huo wa simu,wanashindwaje kufanya hivyo kwa wateja hao wakubwa ambao sasa
wanaendelea kutumia huduma wasiyoilipia bila hofu wala woga.
Ni ajabu na kweli
kwa mamlaka kubwa kama hii kuanza kulia lia bila kuchukua hatua za kukabiliana
na wadaiwa sugu kama magereza,polisi na Idara ya mahakama ambazo kila mwaka
hupokea fedha kwa sababu ya ulipiaji wa ankra za maji,tuwaulize fedha hizo
wanazipeleka wapi ?
Minde alilalamika mbele
ya Makalla kwamba deni hilo limewarudisha nyuma na wakamuomba kwa dhamana
aliyopewa na rais (Jakaya Kikwete)alivalie njuga deni hilo kwa madai kwamba
taasisi hizo hazilipi kipaumbele deni hilo kwa sababu eti wanaona mamlaka hiyo
ni taasisi ya serikali kama walivyo wao.
Kiasi hicho cha fedha
pia kingetosha kukamilisha miradi mbali mbali ambayo mamlaka hiyo wanaitekeleza
kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maji hivyo kutosheleza mahitaji ya wakazi
wa mji wa moshi ambako baadhi ya maeneo yamekuwa hayana maji ya uhakika.
Mtazamo wangu ni kwamba
MUWSA wachukue hatua sasa dhidi ya wadaiwa hawa sugu ikiwamo kuwasitishia
huduma ya maji badala ya kulia kulia na kuishia kufukuzana na wateja
wadogo,kwani waswahili wanasema sheria ni msumeno.
Kwa maoni: +255752847877
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni