Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,
mkoani Kilimanjaro imeingia katika kashfa ya uvamizi na uporaji wa mali za
wafanyabiashara wa Mananasi baada ya kuvamia usiku wa manane katika eneo la
maegesho ya magari wakidai ushuru wa mazao hayo.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea
usiku wa kuamkia Desemba 19 mwaka jana katika eneo la maegesho ya magari la
Manyema lililopo katika Manispaa ya Moshi.
Magari yaliyokuwa na mananasi yenye
thamani ya shilingi milioni 54 yenye namba za usajili T 884 ALF
Suzuki Forward, T 667 AAM Fuso Mitsubishi na T 149 ADD Fuso hayajulikani
yalipo mpaka sasa.
Akizungumza katika eneo la tukio Mlinzi
wa Kampuni la Chui Security Co. Ltd aliyefahamika kwa jina la Benjamin Mayalla
alisema watu 20 wakiwemo askari wawili waliokuwa na silaha za moto walimweka
chini ya ulinzi na kutakiwa kutofanya chochote mpaka wamalize kilichowaleta.
Mlinzi huyo alitii amri ya watu hao,
ambao kati yao aliwabaini kuwa ni askari wa Manispaa ya Moshi waliovalia kiraia
huku wakiwa na magari mawili, moja kati ya hayo lilikuwa ni ‘breakdown’
‘Majira ya saa 8 za usiku nikiwa kwenye
lindo la kazi, walifika watu 20, wawili wakiwa na silaha za moto walivunja geti
kwa kutumia bomba la chuma na kuingia katika eneo la maegesho na kunitaka
nisalimu amri, kitu ambacho nilitii kibaya zaidi ilikuwa ni kuyafungua magari
matatu kwa funguo za bandia walizokuwa nazo,’ alisema Mayalla
Mayalla aliongeza kusema magari mawili
kati ya hayo yalikubali kuwaka na moja walilivuta na ‘breakdown’ hata kukwangua
sehemu ya maegesho na kuyapeleka kusikojulikana.
Kwa upande wao wamiliki, madereva wa
magari hayo waliojitambulisha kwa majina Absamadu Ivere, Shaban Juma na Malaki
Mlay walisema walifika jioni ya Desemba 18 mwaka jana mjini Moshi wakitokea
Bagamoyo kununua mananasi hayo kwa ajili ya kuyauza Jijini Arusha na Babati waliyapeleka
katika eneo la maegesho kwa ajili ya kuendelea na safari siku inayofuata.
‘Alfajiri tulipofika kwa ajili ya
kuendelea na safari yetu, huku tukiwa na funguo za magari tulitaarifiwa na
mlinzi kuwa maaskari wa manispaa wamevamia na kuyachukua magari yote na yeye
(mlinzi) kumweka chini ya ulinzi licha ya kutomdhuru wamechukua magari yetu na
mzigo wetu wote (mananasi) na hatujui walikopeleka,’ alisema Absamadu
Ivere.
Pamoja na juhudi za
wafanyabiashara hao kudai kupeleka taarifa kwa mkuu wa kituo cha Polisi Moshi,
Afande Kasindo aliwajibu kuwa kama waliohusika ni Askari wa Manispaa, hawana
budi kutoa taarifa kwa Mkurugenzi ambako maswali mengi yakishindwa kupatiwa
ufumbuzi huku Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro Geoffrey
Kamwela akidai kutopata taarifa yoyote tangu siku ya tukio na kuahidi
kulifanyia uchunguzi.
Akizungumza kwa njia ya simu Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Shaban Ntarambe amekiri kuwepo kwa
tukio hilo ingawa tayari kesi hiyo imepelekwa Mahakamani.
Hata hivyo, majibu ya mkurugenzi huyo
kuwa kesi hiyo imefikishwa mahakamani, yanazua utata zaidi huku wafanya
biashara hao wakiwa njiapanda kwani hawajaitwa mahakama yoyote ile kutoa
utetezi wao.
Itakumbukwa kwamba askari wa Manispaa
ya Moshi wamekuwa na tabia ya kuchukua mali za wafanyabiashara na kisha
kugawana wao kwa wao kutokana na ukweli kwamba hakuna anayefuatilia hatma ya
mali zikiwa mikononi mwa mamlaka hiyo.
CHANZO: JAIZMELALEO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni