JESHI la polisi mkoani
Kilimanjaro,limemtia mbaroni mfanyabiashara maarufu katika miji ya Moshi
na Arusha,Wilfred Lucas Tarimo kwa kutuhuma za kukutwa na mapipa
kumi yaliyosheheni kemikali bashirifu zilizopigwa marufuku na serikali.
Tarimo ambaye pia ni mmoja wa
wakurugenzi wa Kampuni ya Derrick Global Trading(D.G.T) ya mjini Moshi
watengenezaji wa pombe aina ya banana kupitia kinywaji chake cha
Budget,alikamatwa hivi karibuni na polisi pamoja na mkewe aliyetajwa kwa jina
moja la Irene.
Kaimu kamanda wa polisi mkoani
Kilimanjaro,Koka Moita alidhibitisha kukamatwa kwa mfanyabaishara huyo
alipozungumza na mtandao huu na kwamba upelelezi juu ya tuhuma hizo unaendelea.
Kwa mujibu wa kamanda Koka,tayari
ofisi ya Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa(RCO) imemwandikia barua
mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara kemmikali
hizo na kubaini aina ya kemikali husika pamoja na thamani yake.
“Ni kweli hilo tukio la Wilfred
Tarimo lipo,amekamatwa na mapipa kumi ya kemikali na nimezungumza na RCO
amesema tayari wameshamwandikia barua mkemia mkuu wa serikali li waje
kuzifanyia uchunguzi wa kimaabara hizo kemikali na hapo ndipo tutajua aina ya
kemikali na thamani yake kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa”,alisema
Koka.
Mtandao huu umezungumza na mkemia mwandamizi wa serikali
kanda ya Kaskazini,Christphera Anyango kutaka kujua namna wanavyopokea sampuri
kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.
Kwa mujibu wa Anyango,ofisi yao
hupokea sampuli mbali mbali kutoka polisi na kuzifanyia uchunguzi na kwamba pia
wanaweza kuchukua sampuli wenyewe kulingana na mahitaji ya wahusika.
“Polisi wanaweza wakaleta sampuli
wenyewe na kama kuna kitu kinahitaji utaalamu zaidi wanatuandikia barua na sisi
tunakwenda kuchukua wenyewe na kuzifanyia uchunguzi”,alisema.
Alipoulizwa kama wameshapokea barua
kutoka ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai(RCO) mkoa wa Kilimanjaro
kwa ajili ya kwenda kuchukua sampuli za kemikali zilizokamatwa kwa
mfanyabiashara huyo,ofisa huyo alisema yupo nje ya ofisi.
Hata hivyo aliomba atafutwe ofisa
mwenzake aliyemwachia ofisi aliyetajwa kwa jina la Joyce Njisya ambaye
amekiri kupokea barua hiyo kutoka polisi Kilimanjaro alipozungumza na Jamhuri.
Akizungumza na mtanao huu kwa nija ya simu,Joyce amesema kuwa yatari
wameshachukua sampuli za kemikali hizo na kuzituma makao makuu ya ofisi ya
mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.
“Ni kweli hiyo barua tumeshaipokea
na tumeshachukua sampuli na kuzipeleka makao makuu yetu kwa ajili ya
uchunguzi,tukikamilisha uchunguzi wetu tutarejesha majibu ya uchunguzi kwa
polisi,wao ndo watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuyatolea majibu”,alisema.
Hata hivyo mfanyabiashara huyo hakukiri
wala kukanusha kukamatwa na shehena ya kemikali zilizopigwa marufuku na
serikali kwani baada ya kupigiwa simu alidai yupo kwenye kikao na aliahidi
kuwasiliana na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kikao hicho lakini
hakufanya hivyo.
Na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa
maandishi kupitia simu yake ya kiganjani,bado mfanyabiashara huyo hakuweza
kujibu maswali aliyoulizwa na mwandishi wa habari hizi.
“Mr.Wilfred Tarimo habari za
leo?,naitwa Charles Ndagulla mwandishi wa habari gazeti la Jamhuri,unazungumziaje
tuhuma za wewe na mke wako Irene kukamatwa na polisi mkituhumiwa kukutwa na
mapipa kumi yenye kemikali bashirifu zilizopigwa marufuku na
serikali?,unasomeka ujumbe huo.
Kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo
kunakuja siku chache baada ya maofisa wa Mamlaka ya Chakula la
Dawa(TFDA)Kanda ya kaskazini,kukifunga kiwanda hicho cha kutengeneza pombe aina
ya Banana cha Derrick Global Trading(D.G.T ) baada ya kubainika kuwa na
kasoro .
Kiwanda hicho kilifungwa chini ya
kifungu cha 181 sura ya 209 ya sheria ya chakula na dawa ya mwaka 2003 kutokana
na tuhuma za kutumia nembo ya kiwanda kingine cha kutengeneza pombe kali
kinyume cha sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari
kiwandani hapo hivi karibuni,Mkaguzi wa chakula mwandamizi kutoka TFDA Kanda ya
kaskazini,William Mhina,alisema sababu nyingine za kufungwa kwa kiwanda
hicho ni mazingira yasiyoridhisha ya kiwanda hicho.
Alitaja sababu zingine ni
wafanyakazi kutokuwa na vyeti vya kuonyesha afya zao huku wafanyakazi hasa wa
kike kutokuvaa kofia kichwani.
Alisema uchunguzi wao umebaini
kuwa,eneo la kuoshea chupa ni chafu na kwamba chupa hizo zimekuwa zikioshwa
katika mazingira yasiyoridhisha.
Alisema wamiliki wa kiwanda hicho
wamepewa muda wa kurekebisha kasoro hizo na baada ya kufanya hivyo TFDA itafanya
ukaguzi tena kujiridhisha kama kasoro hizo zimefanyiwa kazi,
Mbali na kufungwa kwa kiwanda
hicho,jeshi la polisi kwa kushirikiana na maofisa wa mamlaka ya mapato
Tanzania(TRA),walifanikiwa kukamata shehena ya vifungashio vinavyotumiwa
na kampuni moja mkoani Shinyanga ya Canon General Supply inayojihusisha
na utengenezaji wa pombe kali aina ya Shujaa.
Vifungashio hivyo vilikamatwa ndani
ya kiwanda hicho kilichopo eneo la Kwa Alphone kata ya Kibolironi huku
baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho wakishikiliwa na jeshi la polisi kwa
mahojiano zaidi.
Akizungumzia tukio hilo,ofisa huyo
kutoka TFDA alisema hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria inayosimamia usajili wa
bidhaa na kuongeza kuwa,vifungashio vilivyokamatwa ndani ya kiwanda hicho
havimo kwenye orodha ya usajili wa bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo.
Kwa upande wake kamanda wa polisi
mkoa wa Kilimanjaro,Hamisi Issah alisema jeshi hilo linamshikilia meneja wa
Kiwanda hicho aliyemtaja kwa jina la Boniface Damas(56) pamoja na wafanyakazi
watatu wa kiwanda hicho.
Kamanda Issah aliwataja wafanyakazi
hao kuwani Severine Pantaleo(37),Riziki Fabian (28) na Daniel Japhet(18) ambao
wanadaiwa kukutwa na pombve kali iliyofungashwa kwenye viroba iana ya Zed
inayodaiwa kutengenezwa kienyeji.
“Viroba hivyo vina alama zake,lakini
watuhumiwa hawa walikuwa wakitengeneza katika mfumo wanaoujua
wenyewe,utengenezaji wa pombe usiozingatia taratibu ni hatari na unaweza kuleta
madhara makubwa kwa wanywaji”,alisema kama Issah.
Kuhusu vifungashio vilivyokamatwa
ndani ya kiwanda cha D.G.T,kamanda Issah alisema kuwa,wamiliki wa kiwanda hicho
hawakuwa na haki stahiki ya kutengeneza pombe hizo kutokana na kutengeneza
pombe hizo pasipo kuzungitia tararibu za kisheria.
Kamanda Issah amesema polisi kwa
kushirikiana na TFDA wanafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo ikiwamo matumizi ya
malighafi isiyo ya kiwanda hicho na uchunguzi ukikamilika sheria itachukua
mkondo wake kwa watakaobainika kutenda makosa.
Hata hivyo tangu kukamatwa kwa
watuhumiwa hao uchunguzi wa Jamhuri umebaini kuwa mpaka sasa hawafikishwa
mahakamani.
MWISHO