Jumatano, 30 Mei 2018

MMILIKI SHULE YA SCOLASTICA KUENDELEA KUSOTA RUMANDE,UPELEZI KESI YAKE BADO NGOMA NZITO


 Edward Shayo,mmiliki wa shule binafsi ya sekondari ya Scolastica iliyopo mji mdogo wa Himo mkoani Kilimanjaro,anakabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo,Humphrey Makundi aliyeuawa Novemba 6 mwaka jana,pichani akiwa na pingu mikononi akipelekwa kizimbani.


NA CHARLES NDAGULLA,MOSHI

MMILIKI wa shule binafsi ya sekondari ya Scolastica iliyopo katika Mji Mdogo wa Himo mkoani Kilimanjaro,Edward Shayo ataendelea kusota rumande katika Gereza kuu la mkoa la Karanga kutokana na upelelezi wa kesi  ya mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo kutokukamilika.

Shayo na wenzake wawili wanashitakiwa na Jamhuri kwa mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo,Humphrey Makundi(16)anyedaiwa kuuawa Novemba 6 mwaka jana.

Washitakiwa hao wamerejeshwa tena rumande leo May 30 baada ya upande wa Jamhuri kuieleza mahakama ya hakimu mkazi iliyoketi chini ya Hakimu Julieth Mawole kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

 Kesi hiyo sasa itatajwa tena mahakamani hapo Juni 13 mwaka huu huku ndugu wa washitakiwa hao akiwamo mke wa mmiliki wa shule hiyo Mama Scolastica Shayo wakiondoka makahamani hapo kwa unyonge.

Shayo ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo amekuwa haamini kilichotokea kwani tangu  aliposomewa shitaka la mauaji ya kukusidia kwa mara ya kwanza Novemba 27 mwaka huu,amekuwa katika hali ya majonzi huku akitoa raia kwa ndugu zake kumwombea.

Mbali na Shayo,washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ni Hamis Chacha ambaye ni mlinzi wa shule hiyo pamoja na Makamu mkuu wa shule hiyo,Laban Nabiswa .


Walisomewa shitaka hilo kwa mara ya kwanza na wakili wa serikali Cassim Nasri akisaidiwa na wakili mwenzake wa Serikali Faygrace Sadallah mbele ya hakimu  Julieth Mawole .

Akisoma hati ya mashitaka,wakili Nasri alidai kuwa,mnamo Novemba 6 mwaka jana huko maeneo ya  Himo wilaya ya Moshi,washitakiwa kwa pamoja walimuua kwa makusudi mtu mmoja aitwaye Humphrey Makundi.

Baada ya kusomewa shitaka hilo,washitakiwa hao hawakautakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji hadi mahakama kuu.

 
HUMPHREY MAKUNDI ALIVYOUAWA KIKATIRI



1.Novemba 6 mwaka jana mwanafunzi huyo alidaiwa kutoweka shuleni hapo

2.Novemba 10 mwaka jana mwili wake uliokotwa ndani ya Mto Wona na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa,Mawenzi

3.Novemba 12 mwili wa marehemu ulizikwa na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga baada ya kutojitokeza ndugu wa kuutambua 

4.Novemba 17 mwaka jana mahakama ya hakimu mkazi mjini moshi ilitoa kibali cha mwili huo kufukuliwa baada ya ndugu wa marehemu kubaini kuwa mwili uliozikwa katika makaburi hayo ni wa mtoto wao.

MWILI  ULIVYOFANYIWA  UCHUNGUZI


Mwili wa marehemu Humphrey ulifanyiwa uchunguzi na madaktari katika Hospital ya rufaa ya KCMC na kushuhudiwa na Baba mzazi wa marehemu na katika uchunguzi huo,ikibainika marehemu alikatwa na kitu chenye ncha kali kiunoni,mgongoni,kwenye mapaja na mbavu mbili zilivunjika.

Baba mzazi huyo akawaeleza wanahabari kuwa kulingana na majibu ya uchunguzi huo ni ukweli ulio wazi kuwa,mwanaye aliuawa na kwamba kifo chake kinatia shaka na kuvitaka vyombo vya uchunguzi kuwasaka wahusika wa mauaji ya mtoto wake mpendwa.

SHULE WALIVYOSUSIA MAZISHI YAKE


Katika  hali ya kusikitisha na kushangaza,uongozi wa shule hiyo,ulisusia mazishi ya marehemu Humphrey  yaliyofanyika DEesemba 2 mwaka jana katika Kijiji cha Komakundi wilaya ya Moshi Vijijini.

Uongozi wa shule hiyo haukuweza kutuma mwakilishi katika mazishi hayo ambayo yaliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira huku ibaada ya mazishi ikiongozwa na msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma ,Mchungaji Samwel Mshana.

 Edward Shayo wa pili kutoka kushoto(hajafungwa pingu) akiwa na washitakiwa wenzake wakipelekwa kizimbani,Shayo  na wenzake waanakabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya Scolastica,Humphrey Makundi.


Jumamosi, 26 Mei 2018

TENGENI MUDA WA KUZUNGUMZA NA MUNGU,WAKRISTO WAASWA




WITO  umetolewa kwa wakristo nchini kujenga tabia ya kutenga muda wao kuzungumza na mungu badala ya kutegemea siku  za ibaada makanisani.

Wito huo umetolewa hivi karibuni  na Makamu Mkuu wa Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of  God (TAG)Dkt .Magnus Mhiche  wakati wa Ibada ya uzinduzi wa Hema la kuabudia la Kanisa la International Christian Centre (ICC) lililoko Soweto mjini Moshi .

Dkt.Mhiche alisema,wakristo wanao wajibu wa kuzungumza na mungu pahala popote iwe makazini,safarini na hata majumbani mwao badala ya kusubiri kwenda makanisani kuhudhulia ibaada.

Askofu  Mhiche alisema kuwa kuna Wakristo wanaoheshimu majengo ya Makanisa kuliko kumuogopa Mungu mwenyewe na kwamba wanapotoka Makanisani humuacha Mungu na kuendelea na mambo yao maovu.

“Kuna watu wanapokuwa Makanisani wanaonekana ni watu waliookoka, wenye unyenyekevu, lakini ukifuatilia matendo yao na mienendo yao haiendani na ukristo wao, nawasihi sana hebu badilikeni acheni kumdhihaki Mungu, Mungu anahitaji ushirika na wewe Mkristo,”alisema  Mhiche.

Aidha Askofu  Mhiche alizungumzia umuhimu wa kutenga muda wa maombi na sala na kutoa rai kwa waamini kuacha kumdhihaki Mungu pale tu wanapokuwa kwenye nyumba za Ibada pekee, ambapo alisema kuwa wakishatoka huko huendelea kutenda dhambi.
 Makamu Mkuu wa Kanisa la TAG,Askofu Magnus Mhiche akiomba kabla ya uzinduzi wa Hema la kuabudia la Kanisa la International Christian Centre(ICC)lililopo Soweto Mjini Moshi,kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira.

“Mungu alipotuumba alitaka tuwe na ushirika na yeye, Ibada ni mfumo wa ushirika, tunapokutana kwenye makanisa yetu huo ni ushirika wako wewe na mimi,” alisema.

Alisema licha ya kuwa watu wote hujua umuhimu wa maombi, wengi wao wanaugumu wa kutenga muda kwa ajili ya maombi wakati wakiwa makazini,safarini na majumbani mwao.

Askofu Mhiche aliwakumbusha wakristo  kuwa ukweli wa moyo wa binadamu daima huwa katika maombi na kuwataka wabadilike kwa  kutenga muda wa kutafakari juu ya mema anayowatedea mwenyezi mungu.

Akawageukia maaskofu na kuwataka waendelee kuwasaidia washirika kutambua majira na nyakati za ulimwengu wa sasa katika  kipindi hiki ambacho watanzania wengi wanaendelea kulalamika ya kuwa hali ya uchumi ni ngumu.

“Mimi wakati wa utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere nilikuwa nasoma kidato cha nne,nimeshuhudia pia utawala wa Marais Mwinyi, Mkapa na Kikwete, wote hawa sikuwahi kumuona hata mmoja wao akiwagawia Watanzania fedha”, alisema.

Alisema wanaoendelea kulialia kuwa hali ni mbaya ama vyuma vimekaza hao ni wale ambao walikuwa wamezoea kuwanyonya baadhi ya watanzania ambao ni watu wa hali ya chini.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Magharibi la Kanisa hilo, Dkt Benjamin Bukuku, alisema kuwa makanisa ya TAG yanakabiliwa na upungufu wa wachungaji hivyo kuomba wachungaji kupelekwa ili kwenda kutoa huduma ya kiroho.

“Bado Kanisa linawajibu mkubwa wa kuendelea kupata makazi ya Kanisa ya kuabudia, kujengwa kwa hema hili kutawezesha waumini kuweza kupata huduma ya kiroho mahali hapa,” alisema.

Naye  mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amelipongeza kanisa la International Christian Centre (ICC), lililoko chini ya TAG, kwa kuona umuhimu wa kujenga hema hilo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa madhehebu ya dini yamekuwa msaada mkubwa kwa serikali katika kuwahudumia watanzania na kuachana na mambo maovu.

Aidha mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa serikali inathamini mchango wa taasisi za dini katika kudumisha amani, utulivu na mshikamano hapa nchini.

Mghwira alisema ya kuwa serikali inatambua huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi za dini ikiwemo Elimu, Afya, miradi ya maji na miradi mingine ya kimaendeleo.

Alisema serikali itaendelea kutoa michango ya hali na mali pale inapowezekana ili kuhakikisha raia wake wanapata maendeleo na wanaishi kwa furaha na utulivu.


Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa hema hilo Mchungaji kiongozi wa Kanisa la International Christian Centre (ICC) Askofu Mstaafu wa TAG Glorius Shoo alisema  hema hilo limegharimu kiasi cha shilingi milioni 100 hadi kukamilika kwa ujenzi huo.

Pia  mchungaji Shoo alimpongeza Rais Dkt John Magufuli kwa kuwapatia eneo hilo ili waweze kujenga jengo ambalo litatumika kutolea huduma za kiroho na za kimwili mahali hapo.
 
 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira akisalimiana na Viongozi wa Kanisa la TAG muda mfupi kabla ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa Hema la kuabudia la kanisa International Christian Centre(ICC) eneo la Soweto mjini Moshi ambalo lipo chini ya TAG.

MUWSA SASA KUWAUNGANISHIA MAJI WANANCHI WA URU KWA MKOPO


 Na FINA LYIMO,MWANANCHI,MOSHI.

Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira   Mjini Moshi  (MUWSA) imeanzisha mpango maalumu wa kuwaunganishia wananchi huduma ya maji safi na salama  kwa njia ya mkopo ikiwa ni mkakati wa mamlaka hiyo kuwafikia wananchi wengi.

Ofisa habari wa mamlaka hiyo, Rashid  Nachan amesema mpango huo  utawanufaisha   zaidi ya wananchi 34,000  kutoka  kata za Uru Kaskazini na Uru Kusini zilizopo  wilaya ya Moshi  Vijijini  kutokana  na wananchi wa maeneo hayo  kukosa huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.

Alisema  tayari mamlaka hiyo  imetumia zaidi ya shilingi  Bilioni mbili  kwa ajili ya  kuchukua maji kutoka  kwenye chanzo cha maji cha Mang'ana kilichopo ndani ya hifadhi ya Taifa ya mlima Kilimanjaro.

“Mamlaka imeamua kutoa huduma kwa njia ya mkopo ili wananchi wote  waweze kupata maji kutokana na wananchi kushindwa kulipa  fedha za kuunganishiwa huduma ya maji kwa mkupuo”alisema.

 Kwa mujibu wa ofisa habari huyo wa MUWSA,mpango huo utavinufaisha vijiji  11 vilivyopo katika kata hizo mbili na kwamba tangu mradi  huo uzinduliwe mwaka jana tayari  kaya 1000  zimeweza  kulipa huduma ya maji kwa mkupuo na kupata maji safi na salama.
 
 Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya maji safi na Uondoshaji wa taka Moshi mjini(MUWSA),Joyce Msiru

Naye diwani wa kata ya Uru kusini Wilhad Kitali, alisema wananchi ndio waliomba mradi huo wa maji na mamlaka kuona umuhimu na kuwaletea  lakini wanashindwa kulipa garama kwa mkupuo kutokana na hali duni ya maisha  ya wananchi hao.

Kitali alisema mpango huo wa kuunganishiwa huduma ya maji kwa  njia  ya mkopo itawarahisishia wananchi kilipa kidogo kidogo na hatimae kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 2 kwenda kuchota maji katika mto Rau.

Alisema awali wananchi walikuwa na dhana potofu ya kuwa maji ni ya bure na kwamba  hayalipiwi  lakini kwa sasa wamepatiwa elimu na wamekubali kufungiwa maji hayo kwa njia ya mkopo kwa kuingia mkataba MUWSA.

Mmoja Wa wananchi kata ya Uru Kusini Rogath Simba alisema hatua yakuunanishiwa  maji kwa njia ya mkopo  imekuwa chachu kwa  wananchi wengi kuhamasika na tayari wameshaanza kulipa ili waweze kupatiwa huduma hiyo muhimu.

Jumamosi, 19 Mei 2018

RUSHWA YA NGONO YATIKISA ARUSHA SERENA HOTEL



 Arusha Serena Hotel,Resort and Spa
 

 NA CHARLES NDAGULLA,ARUSHA

RUSHWA  ya ngono ni moja ya vitendo ambavyo vimekuwa vikiwakwaza wanawake katika  kupata ajira maeneo mbali mbali duniani hatua ambayo inatajwa kama moja ya changamoto kubwa katika mafanikio yao.

Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo,wapo baadhi yao ambao licha ya kuwa na sifa za kuajiliwa wamejikutaka wakikosa fursa hizo kutokana na kushindwa kutoa rushwa ya ngono kwa wanaosimamia mamlaka za ajira.

Pamoja na  kelele ninyi kupigwa kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu yakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali  juu ya kukithiri kwa vitendo hivyo,mambo bado yahajabadilika katika baadhi ya maeneo ya kazi hapa nchini.

Wafanyakazi wa kike katika Hotel ya kitalii ya Arusha Serena Hotel and Resort iliyopo kilometa 4.5 kutoka eneo la Tengeru nje ya Jiji la Arusha ni moja ya wahanga wa matukio hayo ya unyanyasaji wa kingono.

Wafanyakazi hao walioomba kutotajwa majina yao kwa sababu maalumu,wamezungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha na kuelezea kilio chao juu ya vitendo hivyo ambavyo wanadai vinawakwaza katika utendaji kazi wao.

  
Kwa mujibu wa wafanyakazi hao,wamedai wengi wa wanaonyanyasika ni wafanyakazi wa kitanzania huku wafanyakazi kutoka nchini Kenya wakipewa huduma nzuri ikiwamo mishahara minono na maslahi mengine.
 Ndagullablog imezungumza na meneja Raslimali watu wa hotel hiyo John mwamakula juu ya malalamiko ya wafanyakazi hao kunyanyaswa kingono na baadhi ya maofisa wa hotel hiyo akiwamo meneja wake Filex Ongembo.

Katika mahojiano na Ndagullablog ofisini kwake wiki hii,Mwamakula hakukiri wala kukanusha malalamiko hayo huku akisisitiza vitendo hivyo ni kinyume na sera ya hotel hizo.

Amesema sera ya hotel hizo zilizopo maeneo mbali mbali nchini inakataza vitendo hivyo na kwamba anayebainika kufanya hivyo anakuwa katika hatari ya kufukuzwa kazi.

Mwamakula amesema kuwa hawajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi hao kunyanyaswa kingoni lakini akadai zipo njia tatu kwa wafanyakazi hao kuwasilisha malalamiko yao kwa uongozi.

Ametaja njia hizo kuwa ni pamoja na utoaji taarifa kwa njia ya siri(wisow blower),mfanyakazi kwenda moja kwa moja ofisini kwake na kupitia mikutano ya wafanyakazi(Staff General Meeting) ambayo amedai hufanyika kila baada ya miezi mitatu.

“Kwa ujumla hatukubaliani na hivyo vitendo na hata ukiangalia sera yetu inakataza vitendo hivyo na adhabu yake ni kali sana kama ikibainika mtu amehusika na vitendo hivyo tunamfukuza kazi”,amesema.

Hata hivyo meneja huyo alipoulizwa alipo Ongembo amesema hajui alipo zaidi ya kusema hayupo na taarifa ambazo jamhuri limezipata ni kwamba meneja huyo amerejeshwa nchini kwao Kenya.

Malalamiko mengine ya wafanyakazi hao ni kupunguzwa kwa mishahara yao kwa aslimia tano tangu mwaka jana na meneja huyo amekiri kuwepo na punguzo hilo la mishahara kwa wafanyakazi hao.

Akijibu malalamiko hayo,Mwamakula amesema kuwa,makato hayo yalitokana na kuyumba kwa biashara ya utalii mwaka jana madai ambayo wafanyakazi hayo wameyapinga.

 Huduma ya matibabu ni moja ya malalamiko mengine kwa watumishi ambako wanadai mwajili wao kuwaondoa kwenye huduma ya matibabu kupitia bima ya Afya(NHIF) huku wakitibiwa kupitia bima ya Jubilee ambayo wamedai haiwapi nafasi ya kwenda kutibiwa katika hospital za rufaa.

Wametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kutopewa usafiri wa kutoka nyumbani kwenda kazini na kurudi majumbani hali ambayo imewalazimu kutumia zaidi ya shilingi 10,000 kwa siku kama gharama za usafiri fedha ambazo wanadai zinazotoka kwenye sehemu ya mishahara yao.

Licha ya kutopewa usafiri,wafanyakazi hao wamedai kuwa usalama wao uko shakani kutokana na kutumia usafiri wa boda boda usiku wa manane wakati wa kutoka kazini kutokana na boda boda wengi kutowafahamu.

“Tunaomba mtusaidie kwa kweli hali ni mbaya,wafanyakazi wa kitanzania tunanyanyasika sana tofauti na wenzetu wakenya ambao wanaishi vizuri licha ya baadhi yao kutokuwa na hadhi ya kufanyakazi ambazo tunauwezo nazo”,wamesema.

Hata hivyo wafanyakazi hao wamedai  kuwa,wamekuwa katika tishio la kufukuzwa kazi pindi wanapodai kuboreshewa mazingira ya kazi hatua ambayo imewafanya baadhi yao kukaa kimya kwa hofu ya kufukuzwa kazi.

Wafanyakazi hao wameitaka wizara ya kazi,ajira na vijana  pamoja na idara ya uhamiaji Jijini Arusha kufanya uchunguzi wa kina kwa baadhi ya wafanyakazi wa hotel hiyo kutoka nchini Kenya kwani baadhi yao hawana sifa za kufanyakazi hapa nchini.

“Ukienda pale ofisi kuu utawakuta wakenya wamejazana pale wengine hawana sifa za kuwa hapa nchini kwa sababu baadhi ya kazi wanazofanya hazihitaji watu kutoka nje ya nchi,wapo wanafanyakazi kama makatibu mhitasi,je kazi hiyo inahitaji mtu kutoka Kenya?,wamehoji.

  Kuhusu suala la matibabu,Mwamakula amesema kuwa si kweli bima ya Jubilee inawanyima fursa ya kutibiwa katika Hospital za rufaa huku akikiri kujiondoa katika Bima ya Afya ya NHIF.

“Mpango wetu wa matibabu unagusa mfanyakazi na mwenza wake kama ameoa ama kuolewa na watoto wasiozidi wanne wenye umri chini ya miaka 18”,amesema.

Amesema wafanyakazi hao pia ni wanachama wa mfuko wa hifadhi ya Jamii (NSSF) ambako kuna  mpango wa matibabu kupitia fao la matibabu ambako mwanachama anaweza kujiandikisha bila kuathiri michango yake na akachagua Hosptil anayoitaka.

Mbali na huduma hizo,meneja huyo amesema wafanyakazi hao wanayo bima nyingine ambako matibabu yakishindikana hapa nchini wanaweza kupelekewa nchini Kenya kwa matibabu zaidi.