TANGU aingie
madarakani,Rais wa awamu ya Tano,Dk.John Pombe Magufuli amekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha kuwa serikali yake inafanya mapinduzi makubwa katika kuelekea
uchumi wa kati.
Rais Magufuli amekuwa muumini wa Tanzania ya
Viwanda akiamini kuwa ili Taifa lipige hatua kimaendeleo kufikia uchumi wa kati
sharti sekta ya viwanda iimarishwe.
Katika
kufanikisha Tanzania ya viwanda,hivi karibinu serikali ilitangaza zabuni ya ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la
kuzalisha umeme katika maporomoko ya
maji yam to Rufiji yanayofahamika kama Stiegler’s Gorge yanyopatikana ndani ya pori tengefu la
Selous .
Kwa mujibu wa Waziri wa madini,Dk.Medadi Kalemani,mradi huo utazalisha umeme wa kiasi cha megawati 2,100 na na utagharimu kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 2 ambazo zitatolewa na Serikali ya Tanzania.
Dkt. Kalemani amesema malengo ya Serikali ni kuzalisha umeme kiasi cha megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 kama Sera ya Nishati ya mwaka 2015 inavyoelekeza.
"Tunataka kujenga Tanzania ya Viwanda. Tunataka ifikapo mwaka 2019-20 tufike megawati 5,000. Tanzania ya Viwanda inahitaji umeme, mradi kama huu na pia ya Kinyerezi I Extension, MW 185 Kinyerezi II MW 240 na miradi mingine itawezesha kufikia lengo letu," alisema Dkt. Kalemani.
Mbali na
mkakati wa Rais Magufuli kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda,pia amekuwa katika
harakati za kuhakikisha shirika la Ndege Tanzania(ATCL)linafufuliwa kwa kiwango
cha juu pamoja na ununuzi wa ndege mpya.
Lengo la
serikali ya Rais Magufuli ni kuhakikisha shirika hilo la umma linarejea katika
hali yake ili kuinua usafiri wa anga na kuwawezesha watanzania kuendelea
kunufaika na raslimali za Taifa lao.
Hadi sasa
Rais Magufuli amefanikisha ununuzi wa ndege nne zikiwamo mbili aina ya
Dash8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na Dash8-Q300 moja yenye
uwezo wa kubeba abiria 50.
Tayari safari za ndege za shirika
hilo ambazo kwa muda mrefu zilisitishwa,zimeanza ikiwamo safari za Dar es
salaam- Mbeya,Dar es salaam-Dodoma na kwingineko kwa lengo la kuwapatia huduma
bora na kwa bei nafuu watanzania.
Mdau wa maendeleo Jijini Arusha,God'slove Maphie
God’slove Maphie ni mmoja wa wadau
wa maendeleo katika Jiji la Arusha ambaye ameguswa na harakati za Rais Dk.John
Pombe magufuli za kulifufua shirika hilo la ndege ikiwamo ununuzi wa ndege
mpya.
Katika mahojiano maalumu na
mwandishi wa makala haya jijini Arusha,Maphie anasema hatua ya Rais Magufuli
kulifufua shirika hilo ni ya kupongezwa na watanzania wote wapenda maendeleo.
“Mimi sitafuti ajira kwa mheshimiwa
Rais,lakini ni ukweli uliowazi kuwa kitendo cha kulifufua shirika letu la ndege
ni kitendo cha kupongezwa sana hasa katika kuelekea uchumi wa kati”,anasema.
Maphie anasema ilikuwa ni aibu kubwa
kwa nchi kubwa kama Tanzania kutokuwa na shirika lake la ndege linalojiendesha
kwa ufanisi huku nchi ndogo kama Rwanda
yenye watu wachache ikilinganishwa na Tanzania zikiwa na shirika la ndege.
Mbali na hilo pia amepongeza hatua
ya serikali ya Tanzania kuzindua ujenzi wa mradi wa rada nne ambazo zitakuwa mahususi katika
kuhakikisha anga la Tanzania linakuwa salama .
“Unapokuwa huna rada za kuongoza
ndege maana yake ni kwamba anga lako linakuwa haliko salama lakini kwa hatua
hii ya serikali kuanza ujenzi wa rada nne ni hatua nzuri sana kwetu sisi kama
taifa”,anasema.
Pamoja na kupongeza jitihada hizo za
serikali ya Dk.John Pombe Magufuli kulifufua shirika la ndege na ujenzi wa
rada,akashauri usimamizi mzuri wa raslimali hizo za taifa.
Anasema kama hapatakuwa na usimamizi
nzuri katika uendeshaji wa ATCL,basi watanzania watarajie kurejea kule ambako
shirika limetoka baada ya kukosa usimamizi mzuri .
Maphie anasema ni wajibu wa bodi ya
wakurugenzi ya ATCL kuhakikisha shirika hilo halifi kwa kulisimamia vizuri ili
juhudi za Rais Magufuli za kulifufua shirika hilo zilete matunda mazuri.
“Hata wewe mwandishi wa habari ili
ufanye kazi yako kwa ufanisi ni sharti uzingatie miiko ya taaluma yako na hicho
ndicho watanzania wanataka kuona shirika linaendeshwa na watu wanaofuata
misingi na maadili ya taaluma zao”,anasema.
Anasema kuwa,anaamini Rais magufuli
akiuungwa mkono katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo watanzania miaka
michache ijayo Tanzania itapiga hatua kubwa kiuchumi na kuondokana na hali ya
kuwa tegemezi.
Moja ya Ndege za Shirika la Ndege Tanzania(ATCL) ikiwa angani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni