WITO umetolewa kwa wakristo
nchini kujenga tabia ya kutenga muda wao kuzungumza na mungu badala ya
kutegemea siku za ibaada makanisani.
Wito huo umetolewa hivi
karibuni na Makamu Mkuu wa Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies
of God (TAG)Dkt .Magnus Mhiche wakati wa Ibada ya uzinduzi wa Hema
la kuabudia la Kanisa la International Christian Centre (ICC) lililoko Soweto
mjini Moshi .
Dkt.Mhiche alisema,wakristo wanao
wajibu wa kuzungumza na mungu pahala popote iwe makazini,safarini na hata
majumbani mwao badala ya kusubiri kwenda makanisani kuhudhulia ibaada.
Askofu Mhiche alisema kuwa
kuna Wakristo wanaoheshimu majengo ya Makanisa kuliko kumuogopa Mungu mwenyewe
na kwamba wanapotoka Makanisani humuacha Mungu na kuendelea na mambo yao maovu.
“Kuna watu wanapokuwa Makanisani
wanaonekana ni watu waliookoka, wenye unyenyekevu, lakini ukifuatilia matendo
yao na mienendo yao haiendani na ukristo wao, nawasihi sana hebu badilikeni
acheni kumdhihaki Mungu, Mungu anahitaji ushirika na wewe
Mkristo,”alisema Mhiche.
Aidha Askofu Mhiche
alizungumzia umuhimu wa kutenga muda wa maombi na sala na kutoa rai kwa waamini
kuacha kumdhihaki Mungu pale tu wanapokuwa kwenye nyumba za Ibada pekee, ambapo
alisema kuwa wakishatoka huko huendelea kutenda dhambi.
Makamu Mkuu wa Kanisa la TAG,Askofu Magnus Mhiche akiomba kabla ya uzinduzi wa Hema la kuabudia la Kanisa la International Christian Centre(ICC)lililopo Soweto Mjini Moshi,kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira.
“Mungu alipotuumba alitaka tuwe na
ushirika na yeye, Ibada ni mfumo wa ushirika, tunapokutana kwenye makanisa yetu
huo ni ushirika wako wewe na mimi,” alisema.
Alisema licha ya kuwa watu wote
hujua umuhimu wa maombi, wengi wao wanaugumu wa kutenga muda kwa ajili ya
maombi wakati wakiwa makazini,safarini na majumbani mwao.
Askofu Mhiche aliwakumbusha
wakristo kuwa ukweli wa moyo wa binadamu daima huwa katika maombi na
kuwataka wabadilike kwa kutenga muda wa kutafakari juu ya mema
anayowatedea mwenyezi mungu.
Akawageukia maaskofu na kuwataka
waendelee kuwasaidia washirika kutambua majira na nyakati za ulimwengu wa sasa
katika kipindi hiki ambacho watanzania wengi wanaendelea kulalamika ya
kuwa hali ya uchumi ni ngumu.
“Mimi wakati wa utawala wa Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere nilikuwa nasoma kidato cha nne,nimeshuhudia pia
utawala wa Marais Mwinyi, Mkapa na Kikwete, wote hawa sikuwahi kumuona hata
mmoja wao akiwagawia Watanzania fedha”, alisema.
Alisema wanaoendelea kulialia kuwa
hali ni mbaya ama vyuma vimekaza hao ni wale ambao walikuwa wamezoea kuwanyonya
baadhi ya watanzania ambao ni watu wa hali ya chini.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo
la Kilimanjaro Magharibi la Kanisa hilo, Dkt Benjamin Bukuku, alisema kuwa
makanisa ya TAG yanakabiliwa na upungufu wa wachungaji hivyo kuomba wachungaji
kupelekwa ili kwenda kutoa huduma ya kiroho.
“Bado Kanisa linawajibu mkubwa wa
kuendelea kupata makazi ya Kanisa ya kuabudia, kujengwa kwa hema hili
kutawezesha waumini kuweza kupata huduma ya kiroho mahali hapa,” alisema.
Naye mkuu wa mkoa wa
Kilimanjaro, Anna Mghwira amelipongeza kanisa la International Christian Centre
(ICC), lililoko chini ya TAG, kwa kuona umuhimu wa kujenga hema hilo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa
madhehebu ya dini yamekuwa msaada mkubwa kwa serikali katika kuwahudumia
watanzania na kuachana na mambo maovu.
Aidha mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa
serikali inathamini mchango wa taasisi za dini katika kudumisha amani, utulivu
na mshikamano hapa nchini.
Mghwira alisema ya kuwa serikali
inatambua huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi za dini ikiwemo Elimu,
Afya, miradi ya maji na miradi mingine ya kimaendeleo.
Alisema serikali itaendelea kutoa
michango ya hali na mali pale inapowezekana ili kuhakikisha raia wake wanapata
maendeleo na wanaishi kwa furaha na utulivu.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa
hema hilo Mchungaji kiongozi wa Kanisa la International Christian Centre (ICC)
Askofu Mstaafu wa TAG Glorius Shoo alisema hema hilo limegharimu kiasi
cha shilingi milioni 100 hadi kukamilika kwa ujenzi huo.
Pia mchungaji Shoo alimpongeza
Rais Dkt John Magufuli kwa kuwapatia eneo hilo ili waweze kujenga jengo ambalo
litatumika kutolea huduma za kiroho na za kimwili mahali hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira akisalimiana na Viongozi wa Kanisa la TAG muda mfupi kabla ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa Hema la kuabudia la kanisa International Christian Centre(ICC) eneo la Soweto mjini Moshi ambalo lipo chini ya TAG.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni