JESHI la polisi mkoani
Tanga limefanikiwa kuwatia mbaroni watu wanne akiwamo mwanamke mmoja mkazi wa
Kigogo Jijini Dar es salaam wakituhumiwa kuhusika ma mauaji ya mlinzi wa shamba
la Mkonge la Kwa Mduru lililopo wilaya ya Korogwe .
Katika tukio hilo,mlinzi wa shamba
hilo,Omar Athuman aliuawa kwa kupigwa risasi huku meneja mkuu wa Shamba hilo
ambaye ni raia wa Kigeni,Mathias Hendrik akijeruhiwa vibaya sehemu mbali mbali
za mwili wake.
Kamanda wa polisi mkoa wa
Tanga,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi(SACP),Edward Bukombe,amezungumza
na Ndagullablog na kueleza kuwa katika
tukio hilo,majambazi hao mbali na kuua,kujeruhi,pia walipora vitu mbali mbali
zikiwamo,pesa,simu .
Waliokamatwa kuhusiana na tukio
hjilo ni Ebeni Venance Mwaipopo(27)mkazi wa Ngarenairobi mkoani Arusha,Fredrick
Menadi(46) mkazi wa Chekereni ya Bonite mjini Moshi,Diana Godliving(24)na
Dismas Venance Mwaipopo,wote wakazi wa Dar es salaam.
“Katika tukio hilo,watuhumiwa hao
walitumia silaha ya moto kufanikisha uporaji huo ambako walimuua mlinzi wa
shamba hilo,wakamjeruhi mwenzake lakini meneja mkuu wa shamba hilo naye alijeruhiwa
vibaya”,amesema kamanda Bukombe.
Habari kutoka wilayani Korogwe
zinadai kuwa,kutokana na meneja huyo kupata majereha makubwa sehemu mbali mbali
za mwili ,kwa sasa yuko nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi.
Akizungumza na Ndagullablog ofisini kwake hivi karibuni,kamanda Bukombe alisema
uchunguzi wa polisi umebaini kuwa silaha iliyotumika katika tukio hilo la
mauaji ya mlinzi huyo iliibwa mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa kamanda
Bukombe,Bastola hiyo aina ya Norinco Star,ni mali ya mfanyabiashara Denis Swai
mkazi wa Soweto katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ndagullablog imezungumza na Swai
ambaye amekiri kuwa Bastola hiyo ni mali yake na kwamba tayari ameshaitwa na
ofisi ni Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai(RCO) mkoa wa Tanga kwa ajili ya
utambuzi.
“Kama ulivyopata taarifa kwa RPC wa
Tanga ni kweli hiyo bastola ni mali yangu na hivi karibuni niliitwa na RCO
kwenda kuitambua na nimejiridhisha kuwa ni mali yangu japo imefutwa
namba”,amesema Swai.
Mfanyabiashara huyo amesema
kuwa,bastola hiyo iliibwa na watu wanaaminika kuwa ni majambazi baada ya
kuvamia nyumbani kwake eneo la Soweto mwezi julai mwaka jana ambako licha ya
kuiba bastola hiyo waliiba na vitu vingine.
Kwa mujibu wa Swai,majambazi hao
wakiwa na silaha za moto waliiba pia seti moja ya TV aina ya Sony yenye ukubwa
wa inchi 40 ikiwa na thamani ya shilingi milioni 1.2,pete ya ndoa ya mke wake
na pesa taslimu zaidi ya paundi 20,000 za Uingereza.
Hata hivyo mfanyabiashara huyo
amsema kuwa wakati tukio hilo linatokea yeye hakuwepo nyumbani kutokana na kuwa
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) ambako alikuwa akipokea wageni
wake kutoka nchini Marekani.
“Kama ningekuwa nyumbani siku hiyo
basi lolote ningeweza kutokea nap engine leo nisingekuwa hai maana kwa jinsi
walivyoingia nyumbani ni hakika walikuwa wamejipanga kwa lolote”.amesema.
Wakati bastola yake ikipatikana
baada ya kuhusika katika tukio la mauaji huko Korogwe mkoani Tanga,seti yake ya
TV ilipatikana kwa mmoja wa watuhumiwa hao wa mauaji ,Fredrick Menadi eneo la
Chekereni ya Bonite mjini Moshi.
WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MAUAJI YA
MLINZI
Wakati huo huo,watuhumiwa hao
wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mfawidhi wa wilaya ya Korogwe mkoani
Tanga wakikabiliwa na shitaka moja la mauaji ya mlinzi wa shamba hilo la Mkonge
la Kwa Mduru.
Waliofikishwa mahakamani mbele ya
hakimu mfawidhi Kassim Kwawa ni,Ebeni Venance Mwaipopo(27)fundi na mkazi wa
Ngarenairobi mkoani Arusha na Fredrick Menadi (46) boda boda mkazi wa Chekereni
ya Bonite mjini Moshi.
Wengine ni Diana Godliving binti wa
miaka 24 na mkazi wa Kigogo Jijini Dar es salaam pamoja na Dismas Venance
Mwaipopo pia mkazi wa Dar es salaam anayetajwa kuwa ni baba mzazi wa mshitakiwa
wa kwanza.
Washitakiwa hao walisomewa
shitaka moja la mauaji na mwendesha mashitaka mkaguzi wa polisi,Richard
Rweyemamu ambako wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 23 mwaka jana saa 3.20
usiku.
Hata hivyo washitakiwa hao baada ya
kusomewa shitaka hilo hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo ya
wilaya kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji na kurejeshwa rumande katika gereza la wilaya la Korogwe
lililopo Korogwe mjini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni