Jumamosi, 26 Mei 2018

MUWSA SASA KUWAUNGANISHIA MAJI WANANCHI WA URU KWA MKOPO


 Na FINA LYIMO,MWANANCHI,MOSHI.

Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira   Mjini Moshi  (MUWSA) imeanzisha mpango maalumu wa kuwaunganishia wananchi huduma ya maji safi na salama  kwa njia ya mkopo ikiwa ni mkakati wa mamlaka hiyo kuwafikia wananchi wengi.

Ofisa habari wa mamlaka hiyo, Rashid  Nachan amesema mpango huo  utawanufaisha   zaidi ya wananchi 34,000  kutoka  kata za Uru Kaskazini na Uru Kusini zilizopo  wilaya ya Moshi  Vijijini  kutokana  na wananchi wa maeneo hayo  kukosa huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.

Alisema  tayari mamlaka hiyo  imetumia zaidi ya shilingi  Bilioni mbili  kwa ajili ya  kuchukua maji kutoka  kwenye chanzo cha maji cha Mang'ana kilichopo ndani ya hifadhi ya Taifa ya mlima Kilimanjaro.

“Mamlaka imeamua kutoa huduma kwa njia ya mkopo ili wananchi wote  waweze kupata maji kutokana na wananchi kushindwa kulipa  fedha za kuunganishiwa huduma ya maji kwa mkupuo”alisema.

 Kwa mujibu wa ofisa habari huyo wa MUWSA,mpango huo utavinufaisha vijiji  11 vilivyopo katika kata hizo mbili na kwamba tangu mradi  huo uzinduliwe mwaka jana tayari  kaya 1000  zimeweza  kulipa huduma ya maji kwa mkupuo na kupata maji safi na salama.
 
 Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya maji safi na Uondoshaji wa taka Moshi mjini(MUWSA),Joyce Msiru

Naye diwani wa kata ya Uru kusini Wilhad Kitali, alisema wananchi ndio waliomba mradi huo wa maji na mamlaka kuona umuhimu na kuwaletea  lakini wanashindwa kulipa garama kwa mkupuo kutokana na hali duni ya maisha  ya wananchi hao.

Kitali alisema mpango huo wa kuunganishiwa huduma ya maji kwa  njia  ya mkopo itawarahisishia wananchi kilipa kidogo kidogo na hatimae kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 2 kwenda kuchota maji katika mto Rau.

Alisema awali wananchi walikuwa na dhana potofu ya kuwa maji ni ya bure na kwamba  hayalipiwi  lakini kwa sasa wamepatiwa elimu na wamekubali kufungiwa maji hayo kwa njia ya mkopo kwa kuingia mkataba MUWSA.

Mmoja Wa wananchi kata ya Uru Kusini Rogath Simba alisema hatua yakuunanishiwa  maji kwa njia ya mkopo  imekuwa chachu kwa  wananchi wengi kuhamasika na tayari wameshaanza kulipa ili waweze kupatiwa huduma hiyo muhimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni