Alhamisi, 4 Januari 2018

BREAKING NEWS: HATIMAYE MTUMISHI WA P P F APANDA KIZIMBANI KWA DAWA ZA KULEVYA,APELEKWA MAGEREZA



Na Charles Ndagulla,Moshi.

HAYAWI HAYAWI YAMEKUWA,baada ya kusota mahabusu kwa siku 17,hatimaye mtumishi wa mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa (PPF),Anitha Osward Ichwekeleza(32),anayetuhumiwa kujihusisha na usafrishaji wa dawa za kulevya,amefikishwa mahakamani mjini moshi.

Mtumishi huyo wa umma,alikamatwa desemba 19 mwaka jana akiwa na shehena ya madawa ya kulevya aina ya mirungi aliyokuwa akiisafrisha kwa kutumia gari lake dogo aina ya Toyota Sienta lenye namba za usjaili T674DLB.

Anitha alifikishwa katika makahama ya hakimu mkazi mjini Moshi chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto akitokea kituo cha polisi Majengo mjini hapa ambako kwa muda wote tangu akamatwe alikuwa akishikiliwa huko.

Baada ya kufikishwa hapo alishikiliwa kwa muda nje ya mahakama kabla ya kupandishwa kizimbani na kusomewa shitaka moja la uhujumu uchumi mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi,Aidan Mwilapwa.

Alisomewa shitaka hilo na wakili wa serikali Agatha Pima na kutokana na shitaka hilo kuwa ni la uhujumu uchumi na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya aina hiyo hadi mahakama kuu,mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote.

Mshitakiwa huyo ambaye kwenye hati ya mashitaka ametambulishwa kama mtumishi wa umma,ameshitakiwa kwa kosa moja la kusafrisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 15(b) cha sheria namba 5 ya mwaka 2015  ya udhibiti wa usafrishaji wa dawa za kulevya kama ilivyofanyiwa marejeo madogo na sheria namba 23 ya mwaka 2016.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka,mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa,mnamo desemba 19 mwaka jana huku Majengo kwa Mtei Manispaa ya Moshi,mshitakiwa alikutwa akisafrisha kilo 216.37 za dawa za kulevya.

  Baada ya kusomewa shitaka hilo,mshitakiwa huyo alipelekwa mahabusu katika Gereza Kuu la Mkoa,la Karanga ambako sasa ameenda kuanza maisha mapya ya gerezani,shauri hilo litakuja kwa ajili ya kutajwa tena mahakamani hapo Januari 19 mwaka huu.


HIVI NDIVYO ALIVYONASWA NA SHEHENA YA DAWA ZA KULEVYA

 Anitha alikamatwa na askari wa jeshi la polisi waliokuwa doria baada ya kupenyezewa taarifa na raia wema kuwa mtumishi huyo wa umma alikuwa amebeba ‘mzigo’ akitumia gari lake binafsi ambalo kulingana na sheria,kama atapatikana na hatia,gari hilo litataifishwa na serikali .

“Askari wakiwa doria walimkamata Anitha Oswald, ambaye ni mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370”, alisema kamanda Issa. 

Kamanda Issa alisema Anitha Oswald alikamatwa eneo la Majengo kwa Mtei Disemba 19, mwaka jana, akiwa anatokea Njia Panda ya Himo kuchukua mzigo huo. 

Aidha kamanda Issa alisema kwamba usafirishaji wa dawa za kulevya bado ni changamoto kubwa ambapo alielezea kusikitishwa na tabia ya baadhi ya watumishi wa Umma kujihusisha na usafirishaji huo.

“Jeshi la polisi mkoani hapa liko makini, operesheni inaendelea na hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kujihusisha na biashara hii”, alisema.
Hata hivyo kamanda aliongeza kusema kwamba jeshi hilo la polisi mkoani kilimanjaro, bado linaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo, ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza gari alilokuwa akiliendesha baada ya kugonga mti katika jitihada za kuwakimbia polisi. 

 PICHA MBALI MBALI ZIKIMUONYESHA ANITHA OSWARD ALIVYONASWA NA DAWA ZA KULEVYA
 Mtuhumiwa wa dawa za kulevya,Anitha Osward(32)akiwa chini ya ulinzi wa polisi huku akiwa amesimama mbele ya gari lake aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674DLB huku shehena ya dawa za kulevya ikiwa ndani ya gari lake.
 Shehena ya dawa za kulevya iliyokamatwa na polisi mjini moshi ikisafrishwa na mtumishi wa mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma(PPF),Anitha Osward,tayari mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani .
 Gari la mtuhumiwa wa dawa za kulevya Anitha Osward aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB likivutwa baada ya kugonga mti katika jitihada za mtuhumiwa huyo kuwakimbia polisi.
 gari aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB linalomilikiwa na mtumishi wa mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma(PPF)Anitha Osward likiwa limesheheni shehena ya dawa za kulevya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni