Na Charles Ndagulla,Moshi
MAHAKAMA ya hakimu mkazi mjini
Moshi,imewahukumu kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela walimu wawili wa
shule ya Msingi ya Mwereni iliyopo wilaya ya Hai baada ya kukutwa na hatia ya
kuhamisha umiliki wa shamba la shule isivyo halali.
Hukumu hiyo imetolewa januari 3
mwaka huu na kaimu hakimu mfawidhi wa
mahakama hiyo,Aidan Mwilapwa baada ya
kuwatia hatiani washitakiwa hao .
Walimu waliotiwa hatiani na
kuhukumiwa kifungo hicho ni Mwalimu mkuu wa shule hiyo,Onesmo Ernest Kinyaiya
na mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo,Apolinary Denke Pantaleo.
Shamba hilo lilitolewa na walimu hao kwa mtoto wa Marehemu Philemon Ndesamburo aitwaye Tomm ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Rahisi General Marchant Ltd ambayo ni kampuni tanzu ya makampuni ya Rahisi Group ya mjini Moshi.
Walimu hao walifikishwa mahakamani
hapo na kusomewa mashitaka na waendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa(Takukuru),Barry Galinoma akisaidiana na Furahini Kibanga.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka
iliyosomwa makahamani hapo na waendesha mashitaka hao wa Takukuru,wlimu hao
walishitakiwa kwa kosa la kuhamisha umiliki wa shamba la shule hiyo kwenda kwa
kampuni ya Rahisi General Marchant Ltd bila idhini ya kamishna wa Ardhi.
Kulingana na hati hiyo ya
mashitaka,walimu hao hawakuwa na mamlaka hayo kwa mujibu wa kifungu cha 17(5)
cha sheria ya ardhi ya vijijini sura ya 14 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka
2002.
Hivyo uhamishaji huo ulikuwa kinyume na kifungu cha
31 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 hivyo
mahakama hiyo kuwatia hatiani katika shauri hilo la jinai namba 3 la mwaka
2016.
Katika hukumu hiyo,walimu hao
walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au faini ya shilingi laki tano na
baada ya mahakama kuwatia hatiani walimu hao walinusurika kwenda jela baada ya
ndugu walikuwa wamefurika mahakanai hapo kuchangishana fedha na kuwalipia faini.
Baada ya hukumu hiyo,Taasisi ya
kuzuia na kupambana na rushwa(Takukuru) mkoani Kilimanjaro,imetoa taarifa
kupitia kwa Mkuu wa Taasisi hiyo mkoani hapa,Holle Makungu kuwa itafuatilia kwa
mwajiri wa walimu hao ili kuhakikisha wanaondolewa kwenye utumishi wa umma.
KARANI MAHAKAMA YA MWANZO MBARONI KWA RUSHWA YA LAKI MOJA.
Katika tukio jingine,mtego
ulioandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru),umefanikiwa
kumnasa karani mmoja wa mahakama ya Mwanzo iliyopo Maili Sita wilaya ya Hai .
Karani huyo,Rose Jonathan
Urassa(58),alinaswa na Takukuru baada ya kudai rushwa ya shilingi laki moja ili
amsaidie mshitakiwa katika shauri la jinai namba 69/2017 kupitia kwa hakimu
anayesikiliza shauri hilo.
Taarifa ya Takukuru mkoani Kilimanjaro
iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Januari 4 na kusainiwa na Mkuu wa Takukuru
mkoa(RBC),Holle Makungu imeeleza kuwa,karani huyo aliomba fedha hizo ili hakimu
anayesikiliza shauri hilo aweze kutoa hukumu ya upendeleo kwa mshitakiwa.
“Baada ya taarifa hizo
kupokelewa,mtego wa rushwa uliandaliwa na aliweza kukamatwa januari 3 mwaka huu
akiwa amepokea fedha hizo katika eneo hilo la mahakama ya mwanzo,Hai,Rose atafikishwa
mahakamani mara uchunguzi utakapokamilika”,imesema taarifa hiyo.
Takukuru imetoa onyo kwa baadhi ya makarani na wahudumu wa
mahakama wanaoendekeza tabia ya kuomba na kupokea rushwa kwa kisingizio cha kutumwa
na waheshimiwa mahakimu wabadili tabia hiyo.
Kamanda Makungu katika taarifa yake
hiyo kwa vyombo vya habari,ametoa rai kwa makarani na wahudumu wa mahakama
katika mkoa wa Kilimanjaro wanaoendelea na tabia hiyo mwisho wao wa kufanyakazi katika utumishi wa umma kwa mwaka
huu 2018 utakuwa mwisho wao.
Pia alitoa wito kwa wananchi
wanaodaiwa rushwa na baadhi ya makarani na wahudumu wa mahakama kwa kisingizio
cha kutumwa na waheshimiwa
mahakimu,watoe taarifa kwa taasisi hiyo ili iweze kuboresha mahakama kwa
kuwaondoa wachache wanochafua sura za mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni