Jumatatu, 8 Januari 2018

UHABA WA MIUNDOMBINU YA MAJITAKA UNAVYOCHANGIA MAGONJWA YA MLIPUKO KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM



Licha ya idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mitandao ya majitaka katika miji mikuu kuongezeka, ni asilimia 20 tu ya wananchi katika miji hiyo wanafikiwa na huduma hiyo nchini na kuwaweka katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

Miji mikuu 10 ambayo imeunganishwa kwenye mitandao wa majitaka ni Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Tabora, Moshi, Tanga, Songea na Iringa ambapo serikali imeendelea kufanya maboresho ya miundombinu ili kuhakikisha wateja wengi zaidi wanaunganishwa kwenye huduma hiyo.

Kulingana na hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa wakati huo Eng. Gerson Lwenge aliyoitoa kwenye bunge la bajeti ya mwaka 2017/2018 alisema “Idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mitandao ya majitaka katika miji hiyo imeongezeka kutoka 25,361 mwezi Machi, 2016 hadi kufikia wateja 26,636 mwezi Machi, 2017 na kuweza kupunguza kero ya majitaka kutiririka hovyo katika miji hiyo”. 

Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mtandao wa majitaka imeongezeka kutoka 18,436 mwezi Machi, 2016 hadi kufikia wateja 19,034 mwezi Machi, 2017. 

Kwa muktadha huo huduma ya uondoaji majitaka katika miji hiyo ikijumuisha Jiji la Dar es Salaam imefikia asilimia 20.

Matarajio ya wizara ya Maji na Umwagiliaji ni kuongeza huduma ya uondoaji majitaka kutoka asilimia 20 ya sasa hadi kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020. 
  Mabomba yakimwaga majitaka kwenye mto

Licha ya juhudi hizo za serikali, changamoto inabaki kwa jiji la Dar es Salaam ambalo idadi ya wakazi wake inaongezeka kwa kasi na kwamba lina uhitaji mkubwa wa huduma hiyo ili kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama dhidi ya majitaka yanayotiririka katika mitaa mbalimbali.

Kulingana na  Mamlaka ya Maji Dar es Salaam (DAWASCO) inaeleza kuwa mfumo wa majitaka katika jiji la Dar es Salaam ni mkusanyiko wa mifereji  ambayo hukusanya maji kutoka katika maeneo mbalimbali kwa kutumia  pampu zilizofungwa katika vituo 15 ambazo huyaelekeza maji hayo katika mabwawa.

Eneo linalopata huduma hiyo ni kilomita 170 ambalo limetandazwa mabomba yenye kipenyo cha milimita 100 hadi 100 ambapo maeneo ya katikati ya jiji, Kariakoo, Upanga na Muhimbili humwaga maji yake moja kwa moja katika bahari ya Hindi.

Eneo linalopata huduma hiyo ni dogo ikilinganishwa na ukubwa wa jiji hilo ambalo unafikia kilomita za mraba 1,393. 

Ni dhahiri kuwa eneo kubwa lililobaki limezungukwa na majitaka ambayo huchanganyika na maji ya visima yanayotumiwa na wananchi wengi wa jiji hilo na kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.  

Moja ya njia kubwa ambayo inaweza kueneza magonjwa kama kipindupindu ni matumizi ya maji machafu. Maji machafu yanaweza kuwa ya visima au bomba ikiwa hayawekwi dawa kuua vijidudu au kuchemshwa kabla ya kutumika.

Dar es Salaam inatajwa kuongoza kukumbwa na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu kuliko maeneo mengine nchini. 

Hali hiyo inatokana na jiji hilo kuwa na idadi kubwa ya visima vyenye vimelea ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa ya milipuko hasa kipindupindu na homa za matumbo.

Kipindupindu ni ugonjwa unaoambukizwa kupitia maji au chakula chenye vimelea ambavyo kitaalamu hujulikana kwa jina la ‘Vibrio Cholerae.’  Vimelea hivi huishi katika maji yaliyochafuliwa hasa yenye kinyesi.

Maeneo ambayo huathirika zaidi na majitaka ni Buguruni, Kigogo, Tandale, Kariakoo, Manzese na Yombo ambayo hutegemea zaidi maji ya visima virefu kama mbadala wa huduma za Dawasco, lakini visima hivyo havina maji salama.

Hili linathibitishwa na kauli ya Waziri wa Maji na Umwagilia wa wakati huo,  Mhandisi Gerson Lwenge wakati wa bunge la bajeti 2016/2017 alipoelezea kuhusu uchunguzi wa visima 108 ambapo visima 66 vilikuwa sio salama na maji yake yalikuwa na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu. Visima virefu vilikuwa 40 na vifupi ni 26.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Ardhi, unaonesha maji ya visima vingi sio salama na kushauri wachimba visima kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepusha jamii na magonjwa kwa kutumia maji yasiyokuwa salama.

Kufikia Septemba 2016, Dar Es Salaam ilikuwa na visima virefu 676 huku Wilaya za Temeke na Ilala zikiongoza kutokana na kutofikiwa na maji ya DAWASCO. Kinondoni, kwa kuwa na mtandao mkubwa wa maji ya Dawasco, hali ya kipindupindu sio mbaya.

Ni dhahiri kuwa mamlaka husika zinapaswa kutazama upya mfumo wa majitaka na kuboresha miundombinu iliyopo ili kuwafikia watu wengi zaidi katika nyumba zao. 

Pia elimu iendelee kutolewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutumia mfumo rasmi wa kutibu majitaka ili kujiepusha na athari za kiafya.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni