Alhamisi, 4 Januari 2018

URAIA WA MCHUNGAJI WA KANISA LA YESU ANAWEZA MOSHI UTATA


Na Charles Ndagulla,Moshi.

MCHUNGAJI Zakaria Donald Yona wa Kanisa la Yesu Anaweza Centre ameingia matatani akituhumiwa kuishi nchini isvvyo halali  baada ya kudaiwa kuwa ni raia wa Kenya.

Uchunguzi wa mtandao huu  umebaini kuwa,mchungaji huyo ni raia wa Kenya kwa kuzaliwa lakini mwenyewe amekana tuhuma hizo na kudai  ni mtanzania kwa kuzaliwa.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo mtandao wa NdagullaBlog umeziona zinaonyesha kuwa,mchungaji huyo anayeendesha kanisa lake eneo la Mji Mpya Manispaa ya Moshi,alizaliwa mwaka 1964  eneo la Siaya mkoa wa Nyanza nchini Kenya.

Kulingana na nyaraka hizo,baada ya kuzaliwa alipewa cheti chenye namba ya ingizo 4300247/85  akitambuliwa kwa majina ya Donald Oloo Waswani huku pia akiwa na kadi ya utaifa wa Kenya yenye namba 237104963 iliyotolewa Oktoba 10 mwaka 2013.

Pia mke wa mchungaji huyo anayetumia majina ya Redempter William Francis kwa hapa nchini,uchunguzi umebaini kuwa alizaliwa mwaka 1970 huko Machakos nchini Kenya huku akiwa na kadi ya uraia wa nchi hiyo yenye namba 223854431 iliyotolewa mwaka 2007.

Uchunguzi zaidi  umebaini kuwa,mchungaji huyo amesajiliwa kama mlipa kodi na mamlaka ya mapato nchini Kenya(KRA) na kupewa namba ya utamburisho wa mlipa kodi(Personal Identification Number) Na A.010329470.

Mchungaji huyo na mkewe Redempter William Francis,wanadaiwa kufunga ndoa yao Oktoba 13 mwaka 1991 katika Kanisa la Dandora Gaspel Tabernacle na kupewa cheti chenye namba 465369.

Hata hivyo mchungaji huyo amezungumza na NdagullaBlog  na kutupilia mbali tuhuma hizo lakini akishindwa kuweka wazi ni wapi  alipozaliwa akidai wakati ukifika ataweka wazi kila kitu.

“Suala la mimi nimezaliwa wapi tutakuja kuliweka sawa lakini kwa ufupi mimi ni mtanzania kwa kuzaliwa na hayo mengine yote yatajulikana huko mbele ya safari”,alisema .

Wakati mchungaji huyo akikwepa kuweka wazi alikozaliwa,NdagullaBlog imefanikiwa kuona nyaraka mbalimbali baadhi zikidaiwa ni za kughushi zikionyesha mchuangaji huyo alizaliwa Nyamagana mkoani mwanza mwaka 1964.

Kwa mujibu wa cheti cha kuzaliwa kilichosajiliwa Machi 15 mwaka 2010,kinaonyesha mchungaji huyo alizawali eneo hilo na kusajiliwa kwa jina la Zacharia Donald Yona Munuo.

Pia mkewe ambaye kwenye cheti cha kuzaliwa nchini Kenya anatumia majina ya Redempter Ndinda Nthenge,kwenye cheti cha kuzaliwa hapa nchini anatambulika kwa majina ya Dedempter William Francis Munuo akidai alizaliwa Nyamagana mkoani Mwanza mwaka 1969.

Wawili hao pia wanadaiwa kufunga ndoa ya kiserikali mkoani Kilimanjaro Juni 13 mwaka 2007 na kupewa cheti  B/N na.0748488 hali ambayo inazidisha utata zaidi juu ya uraia wa wawili hao.

Mchungaji huyo amekiri kuwahi kukamatwa yeye na familia yake yote na maofisa wa jeshi la uhamiaji mkoani Kilimanjaro na kufikishwa makahamani akidaiwa kuishi nchini isivyo halali.

“Tulikamatwa juni 20 mwaka jana na wakatushikilia kwa siku mbili na baadaye wakatupeleka mahakamani,madai yao ni kwamba mimi na familia yangu si raia wa Tanzania bali ni raia wa Kenya”,amedai.

Amedai kuwa,uhamiaji walidai kuwa wangepeleka mashahidi 15 na vielelezo zaidi ya 20 kudhibitisha kuwa mchungaji huyo si raia wa Tanzania lakini hawakufanya hivyo.

Hata hivyo mchungaji huyo amesema kuwa,uhamiaji waliondoa shauri hilo mahakamani  desemba 6 mwaka jana baada ya kudai upande wa jamhuri hauna nia tena ya kuendelea kuwashitaki.

Mchungaji huyo amedai kuwa,wakati wakiamini suala hilo limeisha na wako huru kuendelea na maisha yao,walijikuta wakikamatwa tena nje ya mahakama na kupelekwa ofisi za uhamiaji .

Kwa mujibu wa mchungaji huyo,baada ya kufikishwa katika ofisi hizo walilazimishwa kusaini nyaraka za kuondolewa nchini na walipokataa kusaini nyaraka hizo waliondolewa nchini kwa nguvu na kupelekwa mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Holili.

“Tulipofika holili maofisa wa uhamiaji wa Kenya walikataa kutupokea baada ya uhamiaji Tanzania kukosa nyaraka mhimu kuonyesha sisi hatutakiwi Tanzania zikiwamo nyaraka za mahakama”,amesema.

Mchungaji huyo amesema kuwa  baada ya zoezi hilo kugonga mwamba,maofisa hao wa uhamiaji waliamua kuwatelekeza mpakani na kuondoka kabla ya mchungaji huyo na familia yake kuamua kurejea  nyumbani kwa kutumia usafiri mbadala.

Msemaji wa uhamiaji mkoani Kilimanjaro(DCI),Albert Rwelamila amedhibitisha kuwepo na uchunguzi unaofanywa na ofisi yake juu ya uhalali wa uraia wa mchungaji huyo na familia yake alipozungumza na NdagullaBlog hivi karibuni.

Hata hivyo,Rwelamila hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo kwa undani zaidi kwa kile alichodai lipo zuio la mahakama kuu linalowataka kusitisha mchakato huo hadi hapo suala hilo litakapotolewa uamuzi.

“Ni mhimu tukaheshimu zuio la mahakama maana ni chombo cha kisheria nadhani baada ya kusikiliza pande zote na kutoa uamuzi hapo tunaweza kuwa na cha kusema,kwa sasa tuliache kwanza”,alisema.

NdagullaBlog imeambiwa kuwa,zuio hilo limewekwa baada ya mchungaji huyo kukimbilia mahakama kuu desemba 15 mwaka jana kupitia kwa wakili wake Caessar  Shayo.

Kwa upande wake wakili Shayo amesema kuwa  hati ya zuio ilitolewa desemba 18 mwaka jana na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi,Aishiel Sumari.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni