Jumatano, 21 Machi 2018

WATOTO WENYE ULEMAVU WA AKILI KAHE HOME WAKABILIWA NA CHANGAMOTO LUKUKI

NA SAFINA SARWATT,MOSHI

KITUO cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili (usonji) cha Kahe Home  kilichopo kata ya Kahe wilayani Moshi vijijini,kinakabiliwa na ukosefu walimu  wenye mahitaji maalumu, majengo ya madarasa pamoja vyumba vya kulala.

Mkurugenzi wa kituo hicho Martha Masenge ametoa kilio hicho hivi karibuni wakati akipokea msaada wa vyakula mbalimbali kutoka kwa kikundi cha akina mama cha TUWAMI kutoka kata ya Bonite wilaya ya  Moshi.

Mbali na hayo,Masenge alisema kuwa kituo hicho  pia kinakabiliwa na uhaba wa chakula pamoja na ukosefu wa majengo ya madarasa na walimu hali inayochangia watoto hao kushindwa kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu kama watoto wengine.     
 Hawa ni watoto wenye usonjo wanaolelewa katika kituo cha watoto cha Kahe Home kilichopo kata ya Kahe wilaya ya Moshi Vijijini.

"Mahitaji ya watoto hawa ni makubwa sana  na kituo  chetu hakina walimu  wa kuwafundisha watoto hao ,madarasa yaliyopo hayatoshi kwa mahitaji ya watoto ,pia chakula kwani kwa mwezi gharama za chakula ni zaidi ya million moja ," alisema.

"Hakuna walimu ambao wanataaluma ya ualimu ,waliopo ni wale ambao wana elimu ya malezi   na jinsi ya kuwahudumia na  hatuna walimu walioajiriwa na serikali," alisema Masenge.

Alisema kuwa kutokana na changamoto hizo wanalazimika kuwafundishia watoto hao katika mazingira magumu.

"Tunaiomba serikali itusaidie walimu wa shule za msingi kwani kituo hakina uwezo wa kuwaajiri ,kutokana na kutokuwa na  fedha ,na watoto wengine wanatoka katika mazingira magumu ," alisema.

Katibu wa chama cha akinamama (TUWAMI) kutoka kata  ya Bonite wilaya Moshi,Sofia Juma ,ameishauri serikali na wadau mbalimbali kuwasaidia watoto hao ili wapate haki zao za msingi kama watanzania wengine.
 Kina Mama kutoka kikundi cha  TUWAMI kutoka Kata ya Bonite wilaya ya Moshi wakila chakula pamoja na watoto wenye ulemavu wa akili(usonjo)wanaolelewa na Kituo cha watoto cha Kahe Home.

Alisema kuwa watoto wenye ulemavu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na kufanyiwa matukio ya ukatili ikiwamo matukio ya kubakwa na kulawitiwa.

"Naomba jamii ya watanzania kuwapenda na kuwasaidia ili wafikie malengo yao ya kuwa na maisha bora kama watanzania wengine,kama mnavyojua wengi wanatoka katika familia maskini ," alisema Juma.
 Mkurugenzi wa kituo cha kulea watoto wenye ulemavu wa akili(usonjo),Martha Masenge (kulia)akitoa neno la shukrani muda mfupi baada ya kupokea msaada wa vyakula,mafuta na vinywaji kutoka kikundi cha kina mama cha TUWAMI kutoka Bonite Moshi.

Jumamosi, 17 Machi 2018

WASIOLIPA ANKARA ZA MAJI MUWSA WAKIONA CHA MOTO,POLISI,MAGEREZA WAVUTIWA PUMZI


NA KIJA ELIAS, MOSHI. 

Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi (MUWSA), imewasitishia huduma ya maji safi na salama wakazi zaidi ya 1,503,  kutokana na kushindwa kulipa malimbikkizo ya ankara za maji wanayodaiwa na Mamlaka hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habati hivi karibuni,Mkurugenzi wa Mamalaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi Joyce Msiru alisema kuwa wateja hao wanadaiwa zaidi ya shilingi Milioni 143.7.

Alikuwa akizungumza kuelekea maadhimisho ya wiki ya maji ambayo huadhimishwa kila mwaka nchini kote kuanzia machi 16 hadi 22  ambako alitumia muda huo kuwaasa wateja wenye madeni kulipa ankara zao ili kukwepa adha ya kusitishiwa huduma hiyo mhimu .

Alisema katika kuadhimishi wiki ya maji mjini hapa Mamlaka hiyo inakusudia kufanya promosheni   mbali mbali kwa wateja wake watakaounganishiwa huduma ya maji safi na maji taka  wakiwemo waliositishiwa huduma ya maji kutokana na malimbikizo ya ankara za maji.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na uondoshaji wa maji taka Moshi Mjini(MUWSA),Joyce Msiru akipanda mti ikiwa ni uzinduzi wa wiki ya maji inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia machi 16 hadi 22.

“Tutakuwa na wiki ya maji, wateja wa maji safi ambao watalipa madeni yao katika wiki ya maji watasamehewa faini ya shilingi 20,000 za kurudishiwa huduma ya maji majumbani mwao na kwa wale watakaohitaji kuunganishiwa huduma ya maji taka watalazimika kulipia nusu ya gharama zinazohitaji na sehemu iliyobaki wataendelea kulipa kwa awamu,”alisema.

Akizungumzia wiki ya maji Mkurugenzi huyo alisema itakwenda pamoja na zoezi la usafi wa mazingira katika soko la Manyema mjini hapa,kuwa na maonyesho ya shughuli mbali mbali zinazofanywa na Muwsa ikiwemo utoaji wa elimu kwa watumiaji wa maji na kuendesha zoezi la upandaji wa miti zaidi ya 12,000 katika vyanzo mbali mbali vya maji mjini hapa.

Meneja biashara wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira John Ndetico, alisema Mamlaka hiyo inakusudia kuzikatia huduma ya kupata maji safi  taasisi za serikali ikiwemo Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani hapa (RPC)Jeshi la magereza  na shule ya mafunzo ya awali ya polisi (CCP) iliyopo mjini hapa.
 Mkuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba akipanda mti kuashiria uzinduzi wa wiki ya maji mjini Moshi

Alisema licha ya serikali kuahidi kuzilipitia taasisi hizo madeni hayo bado zinaendelea kulimbikiza madeni yao na kwamba Muwsa tayari imeshaziandikia baraua za kuziarifu kuzisitishia huduma ya kupata maji safi.

‘Taasisi hizo zilikuwa zinadaiwa malimbikizo ya zaidi ya shilingi 320 milioni lakini madeni hayo yameongezeka hadi kufikia Julai 2017 bilioni 1.8 na kwamba taasisi hizo hazionyeshi nia ya kulipa malimbikizo hayo licha ya serikali kuahidi kuzilipia madeni yao yanayoishia june 2017 ambapo kupitia hazina madai hayo yapo kwenye zoezi la uhakiki ili yaweze kulipwa”alisema Ndetiko.
 Mkuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba(wa pili kutoka kulia) akikatra utepe kuzindua mfumo wa malipo ya huduma za majisafi na majitaka kupitia NMB Mobile ikiwa ni sehemu  ya maadhimisho ya wiki ya maji.
 TUNATEKELEZA: pichani ni Florah Nguma,kaimu ofisa uhusiano MUWSA akipanda mti katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji ambayo uliofanyika mjini moshi

PIERRE NKURUNZINZA KUTAWALA MILELE BURUNDI,HUU NI ULEVI MWINGINE WA MADARAKA KWA WATAWALA WA AFRIKA


Chama tawala nchini Burundi CNDD/FDD kimemtangaza Rais Pierre Nkurunziza kama kiongozi mkuu wa kudumu au kiongozi wa milele ndani ya chama hicho.

 Hatua hii ni mwendelezo wa 'ulevi' wa madaraka kwa watawala wa bara la Afrika ambao pindi wanapoingia madarakani huanzisha harakati za kuendelea kutawala ikiwamo kubadilisha katiba za nchi zao ili kuwaruhusu kuendelea kutawala .
 
 Rais wa Burundi,Pierre Nkurunzinza

Uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao vya siku tatu vya mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika eneo la Buye alikozaliwa Bwana Nkurunziza Kaskazini mwa nchi hiyo.

Uamuzi huo pia unachukuliwa wakati Burundi inajiandaa kufanya marekebisho ya katiba ili kumruhusu Rais Nkurunziza kuendelelea kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.

Taaarifa fupi ya chama cha CNDD/FDD imesema vikao hivyo vilinuwia kuimarisha chama tawala na taasisi zake,alinusurika kupinduliwa mwaka 2015
Lakini pia chama hicho kimechukua uamuzi wa kumuongezea hadhi na kumpa cheo cha juu Rais Nkurunziza na hivyo kumtangaza kuwa ni kiongozi mkuu wa kudumu ndani ya chama.

Kwenye hafla na makundi ya utamaduni ya chama tawala, katibu mkuu wa CNDD/FDD Bwana Evariste Ndayishimiye aliutangazia umati azimio hilo alolitamka kuwa ni muhimu mno katika uhai wa chama tawala.

Tangazo hili la chama tawala CNDD/FDD kumfanya Rais Nkurunziza kama Kiongozi Mkuu wa Kudumu linajiri wakati Burundi inajiandaa kwa kura ya maoni kuhusu Marekebisho ya Katiba baadae mwezi Mei. 

 Kati ya mambo mengi katiba hiyo ikipitishwa itamuwezesha Rais Nkurunziza kuweza kuwania Urais mpaka mwaka wa 2034.

Nkurunziza ni mcheza soka mashuhuri pia nchini Burundi
Wadadisi wengi wa siasa za Burundi wanaamini kuwa hatua hii ya chama tawala inanuwia kumalizia mapema mjadala wa mtetezi wa kiti cha Urais kwa niaba ya Chama hicho na kuonyesha mustakabali wa uongozi kabla hata uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2020.

Lakini pia uamuzi huo unapeleka ujumbe kwa wafuasi wa CNDD/FDD na haswa viongozi wenye nia pengine ya kuwania nafasi hiyo na hivyo kujaribu kukiepusha chama tawala na mpasuko kama ilivyotokea mwaka wa 2015 katika mzozo kuhusu muhula wa sasa wa Rais Nkurunziza.

Isitoshe kwa Wachambuzi wa siasa bado wanaiona hatua hii ya Rais Nkurunziza kutangazwa Kiongozi wa maisha kuwa dalili tosha ya jinsi kiongozi huyo alivyokidhibiti chama cha CNDD/FDD. 
 Rais wa Burundi,Pierre Nkurunzinza(kulia)akisakata soka mjini Bujumbura hivi karibuni.
Chanzo:BBC Swahili

Ijumaa, 16 Machi 2018

MTUMISHI PPF ALIYENASWA NA DAWA ZA KULEVYA AENDELEA KUSOTA GEREZANI

  MTUMISHI  wa mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa umma(PPF)mkoani    Kilimanjaro   ,Anitha Osward(32)anayetuhumiwa kusafrisha shehena ya dawa za kulevya,ameendelea kusota gerezani katika gereza Kuu la Mkoa wa Kilimanjaro,Karanga baada ya gari la mahabusu kuharibika.

Anitha Mkazi wa Karanga Manispaa ya Moshi,alikamatwa desemba 19 mwaka jana akiwa na shehena ya madawa ya kulevya aina ya mirungi aliyokuwa akiisafrisha kwa kutumia gari lake dogo aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674DLB.

Alikamatwa na askari wa Doria eneo la Majengo kwa Mtei mjini Moshi akiwa  anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370”. 
Kutokana na kuharibika kwa karandinga la polisi,kesi hiyo sasa imepigwa kalenda hadi machi 27 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Moshi kutokana na upelelezi wa shauri lake kutokamilika.

Katika kesi hiyo,dereva taksi mkazi wa mjini moshi,Frank Sifael Moshi maarufu kwa jina la ‘Gaucho’ameunganishwa na Anitha na inadaiwa ndiye aliyekuwa akiendesha gari la Anitha wakati wa tukio hilo.
Hata hivyo dereva huyo alitimua mbio baada ya gari hilo kusimamishwa na polisi wa doria na kumwacha Anitha akiangukia mikononi mwa polisi jaoo naye arobaini yake ilitimia baada ya kunaswa na polisi.
 Anitha Osward,mtuhumiwa wa dawa za kulevya,akiwa mikononi mwa polisi muda mfupi baada ya kukamatwa akituhumiwa kusafrisha shehena ya dawa za kulevya aina ya Morungi.
 Hii ndiyo shehena ya dawa za kulevya aina ya mirungi ambayo ilikamatwa ndani ya Gari la Anitha Osward lenye namba za usajili T674DLB aina ya Toyota Sienta,tayari Anitha na dereva wake Frank Sifael Moshi a.k.a Gaucho,wameshafikishwa makahamani wakishitakiwa kwa kosa la kusafrisha dawa za kulevya.