Jumatano, 21 Machi 2018

WATOTO WENYE ULEMAVU WA AKILI KAHE HOME WAKABILIWA NA CHANGAMOTO LUKUKI

NA SAFINA SARWATT,MOSHI

KITUO cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili (usonji) cha Kahe Home  kilichopo kata ya Kahe wilayani Moshi vijijini,kinakabiliwa na ukosefu walimu  wenye mahitaji maalumu, majengo ya madarasa pamoja vyumba vya kulala.

Mkurugenzi wa kituo hicho Martha Masenge ametoa kilio hicho hivi karibuni wakati akipokea msaada wa vyakula mbalimbali kutoka kwa kikundi cha akina mama cha TUWAMI kutoka kata ya Bonite wilaya ya  Moshi.

Mbali na hayo,Masenge alisema kuwa kituo hicho  pia kinakabiliwa na uhaba wa chakula pamoja na ukosefu wa majengo ya madarasa na walimu hali inayochangia watoto hao kushindwa kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu kama watoto wengine.     
 Hawa ni watoto wenye usonjo wanaolelewa katika kituo cha watoto cha Kahe Home kilichopo kata ya Kahe wilaya ya Moshi Vijijini.

"Mahitaji ya watoto hawa ni makubwa sana  na kituo  chetu hakina walimu  wa kuwafundisha watoto hao ,madarasa yaliyopo hayatoshi kwa mahitaji ya watoto ,pia chakula kwani kwa mwezi gharama za chakula ni zaidi ya million moja ," alisema.

"Hakuna walimu ambao wanataaluma ya ualimu ,waliopo ni wale ambao wana elimu ya malezi   na jinsi ya kuwahudumia na  hatuna walimu walioajiriwa na serikali," alisema Masenge.

Alisema kuwa kutokana na changamoto hizo wanalazimika kuwafundishia watoto hao katika mazingira magumu.

"Tunaiomba serikali itusaidie walimu wa shule za msingi kwani kituo hakina uwezo wa kuwaajiri ,kutokana na kutokuwa na  fedha ,na watoto wengine wanatoka katika mazingira magumu ," alisema.

Katibu wa chama cha akinamama (TUWAMI) kutoka kata  ya Bonite wilaya Moshi,Sofia Juma ,ameishauri serikali na wadau mbalimbali kuwasaidia watoto hao ili wapate haki zao za msingi kama watanzania wengine.
 Kina Mama kutoka kikundi cha  TUWAMI kutoka Kata ya Bonite wilaya ya Moshi wakila chakula pamoja na watoto wenye ulemavu wa akili(usonjo)wanaolelewa na Kituo cha watoto cha Kahe Home.

Alisema kuwa watoto wenye ulemavu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na kufanyiwa matukio ya ukatili ikiwamo matukio ya kubakwa na kulawitiwa.

"Naomba jamii ya watanzania kuwapenda na kuwasaidia ili wafikie malengo yao ya kuwa na maisha bora kama watanzania wengine,kama mnavyojua wengi wanatoka katika familia maskini ," alisema Juma.
 Mkurugenzi wa kituo cha kulea watoto wenye ulemavu wa akili(usonjo),Martha Masenge (kulia)akitoa neno la shukrani muda mfupi baada ya kupokea msaada wa vyakula,mafuta na vinywaji kutoka kikundi cha kina mama cha TUWAMI kutoka Bonite Moshi.

Maoni 1 :

  1. Nina muomba mkuu wa mkoa Kilimanjaro mama Mghira afuatilie hili swala la hawa watoto wapate walimu kutokana na mahitaji yao ili nao wapate haki zao kielimu na pia mashirika mbali mbali na watu wenye uwezo wajitolee kuwasaidia hawa watoto hongereni sana wakinamama wa TUWAMI kutoka bonite kwa kuguswa kwenu na kwenda kuwatembea hawa watoto Mungu awabariki sana.

    JibuFuta