Jumatatu, 12 Machi 2018

MAJERUHI WA BODA BODA YAMKUTA KCMC,AOZA MAKALIO YAKE,MKURUGENZI,PRO WANENA


 NA CHARLES NDAGULLA,MOSHI

MAJERUHI  wa ajali ya pikipiki aliyelazwa kwa zaidi ya siku 70 hadi sasa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi,Christian Ngowi(27),amepatwa na mkasa mwingine katikati ya matibabu baada ya kuoza makalio.

Baba mzazi wa majeruhi huyo,Mchungaji Godwin Ngowi amezungumza na Ndagullablog na kudai kuwa tatizo hilo limetokana na mwanaye kulazwa kitandani kwa siku 40 bila kugeuzwa.

Kutokana na tatizo hilo,mchungaji Ngowi amedai kuwa hali hiyo imesababisha mwanaye kukatwa nyama zote za makalio  huku akidai tatizo hilo limechangiwa na uzembe wa madaktari wa hospital hiyo.

Christian alipata ajali ya pikipiki januari mosi mwaka huu huko Bomang’ombe wilaya ya Hai baada ya kugongwa na gari ambalo baada ya tukio hilo lilitoweka bila kujulikana namba zake za usajili.

Katika ajali hiyo,Christian alipata majeraha ya kichwa pamoja na miguu yake kuvunjika baada ya gari hilo kumkanyaga miguu yake na hivyo  kuvuja damu nyingi na hivyo kupoteza fahamu.

Kutokana na ajali hiyo,alikimbizwa katika Hospitali hiyo akiwa mahututi na kupatiwa huduma ya kwanza na baadaye kufungwa mawe kwa lengo la kuirejesha miguu yake katika hali ya kawaida.
 Christian Godwin Ngowi,akiwa amelazwa katika Hospital ya Rufaa ya KCMC baada ya kupata ajali ya pikipiki Januari Mosi huko Bomang'ombe wilaya ya Hai,kwa sasa majeruhi huyo amepatwa na mkasa mwingine baada ya kuoza makalio kutokana na kukaa kitandani muda mrefu bila kugeuzwa, puani ni mipira inayomsaidia kupitisha chakula.

 “Usalama wa maisha ya mtoto wangu yapo hatarini,pamoja na wao kcmc kumsababishia matatizo hayo gharama za matibabu zimeangukia kwangu”,amesema.

Amedai kuwa tatizo alilonalo mtoto wake halitokani na ugonjwa uliompeleka hospitalini hapo na kuongeza kuwa tayari miguu ya mwanaye  kwa mujibu wa madaktari wanaomtibu imeanza kuunga.

Mchungaji Ngowi amedai kuwa,mpaka sasa ametumia zaidi ya shilingi 836,000 kama gharama za matibabu zinazotokana na kuoza kwa makalio ya mwanaye zikijumuisha sindano,kuchonga nyama na kipimo cha CT-SCAN.

Mkurugenzi wa hopsitali hiyo inayoendeshwa na Shirika la Msamariamwema(GSF),Giliad Masenga amezungumza na Ndagullablog  na kukiri kumtambua mgonjwa huyo lakini hakutaka kuingia kwa undnai zaidi juu ya mlakamiko hayo na kumtaka mwandishi kuwasiliana na ofisa uhusiano wa Hospitali hiyo.

“Hilo jambo nalifahamu limeshafika ofisini kwetu na tumeshalifanyia kazi lakini nikuombe uwasiliane na ofisa uhusiano wetu yeye atalitolea ufafanunuzi zaidi”,amesema Masenga.

Akizungumza na Ndagullablog ofisini kwake,ofisa uhusiano wa hospital hiyo,Babriel Chisseo amekiri kuwepo kwa malalamiko ya baba mzazi wa majeruhi huyo nakwamba kwa sasa wanaangalia namna ya kuhakikisha anapona na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Amesema wakati huu hawana muda wa kulumbana na ndugu wa majeruhi huyo huku akikataa kuelezea kwa undani sakata hilo akidai kufaaya hivyo ni kwenda kinyume na maadili ya udaktari.

“Taarifa za mgonjwa ni siri baina yake na daktari anayemtibu hivyo hatuwezi kutoa taarifa za mgonjwa bila idhini yake vinginevyo anaweza akatushitaki”,amesema Chiseo.

Hata hivyo ofisa uhusiano huyo amesema kuwa,kama mzazi wa majeruhi huyo anaona hatendewi haki katika huduma anazopatiwa mtoto wake katika hospital hiyo,anayo hiari ya kumtoa na kumpeleka kwenye taasisi nyingine anayoamini itampa huduma nzuri.

Amesema hospitali ya KCMC ni taasisi ya dini inayoendeshwa kwa taratibu na sheria hivyo haiwezi kuendelea kulumbana na watu na kuacha kazi za kutoa huduma kwa wenye uhitaji.

“Mpaka mpaka sasa tunaona kabisa mgonjwa huyo anaanza kupata maendeleo mazuri kwenye afya yake tofauti na alivyoletwa hapa,madaktari wetu wanapambana usiku na mchana kuona Christian anapona na kurejea katika hali yake ya kawaida,kwa hiyo kwa sasa tunaomba tuwape muda madaktari waendelee na matibabu yake”,amesema.  

Daktari mmoja aliyezungumza na Ndagullablog bila kutaja jina lake,amesema kuwa tatizo hilo la majeruhi huyo kuoza makalio linatokana na kukaa muda mrefu bila kugeuzwa kutokana na Hospitali hiyo kutokuwa na vifaa maalumu ya kumgeuza mgonjwa mwenye tatizo kama hilo vikiwamo vitanda maalumu.

Amesema tatizo kama hilo humtokea mgonjwa yeyote hasa wanaopatwa na matatizo ya kuvunjika miguu kwani huchukua muda mrefu kitandani kwa kuwekewa mawe ambayo husaidia  miguu ya mgonjwa  kuunga taratibu kabla ya kuunga kabisa.
 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni