Baraka Leonard Nafari, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu(PhD) alifariki baada ya kugongwa na gari la teksi nje ya bweni la chuo kikuu februari 23 mwaka huu.
Maafisa wa shirika hilo wameandamana kwa pamoja na baadhi ya wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Johannesburg nje ya bweni kwa jina SophiaTown ambapo mwanafunzi huyo aligongwa na kuuawa.
Yalikua maandamano salama na watu walikusanyika kwenye uzio wa seng'enge pahala gari lilipo mgonga marehemu Baraka Nafari wakiwa wamebeba mabango yanayosema tunataka haki kwa Baraka, haki itendeke kwa Baraka.
Mshukiwa alikamatwa na polisi wa Afrika Kusini lakini baadaye akaachiliwa huru kwa dhamana.
Polisi walisema hakukuwa na ushahidi
wa kutosha wa kumfungulia mashtaka ya mauaji.
Badala yake, Mwandishi wetu Omar
Mutasa aliyeko Johannesburg anasema polisi walimfungulia mashtaka ya kuendesha
gari bila leseni.
Waandamanaji walitoa wito kwa polisi
mtuhumiwa arejeshwe korokoroni.
Waliweka shada la maua kwenye uzio
wa bweni la SophiaTown alipouawa Baraka.
Mkuu wa Africa Diaspora Forum Marc
Bafou ameitaka serikali ya Afrika Kusini na serikali ya Tanzania pamoja na
wakuu wa chuo kikuu cha Johannesburg mauaji haya wayape kipaumbele maana
yatazidi kukiaibisha chuo kikuu cha Johannesburg na taifa la Afrika Kusini,
mauaji yalioonekana kama chuki dhidi ya raia wa kigeni.
Africa Diaspora Forum imesema
Tanzania inafahamu fika gharama ya kumpata mwanafunzi mmoja aliyehitimu shahada
ya udaktari kwa hivyo serikali ya Tanzania isiliachie suala hili kwa wepesi.
Mwandishi wetu anasema marafiki zake
Baraka waliosoma naye na pia kufanya
kazi naye wamesema alikuwa mtu mzuri sana na hata mwanamke mmoja mweupe
alizungumza kwa Kiswahili na kusema watu waliomuua Baraka Nafari hawana utu
hata kidogo.
Wengine kutoka DRC walisema mauaji
haya ya Baraka sio tatizo la Afrika Kusini na Tanzania pekee yake lakini ni
tatizo la Jumuia ya SADC kulitatua kwa raia wanaotoka mataifa mengine ya SADC
wanaosoma katika vyuo vikuu vya Afrika Kusini .
Baadhi ya wanafunzi wanasema kuna
kanda ya video za usalama ambayo inamuonesha mwanafunzi huyo akikimbia na
mwanafunzi mwingine, nyuma wakiandamwa na watu wawili waliokuwa ndani ya gari
la teksi.
Gari hilo linaonekana kuwakimbiza na
hatimaye Baraka akagongwa mara kadha
akiwa kwenye uzio wa bweni.
Chanzo: BBC Swahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni