Na Kija Elias,Moshi.
WADAU wa mchezo wa mpira wa Magongo hapa nchini, wameiomba
serikali kupitia Wizara ya elimu kujenga viwanja vya mchezo huo kuanzia shule za msingi na sekondari ili kuweza kuibua
vipaji kwa wanafunzi kuanzia ngazi za awali.
Ombi hilo limetolewa na mjumbe wa chama cha mpira wa Magongo
Tanzania (Hockey), Nitu Singh Rehal mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe kwenye kikao cha wadau wa mchezo mkoa
wa kilimanjaro, kilichofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.
Alisema kujengwa kwa viwanja vya mpira wa magongo katika
shule nyingi nchini kutawezesha kuibua vipaji lukuki vya mchezo huo hatua
ambayo itawezesha kupata wachezaji bora ambao wataweza kuiwakilisha Tanzania kwenye
mashindani ya kimataifa.
“Mchezo wa magongo unakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba
wa viwanja vya kuchezea mchezo huo, hususani kwa wanafunzi wa shule za msingi
na sekondari, endapo vitajengwa viwanja vingi vya mchezo huu mashuleni tutaweza
kupata wachezaji wazuri ambao wataitangaza nchi yetu kimataifa,”alisema.
Mjumbe wa Chama cha mpira wa magongo Tanzania(Hockey).Nitu Singh Rehal akizungumza kwenye kikao cha wadau wa michezo klichoitishwa na Waziri mwenye dhamana na michezo,Dk.Harrison Mwakyembe hivi karibuni mjini Moshi.
Alisema kufundishwa kwa mchezo huo mashuleni kutawezesha
kuibua vipaji na kuwapeleka wanafunzi hao kuwashindanisha na wanafunzi wenzao
katika mikoa mbalimbali iliyopo hapa nchini.
Vile vile mjumbe huyo Nitu Singh Rehal aliiomba serikali kutazama
upya gharama za kodi kwenye vifaa vya michezo vinavyoingizwa nchini kama msaada
kutoka kwa wafadhili ili kuweza kuboresha michezo hapa nchini.
“Uwepo wa vifaa hivyo utawezesha kuzidi kuibua vipaji kwa
mpira wa magongo, kwani vinauzwa ghali sana, tutashukuru serikali endapo
itatupunguzia kodi ya uingizwaji wa vifaa vya michezo ili wanafunzi wetu waweze
kupenda kucheza mchezo huo,”alisema.
Aliongeza kuwa ili mwanafunzi aweze kuupenda na kujiunga na
mchezo huo wa magongo ni vyema serikali ikapunguza kodi ya vifaa hivyo na
kuweza kusambazwa kwenye mashule mengi.
“Changamoto kubwa hapa inayosababisha wanafunzi kushindwa
kuandaliwa katika mchezo wa magongo na kushindwa kuucheza mchezo huu wa magongo
ni ukosefu wa vifaa hivyo pamoja na viwanja vya kuchezea mchezo huo”alisema
Rehal.
Kwa upande wake Waziri wa habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe alisema kuwa serikali italifanyia kazi suala la
kodi kwa vifaa vya michezo nchini.
“Kwa sasa tupo katika maongezi na wenzetu wa Wizara ya fedha
ili kuhakikisha kwamba vifaa vya michezo vinaingia kwa gharama ndogo,”alisema
Waziri Mwakyembe.
Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo,Dkt.Harrison Mwakyembe(wa nne kutoka kushoto waliokaa)akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa michezo mara baada ya kikao chake na wadau hao hivi karibuni mjini Moshi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni