Jumatatu, 26 Machi 2018

WAFUNGWA UGANDA WAHITIMU SHAHADA YA SHERIA WAKIWA GEREZANI


   
 Pascal Kakuru,Suzzan Kigula na Moses Ekwam,wakipokea shahada za digree ya sheria huku wakiwa wamevalia sare nyeusi za kuhitimu .

Wafungwa watatu (pichani juu)waliosomea gerezani wamehitimu  shahada za digrii katika sheria, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wafungwa nchini Uganda kufuzu shahada ya uanasheria.

Mpango huo unaofanikishwa na Mradi wa wafungwa barani Afrika kwa ushirikiano na chuo kikuu cha London  unanuia kuwapa wafungwa fursa ya kushiriki kikamilifu katika taratibu za kutafuta haki.

Kuhitimu kwa watatu hao kutoka Gereza Kuu la Luzira kumetazamwa kama ishara ya mwamko mpya katika mfumo wa marekebisho magerezani Uganda.

Pascal Kakuru, Suzzan Kigula na Moses Ekwam walipokea shahada za digree huku wakiwa wamevalia sare nyeusi za kuhitimu.

Moses Ekwam mmoja wa waliohitimu alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano lakini alihudumu miaka minne baada ya kupatwa bila hatia.

Kwa miaka hiyo minne alipokuwa gerezani alianza kusomea somo la sheria na hivi sasa Ekwam ni mwendesha mashtaka wa jeshi la Uganda.

"Mimi nilikuja hapa nikaona mimi kukaa hapa kuangalia mpira niliona shule iko ndani kwa hivyo nikaamua kujiunga na shule A level nikapita vizuri 2010 hadi sasa hivi  niko wakili," aliambia BBC.
 


Mwenzake Pascal alikuwa akitumikia kifungo kwa makosa ya uhaini na hivi sasa anaelekea kumaliza kifungo chake baada ya kupata msamaha na sasa anasema analenga kutumia utaalamu wake katika sheria.

"Ninao mpango wa kuzungumzia wale watu wanaoteseka wale watoto, kinamama, wafungwa wakimbizi ni watu hodari sana huwezi kuwaongelea wawe kama wanaharakati watu kama hao.


Kutakuwa na ulimwengu vitu kadhaa vya watu kama hao kwa hivyo nina mpango wa kuwazungumzia mahali popote wapo si kwa nchi ya Uganda peke yake bali ulimwengu mzima popote nitakapopata nafasi ya kuwasaidia watu kama hao. "

Katika ripoti ya hivi karibuni Jarida la Afrika la masuala ya uhalifu na haki, idara ya magereza nchini Uganda imewekwa katika nafasi ya kwanza barani Afrika kwenye suala la mageuzi.

Hata hivyo bado kuna changamoto katika kuzingatia haki za wafungwa.
Owinyi Dollo ni naibu wa jaji mkuu nchini Uganda:

"Unaanza kujiuliza kweli kama hukumu ya kifo inapaswa kuwa katika sheria zetu, unahoji kwa sababu mtu ambaye alivunja sheria jana anaweza kubadirika na kuwa mtu mwenye ushawishi mwema leo.

Kwa kuhitimu wafungwa hao watatu wanafuata nyayo za rais wa zamani wa Afrika kusini Nelson Mandela aliyejiimarisha kitaaluma wakati akiwa gerezani jambo linalowapa matumaini wafungwa wengi na pia kuongeza mskumo wa mageuzi zaidi magerezani.

Nchini Kenya, wafungwa wamewahi kusomea sheria na kuhitimu na baadhi hata kuwasaidia wenzao kupata uhuru.

Peter Ouko, mmoja wao, kwa sasa ni balozi wa shirika la Africa Prisons Project.

Alikuwa amehukumiwa kifo na kuwa mfungwa kwa miaka kumi na minane kabla ya kupunguziwa kifungo na kuwa kifungo cha maisha na kisha kuachiliwa huru kwa msamaha wa rais,alipatikana na kosa la kumuua mkewe.       
 Wafungwa katika gereza Kuu la Luzira nchini Uganda akishuhudia wenzao wakitunukiwa vyeti baada ya kuhitimu shahada ya Sheria wakiwa grezani hivi karibuni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni