OKTOBA 22
mwaka huu ofisi ya Mrajis wa vyama vya ushirika nchini,iliitisha mkutano
mkuu maalumu wa wanachama wa chama kikuu cha ushirika mkoani Kilimanjaro(KNCU)ambao pamoja na mambo mengine mkutano huo ulijadili hoja za
ukaguzi.
Hatua ya kuitishwa kwa
mkutano huo mkuu maalumu ni kutokana na madai ya ofisi ya mrajis kwamba KNCU
imeshindwa kujibu hoja za mkaguzi wa nje katika misimu mitano ya
2008/2009 hadi 2012/2013 hivyo kushindwa kutoa huduma zake kikamilifu kwa wanachama
wake.
Kabla ya hoja hizo
hazijawasilishwa na kujadiliwa na wajumbe wa mkutano huo mkuu,mwenyekiti wa
bodi ya uongozi ya KNCU,Maynard Swai alitoa taarifa ya utetezi
kwa wajumbe hao .
Katika utetezi
huo,mwenyekiti huyo alishutumu vikali ofisi hiyo ya mrajis wa vyama vya
ushirika nchini na kudai ofisi hiyo ni kikwazo katika ustawi wa ushirika
kutokana na kuyumba katika utoaji wa maamuzi..
Mwenyekiti huyo alidai
kuwa,ofisi hiyo ya mrajis imekuwa ikitoa maamuzi tata ikiwamo kuzuia uuzwaji wa
shamba kubwa la kahawa la Gararagua ambalo chama hicho kililenga kuliuza ili
kuweza kulipa mkopo wa benki ya CRDB,madeni ya vyama vya msingi na kuimarisha
hali ya kifedha ya chama hicho.
Akadia kuwa,pamoja na
kuishirikisha ofisi hiyo katika mchakato mzima wa uuzwaji wa shamba hilo na
ofisi hiyo ya mrajis kutoa ruhusa ya kuuzwa kwa shamba hilo kwa barua ya machi
27 mwaka huu,ofisi hiyo ilisitisha uuzwaji wa shama hilo .
Kwa mujibu wa mwenyekiti
huyo,kitendo cha ofisi hiyo ya mrajis kuwa na maamuzi tata ni uvunjifu wa
sheria namba 6 ya ushirika ya mwaka 2013 kifungu cha 132(3) kinachoweka
bayana kuwa mtu yeyote anayekwaza au kuingilia shughuli za ushirika na
kuisababishia hasara atawajibika kwa hasara hiyo.
“Kwa tafsiri hii ya
sheria,kitendo cha kuchelewa kutoa maamuzi kwa mambo mbalimbali ambayo union
ilikwishapeleka ofisini kwake,kimeendelea kuisababishia hasara union”,ilisema
taarifa ya mwenyekiti huyo.
Kutokana na mkanganyiko
huo wa maamuzi ,chama hicho kinadai kuwa kitalazimika kulipa riba na
marejesho ya milioni 250 mapema mwezi huu baada ya mwezi mei mwaka
huu kulipa kiasi kama hicho .
Kuhusu hoja za ukaguzi
,mwenyekiti huyo alidai hoja hizo ni batili kwa mujibu wa kifungu cha 55(9) cha
sheria namba 6 ya ushirika ya mwaka 2013 kinachoweka wazi kuwa,hesabu
zikishawasilishwa na kujadiliwa na kisha kupitishwa na mkutano mkuu,uamuzi wao
dhidi ya hesabu hizo ni wa mwisho.
Kwa mujibu wa mwenyekiti
huyo hoja hizo zilikuwa batili kutokana na kuwasilishwa nje ya muda kama
sheria inavyotamka kwa vile ziliwasilishwa nje ya kipindi cha miezi sita
kama sheria inavyoagiza.
Shutuma hizo za KNCU
dhidi ya ofisi ya mrajis ni nzito na ambazo hazihitaji kufumbiwa macho na ofisi
hiyo ambayo ndiyo mhimili mkuu katika ustawi wa vyama vya ushirika nchini.
Ofisi hii ya mrajis pia
inalalamikiwa na KNCU kwa kushindwa kutatua mgogoro wa shamba la Lyamungo licha
ya aliyekuwa waziri wa ushirika ,George Kahama kuridhia kwamba
shamba hilo ni mali ya KNCU katika barua yake ya Oktoba 21 mwaka 2005.
Shamba hilo lenye ukubwa
wa ekari 112 limekaa kwa zaidi ya miaka kumi sasa tangu mwaka 2004 bila
kuwekezwa baada yak uwekewa pingamizi na hivyo kukikosesha chama hicho mapato
na licha ya kutolewa maamuzi na aliyekuwa mrajis wa vyama vya ushirika wakati huo,hadi
sasa limegeuka kuwa pori.
Katika mkutano huo
mkuu maalum,kundi la wanachama lililojitenga kufanya biashara na KNCU
lilipewa hadhi ya kutoa maamuzi ikiwamo kupiga kura kuamua kama uongozi wa bodi
ya chama hicho uendelee kuwapo madaraka ama la.
Hii ni ajabu ya
mwaka,kwamba watu ambao wameshajiondoa kwenye umoja na kuanzisha umoja
wao walioupa jina la G32 wanapewa hadhi ya kutoa maamuzi ya kuondoa
uongozi ambao hawakuuweka madarakani.
Kwa muda mrefu KNCU
imekuwa ikilalamikia hatua ya mrajis kutochukua hatua za kulifuta kundi hili
ambalo linafanya kazi kinyume na sheria ya ushirika inayokataza kuanzishwa kwa
chombo kingine kinachofanya biashara inayofanana na chombo kilichopo katika
eneo moja.
Kushindwa kwa ofisi
ya mrajis wa vyama vya ushirika kutoa maamuzi sahihi ikiwamo kufuta
usajili wa kundi la G32 linaloendesha biashara kinyume na sheria ya ushirika ni
kuzidi kuyapa nguvu malalamiko ya KNCU dhidi ya ofisi hiyo.
Haya ni baadhi tu ya
malalamiko ya KNCU dhidi ya ofisi ya mrajis wa vyama vya ushirika nchini hatua
ambayo inafifisha ile dhana ya ‘ushirika’ pamoja tunajenga uchumi.
Hakuna ubishi kwamba
ushirika kwa sasa umegubikwa na changamoto nyingi ikiwamo ufujaji wa fedha za
wakulima ambao umewafanya wakulima wengi kukata tama na kuamua kuachama na
ushirika na kujikita katika shughuli nyingine.
Kwa hali hiyo bila
kuwapo na jitihada kubwa za kuinua ushirika kwa msaada wa ofisi ya mrajis wa
vyama vya ushirika,hatutarajii muujiza kuuinua ushirika na kuwawezesha wakulima
kuboresha hali zao za maisha kupitia ushiika.
Kama ofisi ya mrajis
itakuwa kikwazo katika ustawi wa ushirika,ile dhana ya ‘ushirika’ tunajenga
uchumi haitaweza kufanikiwa na itabakia kuwa katika midomo ya watu pasipo
vitendo.
ZILIZOPITA