Jumatatu, 3 Novemba 2014

KNCU: OFISI YA MRAJIS VYAMA VYA USHIRIKA KIKWAZO


Chama  Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro(KNCU),kimeishutumu ofisi ya mrajis wa vyama vya ushirika nchini na kudai ofisi hiyo ni kikwazo katika ustawi  wa ushirika kutokana na kuyumba katika utoaji wa  maamuzi.
 DKT. AUDAX RUTABANZIBWA AKIZUNGUMZA KATIKA MKUTANO MKUU MAALUM WA KNCU, MJINI MOSHI

Shutuma hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na mwenyekiti wa chama hicho,Maynard Swai katika mkutano mkuu maalumu ulioitishwa na mrajis wa vyama vya ushirika nchini kujadili hoja za ukaguzi ambazo ofisi hiyo imedai chama hicho kimeshindwa kuzijibu kwa muda mrefu.

Mwenyekiti huyo alidaia kuwa,ofisi hiyo ya mrajis imekuwa ikitoa maamuzi tata ikiwamo kuzuia uuzwaji wa shamba kubwa la kahawa la Gararagua ambalo chama hicho kililenga kuliuza ili kuweza kulipa mkopo wa benki ya CRDB,madeni ya vyama vya msingi na kuimarisha hali ya kifedha ya chama hicho.

Alidai kuwa,pamoja na kuishirikisha ofisi hiyo katika mchakato mzima wa uuzwaji wa shamba hilo na ofisi hiyo ya mrajis kutoa ruhusa ya kuuzwa kwa shamba hilo kwa barua ya machi 27 mwaka huu,ofisi hiyo ilisitisha uuzwaji wa shama hilo .

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo,kitendo cha ofisi hiyo ya mrajis kuwa na maamuzi tata ni uvunjifu wa sheria namba 6  ya ushirika ya mwaka 2013 kifungu cha 132(3) kinachoweka bayana kuwa mtu yeyote anayekwaza au kuingilia shughuli za ushirika na kuisababishia hasara atawajibika kwa hasara hiyo.

Kutokana na mkanganyiko huo wa maamuzi ,chama hicho kimedai kuwa kitalazimika kulipa riba na marejesho  ya milioni 250 mapema mwezi ujao baada ya mwezi mei kufanya hivyo kwa kiwango kama hicho .

Akizungumzia hoja hizo,mwenyekiti huyo alidai kuwa,hoja hizo ni batili kwa mujibu wa kifungu cha 55(9) cha sheria namba 6 ya ushirika ya mwaka 2013 kinachoweka wazi kuwa,hesabu zikishawasilishwa na kujadiliwa na kisha kupitishwa na mkutano mkuu,uamuzi wao dhidi ya hesabu hizo ni wa mwisho na kwamba hoja hizo ni batili kutokana na kuwasilishwa nje ya muda kama sheria inavyotamka.

Kuhusu mgogoro wa shamba la Lyamungo,chama hicho kimedai kuwa,ofisi hiyo ya mrajis imeshindwa kutekeleza maagizo ya aliyekuwa waziri wa ushirika,George Kahama kwamba shamba hilo ni mali ya KNCU  katika barua yake ya Oktoba 21 mwaka 2005.

Chama hicho kimedai kuwa,pamoja na kuendelea kumkumbusha mrajis juu ya uamuzi huo wa waziri,hakuna hata barua moja iliyojibiwa huku shamba hilo likiendelea kukaa bila kuwanufaisha wanachama.
 WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA KNCU 2014

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni