Jumamosi, 23 Desemba 2017

BREAKING NEWS:MTUMISHI WA SHIRIKA LA UMMA AKAMATWA NA SHEHENA YA DAWA ZA KULEVYA



JESHI la polisi mkoani Kilimanjaro,linamshikilia mtumishi mmoja wa shirika moja la Umma mjini Moshi akituhumiwa kujihusisha na usafrishaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi.

Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro,Hamisi issah,amedhibitisha kukamatwa na kushikiliwa kwa mtumishi huyo ambaye kwa sasa tunahifadhi jina lake baada ya kukamatwa na shehena kubwa ya mirungi aliyokuwa akiisafrisha kwa kutumia gari lake dogo.

Mtumishi huyo alikamatwa desemba 19 mwaka huu nje kidogo ya mji wa Moshi baada ya gari lake kuparamia mti na kupata ajali akiwa katika jitihada za kuwakimbia polisi.

Kwa mujibu wa Kamanda Issah,dereva wa gari hilo alitimua mbio na kumwacha mtumishi huyo wa shirika la umma akitiwa mbaroni.

Taarifa zaidi pamoja na picha za mtuhumiwa huyo zitafuata hivi punde

Kwa taarifa juu ya mkasa huyo pamoja na majina kamili ya mtumishi huyo na taasisi anayofanyia kazi endelea kutembelea mtandao huu

Ijumaa, 22 Desemba 2017

TANZANIA KUJITATHIMINI MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA



Kila ifikapo Juni 25 ya  kila mwaka dunia inaadhimisha siku ya kupiga vita dawa za kulevya na kutathimini jitihada zilizofikiwa katika kupunguza tatizo la matumizi ya dawa hizi.  

Biashara ya dawa za kulevya ni tishio katika nchi mbalimbali duniani huku ikiathiri uchumi wa dunia kutokana na jitihada za kutokomeza kukabiliwa na changamoto nyingi. 

Pamoja na harakati za wadau katika  kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya imeshuhudiwa ongezeko kubwa la biashara hii haramu kutokana na kiasi kikubwa cha dawa  kinachokamatwa  na idadi ya watumiaji kuongezeka. 

Tume ya Kuratibu Uthibiti wa dawa za kulevya iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ndio iliyopewa jukumu la kuratibu masuala yote yanayohusu dawa haramu za kulevya hapa nchini, imefanya kazi nzuri ikishirikiana na vyombo vya dola hususani  kikosi kazi cha kupambana na dawa za kulevya. 
  
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2011 kilo 264.3 za dawa za kulevya aina ya heroin zilikamatwa ikilinganishwa  na kilo 185.8 zilizokamatwa mwaka 2010 ikiwa ni ongezeko la asilimia 42 la kiasi cha heroin kilichokamatwa  katika kipindi cha mwaka mmoja tu.

Kama hiyo haitoshi, mwaka huo huo kilo 126 za dawa za kulevya aina ya cocaine zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 63 zilizokamatwa mwaka 2010, ambapo ni ongezeko la asilimia 100.

Ongezeko hili ni kubwa na linaashiria kukuwa kwa biashara ya dawa za kulevya na kuwa upatikanaji wake ni rahisi huku  watumiaji wake wakiongezeka.

Ingawa hakuna takwimu sahihi za watumiaji wa dawa za kulevya katika nchi yetu lakini inakadiriwa takribani watu laki moja na nusu hadi laki tano wanatumia dawa hizo.
 Kati ya watumiaji hao wengi ni vijana ambao wameacha shule na kujiunga na makundi rika ambayo yana mitandao na wauzaji wa dawa hizo.

 Lakini hali ngumu ya kimaisha ambayo watanzania wengi wanapitia nayo ni kichocheo kingine cha kukua kwa biashara hii.

Athari zaidi za matumizi ya dawa za kulevya inaonekana katika afya za watu ambapo wakati huu watu wengi wanakumbwa na maradhi ya moyo, ini, mapafu, meno, figo, umbo, ngozi, maradhi ya akili, kansa, ugumba, kuzaa watoto wafu.

Pia huwafanya watumiaji kuwa tegemezi kwa ndugu, uteja, kusababisha au kupata ajali na wakati mwingine hata vifo.
Taarifa za tume ya kuratibu uthibiti wa dawa za kulevya zinaonyesha katika kipindi cha mwaka 2011 jumla ya watumiaji 4,684 wa dawa za kulevya walihudumiwa katika vituo vya afya vya manispaa na majiji nchini.

Pia takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwezi Desemba 2011 wajidunga  heroin wapatao 250 walikuwa wakipatiwa tiba katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 

Idadi hii ni kubwa na inaathiri nguvu kazi ya taifa kwa sababu matatizo ya kiafya yanayotokana na dawa za kulevya huwafanya watumiaji kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo hivyo kurudisha nyuma jitihada za serikali kuboresha maisha ya wananchi.

Kutokana athari za kiafya za matumizi ya dawa za kulevya idadi ya wagonjwa wa akili inaongezeka na kuleta mtafaruku katika familia nyingi kwa sababu watumiaji wakipatwa na maradhi yatokanayo na dawa za kulevya huwa tegemezi na kuzidisha umaskini.

Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nayo yanachochewa na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kushirikiana sindano kwa wale wanaojidunga  na kufanya ngono zisizo salama.

Hata wale waliokwisha ambukizwa VVU wanapoendelea kutumia dawa za kulevya kinga yao hushuka haraka zaidi na kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa nyemelezi kama vile homa ya ini, kifua kikuu, kaswende na kisosono.   

Katika utafiti uliofanyika mkoani Dar es salaam mwaka 2006 ulionyesha kuwa asilimia 42 ya wajidungao walikuwa wamepata maambukizi ya VVU. 

Utafiti mwingine kwa wajidunga wilaya ya Temeke mwaka 2010 uliofannywa na Asasi ya Medicine Du Monde uligundua asilimia 34.8 ya wanaojidunga heroin waligundulika na VVU, wengine asilimia 27.7 waligundulika  na virusi vya homa ya ini.

Biashara  na matumizi ya dawa ya kulevya  huvuruga mfumo wa maisha ya jamii ikiwa ni pamoja na mmomonyoka wa maadili. Kutokana na kuiga kwa tamaduni za kigeni kupitia vyombo vya habari watu wamebadili mfumo wa kuishi na kuacha tamaduni za jamii.  

 Jitihada hizo bado hazijafanikiwa kwa sababu biashara hiyo haramu inaongezeka na hili limedhihirika kwa  kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kinachokamatwa kila mwaka.

Tabia hizi zimesababisha vijana wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya ambapo huambatana na unyang’anyi, ngono zembe hivyo kujenga jamii isiyo na mwelekeo mzuri wa maendeleo.

Matukio ya kigaidi utekaji nyara  na vita vya wenyewe kwa wenyewe au vita kati ya serikali na magenge ya  wafanyabiashara wa dawa za kulevya inachochewa zaidi na matumizi yaliyokithiri ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana, hivyo kuhatarisha usalama wa nchi na kujenga jamii isiyo na amani na utulivu.

 Chanzo:fikrapevu.com

Alhamisi, 21 Desemba 2017

TAKUKURU YAFUNGA MWAKA KWA KISHINDO,YAPANDISHA VIGOGO SABA KORTINI KWA UFISADI NDANI YA SIKU TATU




NA CHARLES NDAGULLA,HAI

TAASISI  ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Kilimanjaro(TAKUKURU) imetoa onyo kwa watumishi wa umma kuacha kuchezea fedha za serikali na atakayejaribu ataishia pabaya ikiwamo kufikishwa makahamani.

Onyo hili la Takukuru linakuja siku chache baada ya kuwafikisha makahamani watumishi saba wa Halmashauri ya wilaya ya Hai kwa tuhuma za kujihusisha na ufujaji wa fedha za umma.

“Takukuru tunasisitiza kuwa hakuna mbadhilifu wa fedha za umma mkoani Kilimanjaro atakayeabaki salama,ni suala la muda tu,hivyo ni rai yetu kuwa wenye fikra za kufanya ubadhilifu ni bora wakaacha mara moja na kujifunza kiridhika na vipato vyao halali au wakaacha kazi za umma wakatafute kazi zenye maslahi wanayodhani yatakidhi matamanio yao “,ni onyo la Mkuu wa takukuru,Holle Makungu

Watumishi hao wameshitakiwa kwa makosa ambayo yanafanana ya wizi na ubadhilifu na baadhi yao wamejikuta wakiburuzwa mahamani mara tatu kwa makosa hayo hayo ya ufujaji wa fedha za umma.

Aliyeanza kuonja joto ya jiwe ni Thadeus Theobald Meela ambaye alikuwa mweka hazi wa halmashauri hiyo wakati wa ufujaji wa fedha hizo kabla ya kuhamishiwa wilaya ya Ruangwa na baadaye Pangani mkoa wa Tanga.

Meela alijikuta akiunganishwa tena katika mashitaka ya wizi na ubadhilifu wa fedha hizo za umma  na Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu ,Melkizedeck  Oscar Humbe pamoja na karani wa fedha,Valentina Elisha Mollel .

Watatu hawa wameshitakiwa kwa kosa la wizi na ubadhilifu wa zaidi ya shilingi Milioni 27wanaodaiwa kuufanya mwaka 2014 wakati huo Humbe akiwa Mkuregenzi wa halmashauri hiyo.

Takukuru katika kuonyesha haitanii,safari hii imemfikisha mahakamani Mganga mkuu wa Hospital ya Mkoa wa Kigoma(RMO) Dkt. Paul Christopher Chaote akishitakiwa na wenzake watano kwa makosa 109 ya ubadhilifu wa fedha wa zaidi ya shilingi Milioni 38  na kusaidia kutendeka kwa kosa pamoja na kuandaa nyaraka za uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri.

Wengine ni Philipo Alexander Masasi,Thadeus Theobald Meela,Christopher Nyamagera Manzi,Edwid Mtalemwa Kalokola na Valentina Elisha Mollel ambao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya oktoba 2014 na januari 2015. 

Walifikishwa mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Hai,Arnold Kirekiano na kusomewa mashitka na waendesha mashitaka wa Takukuru,Rehema Mteta akisaidiana na Suzan Kimaro. 

Wanadaiwa kwa matumizi mabaya ya nyaraka ikiwamo kuandaa nyaraka za uongozi kwa lengo la kumdanganya mwajiri,ubadhilifu  na kusaidia kutenda makosa ambako wanadaiwa kutumbua kiasi hicho cha fedha zilizokuwa kwa ajili ya posho ya kuitwa kazini kwa madaktari(on Call allowance) katika hospital ya Machame .


Kwa mujibu wa hati ya mashitaka,washitakiwa hao wenaidaiwa kuwa,mnamo Oktoba mwaka 2014  kwa pamoja wakiwa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya hai, kwa njia za udanganyifu walijimilikisha kiasi cha sh,Milioni 19.200,000 zilizokuwa kwa ajili ya posho ya kuitwa kazini kwa madaktari na wauguzi katika Hospital ya Machame.

Baada ya washitakiwa hao kuzitafuna fedha hizo ndipo walipoandaa nyaraka mbali mbali kuonyesha kuwa fedha hizo zililipwa kwa madaktari na wauguzi wa Hospital hiyo ya Machame kama posho ya kuitwa kazini kwa madaktari hao na wauguzi jambo ambalo halikuwa kweli . 

Baada ya kusomewa mashitaka hayo,washitakiwa Paul Chaote, Thadeus Meela, Valentina Molle na Christopher  Manzi walikana mashitaka yao  huku washitakiwa wengine wawili,Phillipo Alexander Masasi na Edwin Mtalemwa Kalokola wakiingia mitini .

Washitakiwa hao wapo nje kwa dhamana hadi Februari 15 mwaka 2018 kesi yoa itakapokuja kwa ajili ya kutajwa  baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosai bondi ya milioni 5, kila mmoja.



KIWANDA CHA BANANA CHA D.G.T MOSHI KATIKA KASHFA


 Na Charles Ndagulla,Moshi

MAMLAKA  ya Chakula la Dawa(TFDA)Kanda ya kaskazini,imekifunga kiwanda cha kutengeneza pombe aina ya Banna inayotengenezwa na Kampuni ya Derrick Global Trading(D.G.T ) cha  mjini moshi kutoka na kubainika kuwa na kasoro .

Kiwanda hicho kimefungwa chini ya kifungu cha 181 sura ya 209 ya sheria ya chakula na dawa ya mwaka 2003 kutokana na tuhuma za kutumia nembo ya kiwanda kingine cha kutengeneza pombe kali kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari kiwandani hapo,Mkaguzi wa chakula mwandamizi kutoka TFDA Kanda ya kaskazini,William Mhina,alisema sababu nyingine za  kufungwa kwa kiwanda hicho ni mazingira yasiyoridhisha ya kiwanda hicho.

Alitaja sababu zingine ni wafanyakazi kutokuwa na vyeti vya kuonyesha afya zao huku wafanyakazi hasa wa kike kutokuvaa kofia kichwani.

Alisema uchunguzi wao umebaini kuwa,eneo la kuoshea chupa ni chafu na kwamba chupa hizo zimekuwa zikioshwa katika mazingira yasiyoridhisha.

Alisema wamiliki wa kiwanda hicho wamepewa muda wa kurekebisha kasoro hizo na baada ya kufanya hivyo TFDA itafanya ukaguzi tena kujiridhisha kama kasoro hizo zimefanyiwa kazi,

Katika hatua nyingine,jeshi la polisi kwa kushirkiana na maofisa wa mamlaka ya mapato Tanzania(TRA),wamefanikiwa kukamata shehena ya vifungashio  vinavyotumiwa na kampuni moja mkoani Shinyanga  ya Canon General Supply inayojihusisha na utengenezaji wa pombe kali aina ya Shujaa.

Vifungashio hivyo vilikamatwa ndani ya kiwanda hicho kilichopo eneo la Kwa Alphone kata ya Kiborironi  huku baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho wakishikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi.

Akizungumzia tukio hilo,ofisa huyo kutoka TFDA alisema hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria inayosimamia usajili wa bidhaa na kuongeza kuwa,vifungashio vilivyokamatwa ndani ya kiwanda hicho havimo kwenye orodha ya usajili wa bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo.


 Moja ya vifungashio vilivyokamatwa na polisi katika kiwanda cha D.G.T cha mjini Moshi,vifungahio hivyo ni mali ya Kampuni ya Canon General Supply ya mjini Shinyanga.

 Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro,Hamisi Issah alisema jeshi hilo linamshikilia meneja wa Kiwanda hicho aliyemtaja kwa jina la Boniface Damas(56) pamoja na wafanyakazi watatu wa kiwanda hicho.
Kamanda Issah aliwataja wafanyakazi hao kuwani Severine Pantaleo(37),Riziki Fabian (28) na Daniel Japhet(18) ambao wanadaiwa kukutwa na pombve kali iliyofungashwa kwenye viroba iana ya Zed inayodaiwa kutengenezwa kienyeji.

“Viroba hivyo vina alama zake,lakini watuhumiwa hawa walikuwa wakitengeneza katika mfumo wanaoujua wenyewe,utengenezaji wa pombe usiozingatia taratibu ni hatari na unaweza kuleta madhara makubwa kwa wanywaji”,alisema kama Issah.

Kuhusu vifungashio vilivyokamatwa ndani ya kiwanda cha D.G.T,kamanda Issah alisema kuwa,wamiliki wa kiwanda hicho hawakuwa na haki stahiki ya kutengeneza pombe hizo kutokana na kutengeneza pombe hizo pasipo kuzungitia tararibu za kisheria.

Kamanda Issah amesema polisi kwa kushirikiana na TFDA wanafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo ikiwamo matumizi ya malighafi isiyo ya kiwanda hicho na uchunguzi ukimalika shweria itachukua mkondo wake kwa watakaobainika kutenda makosa.
 
 Meneja wa Kiwanda cha Derrick Global Trading(D.G.T) cha mjini Moshi,Boniface Damas(kulia)akiwa ndani ya gari la polisi na watuhumiwa wenzake baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kutengeza pombe kali kwa kutumia vifungashio vya kampuni ya Canon General Supply ya mjini Shinyanga kinyume cha sheria.

Jumanne, 19 Desemba 2017

MKURUGENZI HALMASHAURI YA MJI WA BARIADI KIZIMBANI MOSHI



VIGOGO watatu waliokuwa watumishi katika Halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro,wameburuzwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka manne yakiwamo ya kughushi nyaraka,wizi na ubadhilifu wa fedha za umma.

Walioburuzwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Melkizedeck Humbe ,aliyekuwa mweka hazina wa halmashauri hiyo,Thadeus Meela na aliyekuwa karani wa fedha wa Halmashauri hiyo,Valentina Mollel.

Kabla ya kuhamishiwa mkoani Simiyu,Humbe alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai na Meela alikuwa mweka hazina kabla ya kumishiwa wilaya ya Ruangwa  na baadaye wilaya ya Pangani mkoani Tanga.

Walifikishwa mbele ya hakimu mfawidhi mahakama ya wilaya ya Hai,Arnold Kirekiano na kusomewa mashitaka na wakili na mwendesha mashitaka wa Takukuru,Suzan Kimaro.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo ,washitakiwa hao wameshitakwia kwa makosa ya wizi na ubadhilifu wa fedha wa zaidi ya shilingi Milioni 27. 

Washitakiwa hao wanadaiwa kuandaa nyaraka za uongoza malipo ya   mishahara kwenda Hazina wakiomba fedha za mishahara huku wakitambua kuwa wameingiza majina ya watumishi hewa waliokuwa wamekwisha kuacha kazi katika Halmashauri ya Hai kwa sababu mbalimbali. 

Mwendesha mashitaka huyo wa takukuru aliiambia mahakama kuwa, baada ya kutumiwa fedha hizo waliandaa nyaraka za malipo (payment voucher), yenye namba 2015-000204 ya  Julai 08 mwaka 2014, na madokezo kumdanganya mwajiri kwa kuonyesha kuwa fedha hizo wanazirejesha kwa Katibu mkuu Hazina kama ulivyo utaratibu wa mishahara isiyo na wenyewe.

Pamoja na nyaraka hizo kuonyesha wanarejesha fedha hizo Hazina, waliandaa hundi ya wazi iliyowawezesha kuchukua fedha taslimu milioni 27.44, toka kwenye akaunti ya Halmashauri ya Hai iliyoko Benki ya NMB tawi la Hai na kuzifanyia matumizi binafsi kinyume na sheria.

Washitakiwa walikana mashitaka yao na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika na watakaosaini bodi ya shilini Milioni Tano kila mmoja.

Upande wa mashitaka uliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na washitakIwa hao watarejea tena mahakamani hapo Februari 15 mwaka 2018 ambako watasomewa maelezo ya awali ya kosa.

 Hata hivyo,furaha ya kuachiliwa kwa dhamana kwa washitakiwa wawili,Thadeus Meela na Valentina Mollel ilifutika baada ya kujikuta wakikamtwa tena na maofisa wa Takukuru. 

Baada ya kukamatwa walipelekwa moja kwa moja ofisi za takukuru wilaya ya Hai na taarifa za baadae zimedai kuwa,wawili hao wamepelekwa mahabusu na watafikishwa tena mahakamani desemba 21 mwaka huu kwa tuhuma ziongine za ubadhilifu wa fedha za Halmashauri hiyo.

Katika hatua nyingine , Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu alizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhairishwa kwa kesi hiyo na kutoa  onyo kwa watumishi wa umma ambao wanaendekeza ubadhirifu kupitia nyadhifa walizokabidhiwa wataendelea kuwakamata mmoja baada ya mwingine. 

Makungu ameonya kuwa, Taasisi yake itawasaka watumishi wote waliotenda makosa ya ubadhilifu wa fedha za serikali kokote waliko bila kujali walitenda makosa hayo wakati gani.

“Nirudie tena kutoa wito kwa wananchi wenye taarifa za ubadhirifu, ufisadi na uhujumu uchumi bila kujali kama ni za muda mrefu watuletee kwa kuwa makosa ya jinai huwa hayana ukomo” alisema Makungu.