Jumamosi, 6 Januari 2018

USINDANGANYIKE,BIASHARA YOYOTE INALIPA MHIMU NI KUZITAMBUA FURSA



Ukipata nafasi ya kufika kule *Mbozi, Mbeya* ukakutana na habari za watu wanaotajirika kutokana na *kilimo cha kahawa*, kwa kweli unaweza kuwehuka, na kujiona kama mtu uliyechelewa kweli kweli.

Wakati unarudi, kama ukishuka MAFINGA, NJOMBE na kufuatilia stori na kutazama mamilionea walioupata umilionea kutokana na BIASHRA ya MITI na MBAO unaweza kudhani kwamba hapa duniani fursa inayowatoa watu kiuharaka ni mbao pekee!

Pitia maeneo ya RUAHA MBUYUNI, IRINGA kutana na WAHEHE wakulima wa NYANYA na VITUNGUU wakikuonesha coaster walizonunua kwa kilimo cha msimu mmoja pekee. Aisee kama una akiba utanunua shamba muda huo huo na kuachana na ajira kama ulikuwa mwajiriwa.

Ukitoka pale ukaenda mpaka MANG'ULA na IFAKARA,MOROGORO, ukakutana na habari za watu wanavyopiga hela kwenye MPUNGA kichwa chako kinaweza kuwaka moto. Unaweza kujizaba vibao na kujimaindi, baadae  utajiuliza, "Nilikua wapi siku, zote hizi?"

Ukitoka kule jisogeze mdogo mdogo hadi KARIAKOO,DAR kisha kutana na wafanyabiashara wa maduka pale ambao wana gepu la kufuata bidhaa kule China, Uingereza na Dubai.

 Utapigwa na butwaa utakapoona watu wakiongelea milioni mia tatu, milioni mia saba, bilioni mbili kama vile wanaongelea elfu kumi kumi.

Usipokua na utulivu unaweza kuamini kwamba biashara zinazolipa ni maduka na unaweza kuanza kufight kupata fremu pale!

Usiende kwanza Zanzibar, bali chukua hata bus au Fastjet uende chapchap kule ARUSHA Hapo kutana na stori za mabilionea wa madini wanaotikisa jiji.

Ukisimuliwa ABC za madini na namna ya kucheza nayo, unaweza kuacha kila kitu na kuanza kuhangaika na biashara ya madini. Hapo sijakutajia jeuri utakayoiona kwa watu wanaofanya biashara ya utalii. Nakwambia hela ulizozisikia Kariakoo utaziona ni cha mtoto sana!

Unapoendelea kutafakari, rudi mtandaoni. Kama ukibahatika kukutana na watu wanaoitwa NETWORK MARKETING utakoma kuchagua. Wakikuelezea stori zao, wakikusimulia walivyonunua mavouge yao, wakikuonesha picha zao walizokua wanakula bata *DUBAI,PARIS,MADAGASCAR na UAMERIKANI*, nakwambia korosho utaziona takataka.

Mbao utazihesabu kama biashara ya utumwa, maduka ya Kariakoo utayaona kama michosho na mipunga ya Ifakara utaiona kama madudu flani ya walugaluga waliochelewa! Sasa mara kumi hata ya Network Marketing wa bidhaa, usiombe ukutane na fursa ya digital currency, hakika nakwambia utatembea kifua mbele ukiamini kutajirika ni ishu ya kufumba na kufumbua.

Hapo sijaamua kusafiri na wewe kwenda kwa wale tunaokinadi kilimo kama dhahabu inayoelea.

Ukisikiliza wafuasi wa kilimo, ukasikiliza hesabu wanazokupatia unaweza kusema wanaohangaika na madini wanapoteza muda! Ngoja niuchune kukupeleka kwenye fursa ya samaki kuzitoa Mwanza kupeleka Congo, ngoja nisikurushe roho na habari ya korosho, ngoja nikaushie habari ya ufuta!

KUNA MAMBO MATANO YA KUFAHAMU:

1.Usipokua na utulivu wa fikra, hizi habari za fursa za biashara na ujasiriamali zinaweza kugeuka kuwa kama miluzi mingi, na itakupoteza.

2.Mtu yeyote asikudanganye ya kwamba kuna biashara bora kuliko nyingine. Kila biashara, fursa unayoiona huku duniani inao uwezo wa kutengeneza matajiri.

Kuna matajiri kutokana na kumiliki shule, wengine kwa kumiliki mabasi, wengine kwa kuwa na vituo vya mafuta, wengine kwa kilimo, wengine kwa udalali n.k.

Usisahau kuwa biashara inayomtajirisha mmoja, mwingine akiingia ndio inaweza kumfilisi na kumpoteza kabisa! Kawaulize waliolizwa kwenye kilimo, watakusimulia.

3.Mtu yeyote asikuchanganye na miluzi yake hata ukaamini kwamba kuna fursa inayoweza kumfaa kila mtu.

Sio kila fursa inayompa faida John inaweza kukupa faida wewe Ashura. Ukifuatilia kwa umakini utabaini kwamba mafanikio hayakai katika uzuri wa fursa, bali yanatokana na mchukua fursa.

Mwingine anaweza kujifunza na kumudu kuifanya network
marketing, lakini mwingine nature ya network marketing haimfai, isipokua akienda kule Mafinga akazamia kwenye mbao, mwaka mmoja mbali unaona ana Semitrela zake mbili na mambo yanaenda.

Kuna watu wanapotea kiuchumi kwa kung'ang'ana na fursa kwa kukariri. Kisa kuna mtu alinunua Range Rover katika network marketing na wewe unaendelea kukomaa, mwaka wa tano sasa hata bodaboda huna, kumbe ungeenda zako Mbozi kwenye Kahawa sasa hivi usikute na nyumba ungekua umejenga.

Kisa wanaoenda China wanatoka na wewe unahangaika na biashara za maduka, mwaka wa ishirini bado hakujasomeka na kumbe ungeenda zako kwenye madini huko Mererani muda huu ungekua umeshanunua helkopta yako!

4.Ni kweli kwamba inatakiwa tujifunze fursa mbalimbali, lakini ifike sehemu mtu uchague kukomaa na fursa fulani pasipo kurukaruka.

Utajiri hauji kwa mtu kuwa bize na kila fursa inayoingia, bali unakuja kwa kujifunza fursa nyingi na ku-stick na eneo moja, ama maeneo machache ambayo, utajitambulisha nayo na watu watakutambua.

Na ukishakua katika kukomaa na maeneo yako (fursa ulizoamua kukomaa nazo), usianze tena kuyumbayumba na kutamani ya wengine.

5 .Lazima ifike mahali utambue kwamba kila mtu anahitaji fedha za kutosha lakini hatuhitaji kiwango sawa cha fedha kwa sababu makusudi na malengo yetu hayafanani.

 Nikisema hivi, sikushauri uhangaike na fursa kwa motive ya hela pekee, bali ufanye vitu kama sehemu ya kuufurahia mchakato wa kazi, na fedha ziwe ni matokeo na sio lengo namba moja
Fursa zipo nyingi kuwa makini katika maamuzi.

NAWATAKIENI HERI YA MWAKA MPYA


ALIYECHUNGUZA MADINI YA TANZANITE AULA,ATEULIWA KUWA NAIBU WAZIRI WA MADINI


Alhamisi, 4 Januari 2018

BREAKING NEWS: HATIMAYE MTUMISHI WA P P F APANDA KIZIMBANI KWA DAWA ZA KULEVYA,APELEKWA MAGEREZA



Na Charles Ndagulla,Moshi.

HAYAWI HAYAWI YAMEKUWA,baada ya kusota mahabusu kwa siku 17,hatimaye mtumishi wa mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa (PPF),Anitha Osward Ichwekeleza(32),anayetuhumiwa kujihusisha na usafrishaji wa dawa za kulevya,amefikishwa mahakamani mjini moshi.

Mtumishi huyo wa umma,alikamatwa desemba 19 mwaka jana akiwa na shehena ya madawa ya kulevya aina ya mirungi aliyokuwa akiisafrisha kwa kutumia gari lake dogo aina ya Toyota Sienta lenye namba za usjaili T674DLB.

Anitha alifikishwa katika makahama ya hakimu mkazi mjini Moshi chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto akitokea kituo cha polisi Majengo mjini hapa ambako kwa muda wote tangu akamatwe alikuwa akishikiliwa huko.

Baada ya kufikishwa hapo alishikiliwa kwa muda nje ya mahakama kabla ya kupandishwa kizimbani na kusomewa shitaka moja la uhujumu uchumi mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi,Aidan Mwilapwa.

Alisomewa shitaka hilo na wakili wa serikali Agatha Pima na kutokana na shitaka hilo kuwa ni la uhujumu uchumi na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya aina hiyo hadi mahakama kuu,mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote.

Mshitakiwa huyo ambaye kwenye hati ya mashitaka ametambulishwa kama mtumishi wa umma,ameshitakiwa kwa kosa moja la kusafrisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 15(b) cha sheria namba 5 ya mwaka 2015  ya udhibiti wa usafrishaji wa dawa za kulevya kama ilivyofanyiwa marejeo madogo na sheria namba 23 ya mwaka 2016.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka,mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa,mnamo desemba 19 mwaka jana huku Majengo kwa Mtei Manispaa ya Moshi,mshitakiwa alikutwa akisafrisha kilo 216.37 za dawa za kulevya.

  Baada ya kusomewa shitaka hilo,mshitakiwa huyo alipelekwa mahabusu katika Gereza Kuu la Mkoa,la Karanga ambako sasa ameenda kuanza maisha mapya ya gerezani,shauri hilo litakuja kwa ajili ya kutajwa tena mahakamani hapo Januari 19 mwaka huu.


HIVI NDIVYO ALIVYONASWA NA SHEHENA YA DAWA ZA KULEVYA

 Anitha alikamatwa na askari wa jeshi la polisi waliokuwa doria baada ya kupenyezewa taarifa na raia wema kuwa mtumishi huyo wa umma alikuwa amebeba ‘mzigo’ akitumia gari lake binafsi ambalo kulingana na sheria,kama atapatikana na hatia,gari hilo litataifishwa na serikali .

“Askari wakiwa doria walimkamata Anitha Oswald, ambaye ni mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370”, alisema kamanda Issa. 

Kamanda Issa alisema Anitha Oswald alikamatwa eneo la Majengo kwa Mtei Disemba 19, mwaka jana, akiwa anatokea Njia Panda ya Himo kuchukua mzigo huo. 

Aidha kamanda Issa alisema kwamba usafirishaji wa dawa za kulevya bado ni changamoto kubwa ambapo alielezea kusikitishwa na tabia ya baadhi ya watumishi wa Umma kujihusisha na usafirishaji huo.

“Jeshi la polisi mkoani hapa liko makini, operesheni inaendelea na hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kujihusisha na biashara hii”, alisema.
Hata hivyo kamanda aliongeza kusema kwamba jeshi hilo la polisi mkoani kilimanjaro, bado linaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo, ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza gari alilokuwa akiliendesha baada ya kugonga mti katika jitihada za kuwakimbia polisi. 

 PICHA MBALI MBALI ZIKIMUONYESHA ANITHA OSWARD ALIVYONASWA NA DAWA ZA KULEVYA
 Mtuhumiwa wa dawa za kulevya,Anitha Osward(32)akiwa chini ya ulinzi wa polisi huku akiwa amesimama mbele ya gari lake aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674DLB huku shehena ya dawa za kulevya ikiwa ndani ya gari lake.
 Shehena ya dawa za kulevya iliyokamatwa na polisi mjini moshi ikisafrishwa na mtumishi wa mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma(PPF),Anitha Osward,tayari mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani .
 Gari la mtuhumiwa wa dawa za kulevya Anitha Osward aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB likivutwa baada ya kugonga mti katika jitihada za mtuhumiwa huyo kuwakimbia polisi.
 gari aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB linalomilikiwa na mtumishi wa mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma(PPF)Anitha Osward likiwa limesheheni shehena ya dawa za kulevya.

MTOTO WA NDESAMBURO AWAPOZA WALIMU,WAFUNGWA MIAKA MITATU



Na Charles Ndagulla,Moshi

MAHAKAMA ya hakimu mkazi mjini Moshi,imewahukumu kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela walimu wawili wa shule ya Msingi ya Mwereni iliyopo wilaya ya Hai baada ya kukutwa na hatia ya kuhamisha umiliki wa shamba la shule isivyo halali.



Hukumu hiyo imetolewa januari 3 mwaka huu na kaimu hakimu mfawidhi  wa mahakama hiyo,Aidan Mwilapwa  baada ya kuwatia hatiani washitakiwa hao .



Walimu waliotiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo hicho ni Mwalimu mkuu wa shule hiyo,Onesmo Ernest Kinyaiya na mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo,Apolinary Denke Pantaleo.

Shamba hilo lilitolewa na walimu hao  kwa mtoto wa Marehemu Philemon Ndesamburo aitwaye Tomm ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Rahisi General Marchant Ltd ambayo ni kampuni tanzu ya makampuni ya Rahisi Group ya mjini Moshi.



Walimu hao walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka na waendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru),Barry Galinoma akisaidiana na Furahini Kibanga.



Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa makahamani hapo na waendesha mashitaka hao wa Takukuru,wlimu hao walishitakiwa kwa kosa la kuhamisha umiliki wa shamba la shule hiyo kwenda kwa kampuni ya Rahisi General Marchant Ltd bila idhini ya kamishna wa Ardhi.



Kulingana na hati hiyo ya mashitaka,walimu hao hawakuwa na mamlaka hayo kwa mujibu wa kifungu cha 17(5) cha sheria ya ardhi ya vijijini sura ya 14 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.



Hivyo  uhamishaji huo ulikuwa kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 hivyo mahakama hiyo kuwatia hatiani katika shauri hilo la jinai namba 3 la mwaka 2016.



Katika hukumu hiyo,walimu hao walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au faini ya shilingi laki tano na baada ya mahakama kuwatia hatiani walimu hao walinusurika kwenda jela baada ya ndugu walikuwa wamefurika mahakanai hapo kuchangishana fedha na kuwalipia faini.



Baada ya hukumu hiyo,Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(Takukuru) mkoani Kilimanjaro,imetoa taarifa kupitia kwa Mkuu wa Taasisi hiyo mkoani hapa,Holle Makungu kuwa itafuatilia kwa mwajiri wa walimu hao ili kuhakikisha wanaondolewa kwenye utumishi wa umma.





KARANI MAHAKAMA YA MWANZO  MBARONI KWA RUSHWA YA LAKI MOJA.



Katika tukio jingine,mtego ulioandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru),umefanikiwa kumnasa karani mmoja wa mahakama ya Mwanzo iliyopo Maili Sita wilaya ya Hai .



Karani huyo,Rose Jonathan Urassa(58),alinaswa na Takukuru baada ya kudai rushwa ya shilingi laki moja ili amsaidie mshitakiwa katika shauri la jinai namba 69/2017 kupitia kwa hakimu anayesikiliza shauri hilo.



Taarifa ya Takukuru mkoani Kilimanjaro iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Januari 4 na kusainiwa na Mkuu wa Takukuru mkoa(RBC),Holle Makungu imeeleza kuwa,karani huyo aliomba fedha hizo ili hakimu anayesikiliza shauri hilo aweze kutoa hukumu ya upendeleo kwa mshitakiwa.



“Baada ya taarifa hizo kupokelewa,mtego wa rushwa uliandaliwa na aliweza kukamatwa januari 3 mwaka huu akiwa amepokea fedha hizo katika eneo hilo  la mahakama ya mwanzo,Hai,Rose atafikishwa mahakamani mara uchunguzi utakapokamilika”,imesema taarifa hiyo.



Takukuru imetoa  onyo kwa baadhi ya makarani na wahudumu wa mahakama wanaoendekeza tabia ya kuomba na kupokea rushwa kwa kisingizio cha kutumwa na waheshimiwa mahakimu wabadili tabia hiyo.



Kamanda Makungu katika taarifa yake hiyo kwa vyombo vya habari,ametoa rai kwa makarani na wahudumu wa mahakama katika mkoa wa Kilimanjaro wanaoendelea  na tabia hiyo mwisho wao wa  kufanyakazi katika utumishi wa umma kwa mwaka huu 2018 utakuwa mwisho wao.



Pia alitoa wito kwa wananchi wanaodaiwa rushwa na baadhi ya makarani na wahudumu wa mahakama kwa kisingizio cha  kutumwa na waheshimiwa mahakimu,watoe taarifa kwa taasisi hiyo ili iweze kuboresha mahakama kwa kuwaondoa wachache wanochafua sura za mahakama.


URAIA WA MCHUNGAJI WA KANISA LA YESU ANAWEZA MOSHI UTATA


Na Charles Ndagulla,Moshi.

MCHUNGAJI Zakaria Donald Yona wa Kanisa la Yesu Anaweza Centre ameingia matatani akituhumiwa kuishi nchini isvvyo halali  baada ya kudaiwa kuwa ni raia wa Kenya.

Uchunguzi wa mtandao huu  umebaini kuwa,mchungaji huyo ni raia wa Kenya kwa kuzaliwa lakini mwenyewe amekana tuhuma hizo na kudai  ni mtanzania kwa kuzaliwa.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo mtandao wa NdagullaBlog umeziona zinaonyesha kuwa,mchungaji huyo anayeendesha kanisa lake eneo la Mji Mpya Manispaa ya Moshi,alizaliwa mwaka 1964  eneo la Siaya mkoa wa Nyanza nchini Kenya.

Kulingana na nyaraka hizo,baada ya kuzaliwa alipewa cheti chenye namba ya ingizo 4300247/85  akitambuliwa kwa majina ya Donald Oloo Waswani huku pia akiwa na kadi ya utaifa wa Kenya yenye namba 237104963 iliyotolewa Oktoba 10 mwaka 2013.

Pia mke wa mchungaji huyo anayetumia majina ya Redempter William Francis kwa hapa nchini,uchunguzi umebaini kuwa alizaliwa mwaka 1970 huko Machakos nchini Kenya huku akiwa na kadi ya uraia wa nchi hiyo yenye namba 223854431 iliyotolewa mwaka 2007.

Uchunguzi zaidi  umebaini kuwa,mchungaji huyo amesajiliwa kama mlipa kodi na mamlaka ya mapato nchini Kenya(KRA) na kupewa namba ya utamburisho wa mlipa kodi(Personal Identification Number) Na A.010329470.

Mchungaji huyo na mkewe Redempter William Francis,wanadaiwa kufunga ndoa yao Oktoba 13 mwaka 1991 katika Kanisa la Dandora Gaspel Tabernacle na kupewa cheti chenye namba 465369.

Hata hivyo mchungaji huyo amezungumza na NdagullaBlog  na kutupilia mbali tuhuma hizo lakini akishindwa kuweka wazi ni wapi  alipozaliwa akidai wakati ukifika ataweka wazi kila kitu.

“Suala la mimi nimezaliwa wapi tutakuja kuliweka sawa lakini kwa ufupi mimi ni mtanzania kwa kuzaliwa na hayo mengine yote yatajulikana huko mbele ya safari”,alisema .

Wakati mchungaji huyo akikwepa kuweka wazi alikozaliwa,NdagullaBlog imefanikiwa kuona nyaraka mbalimbali baadhi zikidaiwa ni za kughushi zikionyesha mchuangaji huyo alizaliwa Nyamagana mkoani mwanza mwaka 1964.

Kwa mujibu wa cheti cha kuzaliwa kilichosajiliwa Machi 15 mwaka 2010,kinaonyesha mchungaji huyo alizawali eneo hilo na kusajiliwa kwa jina la Zacharia Donald Yona Munuo.

Pia mkewe ambaye kwenye cheti cha kuzaliwa nchini Kenya anatumia majina ya Redempter Ndinda Nthenge,kwenye cheti cha kuzaliwa hapa nchini anatambulika kwa majina ya Dedempter William Francis Munuo akidai alizaliwa Nyamagana mkoani Mwanza mwaka 1969.

Wawili hao pia wanadaiwa kufunga ndoa ya kiserikali mkoani Kilimanjaro Juni 13 mwaka 2007 na kupewa cheti  B/N na.0748488 hali ambayo inazidisha utata zaidi juu ya uraia wa wawili hao.

Mchungaji huyo amekiri kuwahi kukamatwa yeye na familia yake yote na maofisa wa jeshi la uhamiaji mkoani Kilimanjaro na kufikishwa makahamani akidaiwa kuishi nchini isivyo halali.

“Tulikamatwa juni 20 mwaka jana na wakatushikilia kwa siku mbili na baadaye wakatupeleka mahakamani,madai yao ni kwamba mimi na familia yangu si raia wa Tanzania bali ni raia wa Kenya”,amedai.

Amedai kuwa,uhamiaji walidai kuwa wangepeleka mashahidi 15 na vielelezo zaidi ya 20 kudhibitisha kuwa mchungaji huyo si raia wa Tanzania lakini hawakufanya hivyo.

Hata hivyo mchungaji huyo amesema kuwa,uhamiaji waliondoa shauri hilo mahakamani  desemba 6 mwaka jana baada ya kudai upande wa jamhuri hauna nia tena ya kuendelea kuwashitaki.

Mchungaji huyo amedai kuwa,wakati wakiamini suala hilo limeisha na wako huru kuendelea na maisha yao,walijikuta wakikamatwa tena nje ya mahakama na kupelekwa ofisi za uhamiaji .

Kwa mujibu wa mchungaji huyo,baada ya kufikishwa katika ofisi hizo walilazimishwa kusaini nyaraka za kuondolewa nchini na walipokataa kusaini nyaraka hizo waliondolewa nchini kwa nguvu na kupelekwa mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Holili.

“Tulipofika holili maofisa wa uhamiaji wa Kenya walikataa kutupokea baada ya uhamiaji Tanzania kukosa nyaraka mhimu kuonyesha sisi hatutakiwi Tanzania zikiwamo nyaraka za mahakama”,amesema.

Mchungaji huyo amesema kuwa  baada ya zoezi hilo kugonga mwamba,maofisa hao wa uhamiaji waliamua kuwatelekeza mpakani na kuondoka kabla ya mchungaji huyo na familia yake kuamua kurejea  nyumbani kwa kutumia usafiri mbadala.

Msemaji wa uhamiaji mkoani Kilimanjaro(DCI),Albert Rwelamila amedhibitisha kuwepo na uchunguzi unaofanywa na ofisi yake juu ya uhalali wa uraia wa mchungaji huyo na familia yake alipozungumza na NdagullaBlog hivi karibuni.

Hata hivyo,Rwelamila hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo kwa undani zaidi kwa kile alichodai lipo zuio la mahakama kuu linalowataka kusitisha mchakato huo hadi hapo suala hilo litakapotolewa uamuzi.

“Ni mhimu tukaheshimu zuio la mahakama maana ni chombo cha kisheria nadhani baada ya kusikiliza pande zote na kutoa uamuzi hapo tunaweza kuwa na cha kusema,kwa sasa tuliache kwanza”,alisema.

NdagullaBlog imeambiwa kuwa,zuio hilo limewekwa baada ya mchungaji huyo kukimbilia mahakama kuu desemba 15 mwaka jana kupitia kwa wakili wake Caessar  Shayo.

Kwa upande wake wakili Shayo amesema kuwa  hati ya zuio ilitolewa desemba 18 mwaka jana na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi,Aishiel Sumari.