Jumatano, 17 Desemba 2014

JAJI WEREMA AJIUZULU KWA KASHFA YA ESKROW, IKULU YABARIKI

 
M
wanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Jaji Frederick Werema amejiuzulu nafasi yake hiyo kuanzia jana, Jumanne, kufuatia sakata la uchotaji wa fedha kutoka akaunti ya ESCROW ambapo zaidi ya dola milioni 120 zilihamishwa.

Mwanasheria mkuu, pamoja na baadhi ya wanasiasa na maafisa waandamizi wa serikali walituhumiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, imesema Rais Jakaya Kikwete alikubali ombi hilo la kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali.

Katika barua yake kwa Rais Kikwete, Jaji Werema alisema ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na umechafua hali ya hewa. 

Rais Kikwete amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu.

Itakumbukwa kwamba sakata la Akaunti ya Escrow liliibuliwa bungeni na mmoja wa wabunge wa bunge la Tanzania, David Kafulila na kusababisha mjadala mkali na kuamua Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kupewa jukumu la kuchunguza kashfa hiyo.

Baada ya uchunguzi kuwasilishwa katika mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni mwa mwezi Novemba, kamati hiyo ilikuja na maazimio manane kuhusu taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya IPTL.

Miongoni mwa maazimio ya bunge yaliwataja baadhi ya wanasiasa, mwanasheria mkuu, maafisa waandamizi wa serikali, majaji, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kuhusika katika kashfa hii na hivyo kuagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria wahusika na wengine kuondolewa katika nyadhifa zao za kuteuliwa.



GARI LA BENKI YA NMB LAKAMATWA KWA AMRI YA MAHAKAMA

G
ari aina ya Toyota LandCruiser lenye namba za usajili T394BVJ,linashikiliwa na Kampuni ya udalali ya Independent Agencies ya mjini hapa ili kurejesha fedha za mteja wa benki hiyo sh,Milioni 15,500,000 aliyeuziwa shamba na nyumba iliyopo katika mgogoro wa kifamilia.

Benki hiyo kupitia kampuni ya Udalali ya Mwafrica Group LTD inadaiwa kumuuzia nyumba  mteja huyo,Efrem Isaack Joseph  iliyopo katika kijiji cha Mdawi kata ya Kimochi wilaya ya Moshi vijijini may 18 mwaka huu  huku ikifahamu kuwa eneo hilo linao mgogoro.

Uamuzi wa kukamatwa mali za benki hiyo ili kurejesha fedha hizo ulitolewa wiki iiyopita mjini hapa na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Nyumba wilaya ya Moshi,Muhelele Sukumba baada ya kukubaliana na madai ya mteja huyo kupitia kwa wakili wake David Shilatu .

Mteja huyo alifungua shauri  katika baraza hilo  akidai kutapeliwa na benki hiyo baada ya kumuuzia shamba lenye mgogoro huku akiiomba mahakama ya usuluhishi wa masuala ya Ardhi na Nyumba kuiamuru benki hiyo kumrejeshea fedha zake ama kumkabidhi mali yake huku pia akitaka alipwe fidia .

Hatua hiyo ilitokana na benki hiyo kumpa mkopo mteja wake  Adam Gard Moshi wa sh,Milioni na kuweka dhamana eneo hilo ambalo baadaye wazazi wake walijitokeza na kupinga uuzwaji wa shamba hilo kwa madai kuwa si mali ya mdeni wa benki hiyo.

Familia hiyo nayo ilifungua shauri katika baraza hilo kupinga uuzwaji wa shamba hilo na nyumba ambako baada ya ushahidi kuwasilishwa mbele ya baraza hilo,uuzwaj huo ulitenguliwa na shamba hilo kurejeshwa mikononi mwa familia.

Kutokana na kuwapo kwa mgogoro huo,benki hiyo ilishindwa kumkabidhi mteja huyo eneo hilo na hivyo kulazimika kuomba msaada wa kisheria kupata haki yake kutokana na kutishiwa  usalama wake muda mfupi baada ya maofisa wa benki hiyo kwenda kumkabidhi eneo hilo.

Kwa upande wake meneja wa NMB tawi la Nelson Mandela mjini hapa,Emmanuel Bushiri alikiri kukamatwa kwa gari hilo alipozungumza na blog hii mwishoni mwa wiki na kuongeza kuwa hilo lilitokana na baraza kujiridhisha kuwa taratibu za mnada zilikiukwa.

Alitaja baadhi ya taratibu zilizokiukwa na kampuni ya udalali ya Mwafrica kuwa ni pamoja na kutolipa kodi manispaa,kutoshirikishwa viongozi wa serikali ya Kijiji cha Mdawi pamoja na familia ya mdaiwa aliyekopeshwa na benki hiyo.

Jumanne, 16 Desemba 2014

THIERRY HENRY ASTAAFU SOKA



Mshambuliaji wa zamani wa Ufaransa Thierry Henry amestaafu kandanda la kulipwa baada ya miongo miwili na sasa atakuwa mchambuzi wa kandanda kwenye televisheni ya Sky Sports nchini Uingereza.

Henry (Anri) mwenye umri wa miaka 37, alishinda Kombe la dunia na la Ulaya akiichezea timu ya taifa ya Ufaransa, na pia ndiye mfungaji wa magoli mengi zaidi katika klabu ya Arsenal kwenye Ligi Kuu ya England akiwa na mabao 226 katika mechi 370.

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger alisema hivi karibuni kuwa Henry "bila shaka" atajiunga tena na klabu hiyo katika wadhifa mwingine katika siku  za usoni.


BENKI YA USHIRIKA K’NJARO YACHUNGULIA KABURI

Benki kuu ya Tanzania(BoT) imesitisha baadhi ya huduma za biashara kwa benki ya Ushirika Kilimanjaro(KCBL) kutokona na mtaji wa benki hiyo kuwa chini ya sh, bilioni 2  na hivyo kuwa  katika hatari ya kukosa sifa kwa mujibu wa sheria ya  benki kuu ya mwaka 2006.

Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi iliyowasilishwa katika mkutano mkuu wa 20 wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika hivi karibuni mjini hapa inaonyesha kuwa,kwa sasa benki hiyo ina mtaji  wa sh,Milioni 195,111,000 tu hali ambayo wakaguzi hao wameonya kuwa inaweza kuathiri uwepo wa benki hiyo.

Aidha taarifa hiyo imeonya kuwa,mikopo inayotolewa kwa wateja imekuwa hairejeshwi kila  mwezi kwa  mujibu wa mikataba iliyowekwa hali iliyopelekea kufutwa kwa mikopo mibaya yenye thamani ya sh,Milioni 255,611,441 kwenye vitabu baada ya kupata kibali kutoka bodi ya uongozi.

Wakati kiasi hicho kikubwa cha fedha kikufutwa,benki hiyo ilifanikiwa kukusanya kiasi kidogo cha fedha cha sh,Milioni 62.073,000 huku taarifa hiyo ya ukaguzi ikigundua kuwapo kwa tengo la ziada la mikopo mibaya la sh,33,740,683 likipitishwa kwenye vitabu.       

Taarifa hiyo ya ukaguzi imeendelea kufichua kuwa,kuongezeka kwa matumizi yasiyo na riba kunachangia benki kutokuendelea vizuri na kusababisha hasara ya sh,milioni 343,260,000 katika mwaka husika na kuongeza jumla ya  hasara kutoka sh,Bilioni  1.169,834,000  mwaka 2012    hadi sh,Bilioni 1.513,094,000 mwaka jana.

Hata hivyo menejimenti ya benki hiyo imejibu hoja hizo za ukaguzi na kuelezea kuwa itaongeza biashara kwa sh,Bilioni 1.5 ambayo itazalisha mapato ya sh,Milioni 150 ili kuongeza faida bila kuonyesha mchanganuo jinsi itakavyoongeza biashara hiyo.

Katika hatua nyingine,benki hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha inarejesha mabilioni ya shilingi yaliyotolewa na benki hiyo kwa wateja mbalimbali kama mikopo kutokana na kuwapo na mwitikio mdogo katika ujereshaji wake.              
Taarifa ya meneja wa benki hiyo,Elizabert Makwabe kwa mkutano mkuu wa wanahisa hao imeeleza kuwa,hadi kufikia septemba 30 mwaka huu jumla ya sh,Bilioni 4.333,036,114 zilikuwa zimetolewa kama mikopo kwa wateja mbalimbali.

Inaeleza kuwa aslimia 63.3 ya mikopo hiyo ilielekezwa katika sekta ya kilimo ambayo ni kiasi cha sh,Bilioni 2.758,217,111 na kwamba ni sh,Milioni 370,258,855 tu zilizokuwa zimekusanywa katika kipindi cha kuanzia januari hadi septemba mwaka huu.

Meneja huyo amelalamika kuwa,baadhi ya wateja wanatumia njia mbalimbali ili wachelewe kulipa na wakati mwingine wanatumia kauli za matusi pale inapolazimika madeni  yasiyolipwa yakusanywe.

Alitoa wito kwa wale wote ambao hawajarejesha au marejesho yao hayaendi vizuri,kuchukua hatua za makusudi na kulipa madeni yao na kwamba bila kufanya hivyo benki italazimika kutenga matengo kwa ajili ya madeni mabaya hali itakayoathiri mtaji wa benki hiyo.

Ijumaa, 12 Desemba 2014

MOTO WATEKETEZA MADUKA 6, BASI LA ABIRIA; MOSHI



Mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 zimeteketea kwa moto yakiwemo maduka sita na basi dogo la abiria lililokuwa gereji kwa ajili ya matengenezo katika tukio lililotokea mjini Moshi hapa mkoani Kilimanjaro.

Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea katika mtaa wa Bakwata-Sido katika Manispaa ya Moshi walisema moto ulianza majira ya saa 6:30 usiku wa kuamkia leo, ukianzia katika kibanda cha kuchaji betri za magari.

“Kuna kibanda cha kuchaji betri za magari katika gereji ya vijana ambako betri zilikuwa zikichajiwa humo ambako shoti ya umeme ilitokea na kulikuwa na oil zilizokuwa zimetapakaa chini hivyo cheche za moto ziliruka na kusababisha mlipuko huu,” alisema shuhuda mmoja.

Mmiliki wa mojawapo ya maduka aliyetambulisha kwa jina la Justo Elias Mboho alisema taarifa za kulipuka kwa maduka katika mtaa ulio na shughuli nyingi za ufundi magari na uuzaji wa mitungi ya gesi alizipata usiku na kwamba kila kitu kimeteketea kwa moto.

“Sikuwa na jinsi nilipoambiwa kwamba mali zote zimeteketea kwa moto hivyo nikaona hakuna haja ya usiku huo kuja katika eneo la tukio hadi asubuhi ambako kila kitu kimeteketea… mali zenye thamani ya shilingi milioni 5 katika duka langu zimeteketea zote,” alisema Mboho.

Aidha mmiliki mwingine aliyejifahamika kwa jina la Living Mrema alisema duka lake lilikuwa na vifaa vyenye thamani ya  shilingi milioni 20 viliteketea kwa moto na kuongeza kwamba kwa ujumla wa maduka yote sita zaidi ya shilingi milioni 90 zimeteketea kwa moto.

Katika tukio hilo mashuhuda waliongeza kusema gari la zimamoto la Manispaa ya Moshi liliishiwa maji hivyo kuomba msaada wa zimamoto ya Kiwanda cha Sukari (TPC) ambao walifika na kuambulia kuzima moto tu kutokana na umbali hadi eneo la tukio.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Korongoni, Said Mwamba alilitupia lawama Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, kikosi cha Zimamoto-Kilimanjaro na Manispaa ya Moshi kutokana na uzembe wa matukio kadhaa ya moto.

“Niliamshwa usiku na vijana kwamba moto unawake katika mtaa wa Bakwata-Sido, nikapiga simu jeshi la polisi simu zilikuwa zikiita bila kupokelewa na nyingine kuzimwa kinyume na maadili ya kazi yenyewe, zimamoto nao waliishiwa maji huku Manispaa nilishawaambia mapema kwamba uuzwaji wa gesi katika eneo hili ambalo ni makazi ya watu ni hatari,” alisema Diwani Mwamba

Diwani huyo aliongeza kuwa chanzo ni mrundikano  wa vifaa vya gereji ya karibu (Vijana Garage) bila kufanyiwa usafi na kuwekwa kwa utaratibu  hali ambayo ingeweza kuleta maafa zaidi katika eneo hilo.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
CHANZO: JAIZMELALEO